Jinsi ya kuepuka kuwa usichotaka kuwa

Jinsi ya kuepuka kuwa usichotaka kuwa

GoldDhahabu

JF-Expert Member
Joined
Apr 29, 2023
Posts
7,189
Reaction score
10,375
Aliposikia hilo kwenye runinga, aliamua kujaribisha kuona kitakachotokea.

Mada iliyokuwa ikiendelea kwenye TV ilihusiana na Elimu nafsi, kwa jina jingine, Saikolojia.

Mtoa mada alitahadharisha kuwa ni hatari kuwaambia watoto wasifanye kitu fulani, kwani inakuwa kama wamechochewa kufanya walichokatazwa.

Huyo baba, kwa kutaka kulithibitisha hilo, alienda nje na kuzunguka nyuma ya nyumba ambako mtoto wake na watoto waajirani zake walikuwa wakicheza. Umri wao ulikuwa wa wastani wa miaka tisa hivi.

Alipowaita, aliwaambia wacheze wanavyotaka, na wafanye cho chote watakachokipenda, isipokuwa tu wahakikishe hawautemei mate mti uliokuwa nyuma ya nyumba.

Watoto waliitikia, kuonesha kukubali kufuata amri waliyopewa.

Huyo baba aliporudi ndani, alijibanza dirishani kufuatilia mwenendo wao wakicheza.

Muda ulipita, na kila mmoja alicheza kwa furahi, lakini wakiwa makini wasifanye kinyume na walivyoelekezwa.

Lakini kujizuia huko kulikuwa ni kwa muda tu!

Hatimaye, alijitokeza mmoja aliyedhubutu, na akafanikiwa kufanya kinyume na agizo walilopewa.

Aliangalia kulia na kushoto, na alipoona hakuna anayemtazama, akautemea mate.

Mwingine naye alifanya vivyo hivyo. Ilifikia hatua wakawa wanashindana kuutemea mate huo mti. Katika kundi zima , ni watoto watatu tu ndiyo waliofanikiwa kujizuia kuutemea mate huo mti. Asilimia kubwa waliutemea.

Kwa nini ilikuwa hivyo? Nitakuambia!

Kama ulishawahi kusoma Biblia, utakumbukua habari ya wana wa Israel, jinsi walivyoamrishwa kutokuiabudu sanamu. Walifanya hivyo?

Muda mfupi baadaye, walifanya yayo hayo walichokatazwa. Walichonga sanamu ya ndama na kuiabudu.

Fikiri, mtu amekulia katika maisha ya taabu kwa sababu ya ulevi wa wazazi wake, na kutokana na mateso hayo, akaapa kutokuonja pombe maishani mwake, lakini katika utu uzima wake, akaishia kuwa mlevi kuwazidi wazazi wake..

Kuna watu wanaouchukia sana umaskini, lakini kadiri chuki inavyoongezeka, ndivyo umaskini unavyoshamiri.

Kuna wazazi waliowausia watoto wao kuepuka ngono mpaka watakapoingia kwenye ndoa, lakini wakaishia kubebesha na kubebeshwa ujauzito wangali shuleni.

Kwa nini imakuwa hivyo? Ni kwa sababu siyo wasikivu?

Jibu linaweza likawa ni kwa sababu walikuwa wakijitahidi kutokufanya tofauti na walivyoagizwa!

Akili ni kama camera. Kuchukia kitu fulani ni sawa na umeielekeza camera yako huko. Vivyo hivyo na kuwa na shauku ya kufanya kitu.

Wale watoto walipoambiwa wasiutemee mti mate, picha ya wao wakiutemea mate ilimea ndani yao. Ilipokua kwa kiwango kikubwa, hawakuweza kuendelea kujizuia tena

Kuwakataza watoto kufanya jambo fulani inaweza ikawa si njia sahihi sana. Kama kuna namna nyingine, hasa ya kuwajengea shauku kubwa ya kutaka kufanya kitu sahihi, ni vizuri zaidi. Misamiati ya "usifanye" hivi na vile inapaswa kuwa michache sana, kama haiwezekani kuufikisha ujumbe bila ya kukitumia. Inayopaswa kutawala ni misamiati ya "kufanya"

Unataka labda wafanye vizuri darasani? Usiwatishe kuwa wasiposoma kwa bidii watafeli na kuishia kuwa maskini. Siyo wote wanaweza kulipokea hilo kiusahihi. Kwa wengine inakuwa kama umewaloga kimasomo.

Badala yake, wajengee shauku ya kufaulu kwa kuwaeleza raha na faida zitokanzao na kufaulu.

Unataka wasijihusishe na ngono wangali wanasoma? Wajengee shauku ya kuona faida ya hilo.

Unajua, kitu pekee kitakachomfanya mtu afanye kitu anachotakiwa kukifanya, ni yeye kuamua kufanya. Badala ya kuwaamrisha, "wauzie" wazo lako, walione kuwa ni la kwao na si la mzazi wao.

Na hata kama ni wewe binafsi, usijenge taswira ya usichokitaka.

Kama unataka, kwa mfano, kuondokana na hali duni, jenga taswira njema akilini mwako, ya mafanikio. Taswira ya mafanikio ikiimeza taswira ya umaskini, kutaweza kusaidia jitihada zako za kutafuta mafanikio kuzaa matunda mema.

Usipambane na hali usiyoitaka. Kazana kuijenga taswira sahihi huku ukiendelea kufanya matendo sahihi.

Kama ni mwanafunzi uliyebatizwa jina la "kilaza", na unataka kuaondokana na hiyo fedheha, fanya yafuatayo.

1. Iruhusu fikra chanya itawale ufahamu wako. Jijengee picha ya mwanafunzi mwenye mafanikio.

2. Endelea kusoma kwa bidii. Muda sio mrefu, utaanza kuyaona matokeo ya jitihada zako.

Nilishawahi kufanya hayo.

Nilipokuwa shule ya Msingi, almanusura ningeacha shule kabisa. Ufaulu wangu ulikuwa wa chini sana. Ilifikia hatua nikawa naiona shule ni mateso.

Nilipobadilisha mtazamo, na kuanza kuisaka namba moja, kidogo kidogo, nilipanda na hatimaye, kabla ya kuhitimu darasa la saba, nilijikuta mimi ndiye ninayeongoza kitaaluma darasani kwetu.

Akili yako inahitaji kujengewa taswira chanya ili ikusaidie kupata matokeo mazuri.

Kama inawezekana, epuka kuongea kauli zinazoweza kujenga taswira hasi akilini mwako.

Sema unayoyataka.
Ona unayoyataka.
Waza unayoyataka.

Lakini wakati huo huo, ukiyafanya yakupasayo.

Utafanikiwa!!!
 
Barikiwa sana, kuna nafsi itaokoka kupitia bandiko hili
 
Nitakuuliza swali kwa mfano nimenunua sumu ya panya nyumbani je nitumie kauli gani kumkataza mtoto wangu ili asiionje????
 
Back
Top Bottom