JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 685
- 1,124
Kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika kuzuia na kupambana na rushwa kwa kufanya yafuatayo;
Kutoa taarifa
Kila mwananchi ana jukumu la kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa TAKUKURU au kwa vyombo vingine vya sheria au dola. Taarifa zinaweza kutolewa kwa njia ya simu, barua, barua pepe au kufikisha taarifa hizo katika ofisi ya TAKUKURU Makao Makuu au ofisi zilizopo mkoani na wilayani kote nchini.
Kutoa ushahidi
Kutoa tu taarifa bila kuwa tayari kutoa ushahidi hakutasaidia kuwachukulia hatua za kisheria wala rushwa. Hivyo wewe mwananchi una jukumu la kuwa tayari kutoa ushahidi wa vitendo vya rushwa ulivyoshuhudia katika Mahakama au popote pale unapohitajika kufanya hivyo.
Kutoa elimu
Mwananchi yeyote una jukumu la kumuelimisha mwananchi mwenzako kuhusiana na suala la rushwa na athari zake kwake yeye na jamii kwa ujumla. Kwa kufanya hivyo utakuwa umesaidia mwananchi huyo kuepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Kuacha rushwa.
Mwananchi unatakiwa kuichukia rushwa na kuepuka kushiriki vitendo vya rushwa. Rushwa ni kikwazo kikubwa kwa demokrasia, utawala bora, haki za binadamu na ni tishio kwa amani, utulivu na usalama katika jamii. Wewe ndiye unayeathirika zaidi katika kila tendo la rushwa unaloshiriki, hivyo AMKA, ACHA RUSHWA!
Kutii sheria
Mwananchi, ni lazima uishi kwa kutii sheria, kanuni na taratibu za nchi pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali za kuzuia na kupambana na rushwa. Mwananchi unatakiwa kubadili mawazo na mtazamo kwamba mapambano dhidi ya rushwa ni ya TAKUKURU au vyombo fulani peke yake.
Upvote
1