SoC02 Jiwe la Msingi 5.2: Wanafunzi kuelewa wanachojifunza

SoC02 Jiwe la Msingi 5.2: Wanafunzi kuelewa wanachojifunza

Stories of Change - 2022 Competition

onea 22

Member
Joined
Jul 31, 2020
Posts
34
Reaction score
20
Wanafunzi kuelewa wanachojifunza.

Mnamo mwaka 2011, nilikuwa miongoni mwa wanafunzi 80 tuliokuwa tukisoma masomo ya sayansi katika shule fulani ya sekondari mkoani Tabora. Sikuwa miongoni mwa wanafunzi bora katika darasa lile.

Na wala sikuwa muulizaji sana wa maswali. Inawezekana hiyo ilikuwa ni moja ya sababu za kutofanya vizuri kwangu kwa kipindi kile. Siku moja tulikuwa katika kipindi cha Fizikia. Mwalimu alikuwa akielezea jinsi kanuni mbalimbali zilivyopatikana (alikuwa ana derive formulas) kwenye mada ya thermodynamics.

Ilipita kama saa moja zima nikiwa sielewi kinachoendelea mle ndani. Mwalimu akachora magrafu mengi ubaoni na kuanza kuyaelezea, pia sikuwa naelewa kilichokuwa kinaelezewa. Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu ya shuleni pale nilijikuta nikiomba poo na kunyoosha mkono juu.

Sikuwa na swali gumu sana siku ile lakini kwa bahati mbaya swali lile sikupewa jibu lake hadi leo. Sikumbuki swali kamili lakini nilichokuwa nakimaanisha kwa siku ile ni kwamba hao waliochora hayo magrafu walikuwa katika mazingira gani?

Au kwa maana nyingine nilitaka anipe mfano wa mazingira ambayo yananizunguka ili tuweze kuelewa vizuri zaidi somo lake. Nilichokuja kukigungua ni kwamba hata mwalimu hakuwa anafahamu kwa vitendo kitu alichokuwa anatufundisha.

Mfano huu ni sawa na wa fundi mkuu na fundi msaidizi wawe wanatengeneza jengo. Wakati wanaendelea kujenga yule saidia fundi akawa haelewi wanajenga kitu gani. Wanendelea tu kupandisha kuta, hakuna madirisha hakuna milango yaani bora mnajenga tu.

Yule saidia fundi alipochoshwa na ile hali na kuamua kumuuliza fundi wake tunajenga kitu gani hapa? Jibu la fundi mkuu liwe kwamba, “we kila siku tunajenga halafu leo hii uwe haujui tunajenga nini?”

Sasa bora saidia fundi hatakuja kuambiwa atolee maelezo kitu walichokitengeneza siku ya kukabidhi kazi, ila kwa wanafunzi wao ndio watakaokuja kutahiniwa kwenye mtihani na mwalimu hatakuwepo siku hiyo.

Miaka mingi imepita tangu tukio hilo kunitokea, na liliniachia funzo zuri tu kichwani mwangu ambalo siku moja ningependa wanafunzi wote walifahamu. Mwaka 2017 kulitokea tukio jingine ambalo ni tofauti na lile la kwanza, lakini yana uhusiano mkubwa sana kwenye somo ambalo ningependa tujifunze.

Nilikuwa namuelekeza mwanafunzi wa darasa la saba somo la Hisabati. Katika kufundishana nilimuuliza kanuni ya kutafuta eneo la duara lenye kipenyo kizima, akanijibu kuwa ni πd2/4. Nikamwambia vizuri, je pai ni nini? Na d ni nini? Yule mwanafunzi hakuwa na uelewa wa mambo hayo.

Ikabidi nianze kumwelezea historia ya pai na ugunduzi alioufanya, nikamwambia kwamba alichokigundua pai ni kwamba kwenye mduara wowote ule ulimwenguni, ukichukua urefu wa mzunguko wa duara ukigawanya kwa kipenyo chake basi jibu lake ni moja kwa miduara yote (3.1428571).

Yule mwanafunzi alitaharuki kidogo na nikaona udadisi ukiongezeka kwa yule mwanafunzi ikafikia kipindi akaniambia tuanze kupima vitu mbalimbali vya duara mle ndani ili tuhakikishe kama alichogundua pai ni kweli au kitabu kinatudanganya tu?

Tukaacha kusoma kwenye makaratasi tukachukua tape measure na kuanza kupima vitu mle ndani. Vilikuwa ni vitu vyenye ukubwa tofauti lakini tulipotafuta huo uwiano wa mzingo na kipenyo kwa miduara tuliyoipima hatukupata jibu kamili la 3.13428571, lakini yote yalikuwa kati ya 3.1 na 3.4.

Nikamwambia kwamba hiyo tofauti iliyojitokeza ni kutokana na makosa ya upimaji na tukaelewana. Kitu ambacho nilimwambia mwanafunzi wangu na ningependa wanafunzi wote wawe nacho ni kwamba wasikubali kusoma bila kujua umuhimu wa elimu wanayosoma au kama hawajui umuhimu basi waelewe angalau wajue historia ya hivyo vitu wanavyosoma.

Ni imani yangu kwamba hakuna mwanafunzi ambaye ni kilaza asilimia mia hapana, bali jinsi ambavyo wanafundishwa ndivyo kunavyoweza kuwarahisishia wanafunzi kwenye kujifunza na kuongeza udadisi kwao.

Kwa mfumo uliopo sasa wanafunzi wengi wanakariri mambo ambayo hawayaelewi undani wake kitu ambacho sio sawa.

Mfumo wa uandishi wa vitabu pia una shida na mbinu za ufundishaji za walimu pia hazifanyi kazi vizuri. Ingekuwa bora kama vitabu vyote vya kufundishia katika kila mada au kipengele ambacho mwanafuzi anafundishwa basi ielezwe historia ya hiyo mada.

Ni wapi hicho kitu kinapatikana katika mazingira ya kawaida lakini cha muhimu zaidi nini umuhimu wa kusoma hicho kitu. Hapo angalau tutakuwa tunaelekea kutimiza lengo la elimu ambalo ni kutuwezesha Watanzania wote kuyaelewa mazingira yetu vizuri.

Watu wanahisi kwamba tatizo la elimu yetu ni kuwa ya nadharia zaidi. Ukweli ni kwamba wanaoelewa hizo nadharia ni wanafunzi wachache sana, wengi wao hata hizo nadharia hawazielewi.

Kwa mfano, kuna njia mbili za kufundishwa kupika ugali, mosi kufundishwa moja kwa moja jikoni unaambiwa tia unga, koroga uji na hatua nyingine. Njia nyingine ni kukaa sebuleni halafu unaelekezwa namna ya kupika ugali.

Sasa kwa kiasi kikubwa Tanzania tunatumia njia ya pili ya kuelekeza tu namna ya kupika ugali bila hata ya kufika jikoni na maelekezo ambayo wanafunzi wanapewa hayajitoshelezi kuwawezesha kuja kusonga ugali jikoni.

Kuna wale ambao ukiwapeleka jikoni watatoa ugali mbichi, wengine wataivisha na wengine ambao ndiyo kundi kubwa zaidi wanaweza wakatia majani ya chai kwenye harakati za kusonga ugali.

Kuwajengea wanafunzi uwezo wa kutatua changamoto za jamii.

Mfumo wa elimu uliopo sasa hauwajengei wanafunzi uwezo wa kugundua mbinu mpya za kutatua matatizo ya jamii, wala hauwawezeshi vijana wetu kuwa wadadisi na mwisho wa siku kuja na vitu vipya.

Akili ya mwanadamu haina mipaka katika kutatua changamoto, ila sisi wenyewe tumejiwekea ukomo wa kufikiri na kusema kwamba hili jambo ni kwa ajili ya kundi fulani la watu. Uwezo wa mtu kutatua changamoto zinazomzunguka unatofautiana na ilitegemewa kwamba kwa Tanzania na nchi nyingine za dunia ya tatu kungekuwa na maendeleo makubwa kwenye teknolojia mbalimbali kutokana na mzigo mkubwa wa changamoto zilizopo kwenye jamii yetu.

Lakini kinyume chake watu kutoka nje ya Afrika wanakuja nchini kwa malengo ya kujifunza na kugundua vitu mbalimbali tofauti vilivyopo nchini. Sio kwamba Wazungu wana akili nyingi kuliko sisi, hapana bali sisi wenyewe hatujishughulishi hata kuanza na kutatua changamoto ndogo ndogo zinazotuzunguka.

Jambo hilo tunalirithisha kwa watoto wetu ambao nao pia wanaendelea kuishi kwa mazoea mpaka umri unapita. Matokeo yake jamii inakuwa imedumaa tu bila ya kwenda popote. Wanafunzi wetu wamekuwa wakipewa taarifa tu za mambo ambayo yalifanywa huko nyuma, au mambo ambayo yalitokea huko nyuma.

Baada ya hapo, siku ya mtihani watatahiniwa kwa kuangalia ni nani mwenye uwezo mzuri zaidi wa kukumbuka mambo hayo. Kuna mambo mengi mazuri ambayo wanafunzi wetu wanafundishwa wakiwa shuleni, lakini kuna kitu kinapungua kwenye mfumo wetu wa elimu.

Kitu hicho ni kwamba wanafunzi hawapati fursa ya kuzitumia akili na uwezo wao binafsi katika kuzitatua changamoto za jamii inayowazunguuka. Dunia inakwenda mbali sana siku hizi kwenye masuala ya maendeleo.

Je, tunawandaa vipi vijana wetu kwenda sambamba na maendeleo haya? Ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu hii na kuichanganya na ile ya darasani ili manufaa yaweze kuonekana kwenye jamii, kwanza kabisa ni lazima wanafunzi wapangwe katika vikundi vya wanafunzi wasiozidi watano.

Kisha wanafunzi hao watatakiwa kutambua changamoto ndogo ndogo zinazowakabili wakiwa shuleni au majumbani. Wakishapata changamoto itabidi waanze kujadili ni kwa njia zipi wanaweza kumaliza hilo tatizo.

Sio lazima changamoto iwe kubwa sana, hapana. Hapa tunaanza tu kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuzimulika changamoto na kuzitatua.

Kwa mfano shule inaweza kuwa ipo sehemu ya jangwani tangu imeanzishwa. Lakini kama kuna wanafunzi waliliona hilo miaka saba nyuma na wakaazimia kila mwanafunzi aje na mche mmoja wa mti, kisha akauhudumia mpaka anamaliza shule, miaka ya mbele shule hiyo haitakuwa na tatizo hilo tena badala yake wanafunzi watatafuta changamoto nyingine na kuitatua.

Mfano mwingine inawezekana wanafunzi wakawa wanasoma darasa ambalo halina mlango, na tuchukulie ni darasa la wanafunzi 50. Basi wanafunzi wenyewe wanaweza kuamua kuchanga kiasi cha shilingi 3000 kila mmoja na kuanza utaratibu wa kuweka mlango mwingine.

Wanafunzi wakijengeka katika msingi huu wanaweza kuwa wabunifu wazuri na kuja kujenga jamii ambayo wengi wetu tunaitamani. Lakini pia wanafunzi watatakiwa kupewa mafunzo kidogo kuhusu njia za kisayansi za kutatua matatizo.

Mpaka leo hii kwenye vitabu vyao vya kidato cha kwanza hizo njia za kisayansi za kutatua matatizo zipo, lakini uzingatiaji kwa wanafunzi pamoja na uelewa juu ya jinsi ya kuzitumia njia hizo kwenye maisha ya kawaida.
 
Upvote 2
Changamoto inabaki palepale.
Tumezalisha walimu wasiona ubunifu maana nawao walisoma vilevile.

Hao walimu wanaenda kutuzalishia wanafunzi wa aina ileile ya walimu.

Bado kuna dhana ya kusoma sana upate Dv 1 wakati dunia ya leo inahitaji ubunifu na uvumbuzi kutokana na changamoto zinazotukabili. Mfano suala la ajira, magonjwa, uharibifu wa mazingira.

Jamii yetu imekuwa ikihasishiwa Ngono ngono ngono ngono..

Unakuta mwalimu, mwanafunzi, mzazi, kila sehemu watu wanawazia ngono tu. Tutabakia kuwa wasindikizaji na wapokeaji wa mabadiriko kutoka kwa wenzetu wanao jua nini maana ya kuishi
 
Changamoto inabaki palepale.
Tumezalisha walimu wasiona ubunifu maana nawao walisoma vilevile.

Hao walimu wanaenda kutuzalishia wanafunzi wa aina ileile ya walimu.

Bado kuna dhana ya kusoma sana upate Dv 1 wakati dunia ya leo inahitaji ubunifu na uvumbuzi kutokana na changamoto zinazotukabili. Mfano suala la ajira, magonjwa, uharibifu wa mazingira.

Jamii yetu imekuwa ikihasishiwa Ngono ngono ngono ngono..

Unakuta mwalimu, mwanafunzi, mzazi, kila sehemu watu wanawazia ngono tu. Tutabakia kuwa wasindikizaji na wapokeaji wa mabadiriko kutoka kwa wenzetu wanao jua nini maana ya kuishi
nimekuelewa sanaa!!but we unahisi tunaweza kufanya nini kubadili hili?

as for me, naona tunaweza pita mahali na tukafika tunakotaka kwenda. tuchukulie kwamba tupromote mishahara ya walimu mwenye division one olevel na advance,na chuo akamaliza na grades za juu..obvious wanaofaulu sana hawasomeagi ualimu,na wala hawanaga ndoto za ualimu.why ?malahi madogo na heshima mtaani...juzi nilikuwa nacheck mahojiano T.O mmoja mdada akihojiwa..ndoto zake ni kuwa daktari,which is not bad,,ila yule bint kama angepewa special treatment ili kupika watu wengi zaidi kama yeye,kwa miaka ishirini tutakuwa na best teachers(with no disrespect to walimu waliopo,they are doing thr best kwa kweli).
 
Back
Top Bottom