Kikwete: Nina mke mmoja
Asema hakusudii kuoa, kuzaa tena
na Salehe Mohamed
RAIS Jakaya Kikwete jana alirejesha fomu zake za kuomba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimpitishe kuwa mgombea wake wa wadhifa huo, huku akisisitiza kuwa yeye ni mume wa mke mmoja na hakusudii tena kuoa.
Kikwete aliyerejesha fomu hizo za urais baada ya kudhaminiwa na wanachama 25,000 wa CCM kutoka mikoa 10 ya Tanzania, aliwaomba wanachama wa chama hicho kumpa fursa ya kugombea kiti hicho ili hatimaye aweze kumaliza kazi aliyoianza.
Akizungumza mbele ya umati mkubwa wa viongozi wa juu na makada wa CCM na serikali waliomsindikiza wakati akirejesha fomu za kugombea urais, aliomba apewe kipindi kingine ili amalizie kazi aliyoianza kwa mafanikio mazuri.
Nina mke mmoja na watoto wanane, pamoja na mwingine ambaye tulimuokota baada ya kutupwa na mama yake mara baada ya kujifungua, sitarajii kupata mke mwingine wala mtoto, alisema Rais Kikwete, hali iliyowafanya watu waangue kicheko.
Alisema pamoja na ukweli kwamba anacho kibali kwa mujibu wa dini yake ya Kiislamu kuoa wake wanne, anaamini hana sababu ya kufanya hivyo katika siku za usoni.
Kikwete alilazimika kutoa ufafanuzi huo kutokana na kauli aliyoitoa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ambaye alisema kiongozi huyo alikuwa ana sifa zote anazopaswa kuwa nazo askofu isipokuwa alikuwa hana uhakika iwapo ile ya kuwa na mke mmoja ni sifa ambayo alikuwa nayo pia.
Awali Makamba ambaye ndiye aliyepokea fomu za Kikwete na kuzihakiki alisema kiongozi huyo alikuwa na sifa zote za askofu za uadilifu, uchapa kazi na ile ya kutopenda pesa kama zilivyoandikwa katika kitabu cha Timotheo kwenye Biblia.
Hata hivyo, si Makamba wala Kikwete aliyekuwa tayari kueleza kwa undani ni kwa sababu gani hasa hoja ya mke zaidi ya mmoja iliibuliwa katika hafla hiyo ya urejeshwaji fomu ambayo pia ilihudhuriwa na mke wa rais, Salma Kikwete.
Tukio linaloweza kufananishwa na hilo ni lile lililotokea Machi 3, mwaka jana nchini Kenya, wakati rais wa nchi hiyo, Mwai Kibaki, alipoitisha mkutano wa dharura wa waandishi wa habari na kukanusha tetesi zilizosambaa za yeye kuwa na mke mwingine zaidi ya Lucy.
Ingawa Makamba anakuwa kiongozi wa kwanza kueleza wasiwasi huo hadharani, hakujapata kuwapo taarifa zozote za wazi zinazoeleza kuhusu maisha binafsi ya Rais Kikwete.
Hafla hiyo ya Kikwete kurejesha fomu ilishuhudiwa pia na umati mkubwa wa watu wakiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Philip Mangula.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kikwete aliwaomba Watanzania na wanachama wenzake wamchague ili aweze kumalizia kazi aliyoianza katika miaka mitano ya utawala wake.
Alibainisha kuwa watu wenye sifa za kuwania urais wapo wengi ndani ya CCM lakini hawajajitokeza kuwania nafasi hiyo kwa sababu ya kuwa na imani naye.
Alisema hana cha kuwalipa ila anawaahidi Watanzania kuwa kazi aliyoianza katika utawala wake ataendelea nayo ili nchi iweze kupiga hatua kwenye maendeleo sambamba na kuwakomboa Watanzania katika lindi la umaskini.
Napenda kuwaahidi wanachama wenzangu na Watanzania kuwa mkinichagua nitaendeleza yale mafanikio tuliyonayo hivi sasa, naomba NEC na Kamati Kuu ya chama inipitishe na hatimaye wananchi wanichague kuwa rais wao Oktoba 31, niendeleze yale niliyoyaanza, alisema.
Rais Kikwete alitumia fursa hiyo kueleza kuwa aliamua kumkabidhi mwanawe Ridhiwan na marafiki zake fomu za kuomba wadhamini kwa sababu jukumu hilo si la chama, bali ni la mgombea binafsi na yeye kwa kuwa ana mtoto mkubwa ndiyo maana ameamua kumpa kazi hiyo.
Sijawadharau viongozi wa chama kama watu wanavyosema, bali mchakato huu unamhusu mgombea mwenyewe. Namshukuru Ridhiwan, Beno Malisa na marafiki zao kwa kutembeza fomu zangu za wadhamini mikoani, alisema.
Kwa upande wake Makamba alisema, Rais Kikwete ni mtaji mkubwa kwa chama hicho na kwa kuonyesha hilo amedhaminiwa na wanachama 14,690 katika mikoa yote, idadi ambayo ni kubwa kuliko iliyokuwa ikitakiwa ya wanachama 2,500 katika mikoa isiyopungua 10.
Alibainisha kuwa wana CCM wenzake hawakutangaza nia ya kuwania kiti hicho ndiyo maana Mbunge wa Maswa, John Shibuda, aliyekuwapo katika hafla hiyo ya jana aliamua kutoendelea na nia yake ya kugombea kama alivyokuwa ametangaza awali.
Alisema kuwa jina la kiongozi huyo linatarajiwa kupelekwa kwenye vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho kabla ya kufikishwa kwenye mkutano mkuu utakaofanyika Julai 10-11 ambao ndio utakaomteua mgombea wa urais, ambaye atapambana na wagombea wengine kutoka vyama vya upinzani.
Naye mwakilishi wa mtandao wa wanafunzi wa vyuo vikuu (CCM), Harous Sanga, alitoa tamko la mtandao huo kuwa wataendelea kushirikiana na Rais Kikwete bega kwa bega mpaka hapo atakaposhinda urais.
Akizungumza katika hafla hiyo, Shibuda alitoa shilingi 200,000 kuchangia kampeni za urais za Kikwete.
Alisema kuwa alitangaza nia ya kutaka kuwania kiti hicho lakini baada ya kufanya upembuzi yakinifu, aliamua kutowania kwa sababu ya utendaji mzuri wa kiongozi huyo kwenye nyanja za uchumi, elimu, kilimo na nyinginezo. Sikulazimishwa na wana usalama wala viongozi wa juu wa chama changu kutowania urais mwaka huu, dhamira yangu ndiyo iliyonituma, sikunyanyaswa na mtu, hii inadhihirisha kuwa Rais Kikwete anatuongoza kwa demokrasia, alisema. Aliongeza kuwa Rais Kikwete si kiongozi mwenye fikra kandamizi, ndiyo maana kila mwanachama ndani ya chama hicho ana fursa ya kuwania uongozi kulingana na matakwa yake.
" Ridhwani na Marafiki zake" hapo haoni kuwa hata huo umoja wa vijana kama hajabinafishwa , basi huko njiani kubinafsishwa.
Kama Uongozi iwe kwenye CCM au serikali ni wa kidemokrasia mbona hakuna usawa katika kampeni na uteuzi, ume kaa kirafiki rafiki na kindugu?
RA na mashabiki wake, EL na washabiki wake nk nk. Wezi wa EPA na Mashabiki wao