Posted Date::11/29/2007 MWANANCHI
Ukaguzi wa Benki Kuu Tanzania wabaini kasoro
*Ripoti za awali zaonyesha utata
*Baadhi ya vigogo BoT watajwa kuhusika
*Wahusika kuchukuliwa hatua
*Meghji asema hajaipata, iko kwa CAG
Na Ramadhan Semtawa
JOTO la tuhuma za ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) limepanda, kutokana na taarifa za awali za ukaguzi kuonyesha kuwa kuna utata katika matumizi ya akaunti hiyo.
Ukaguzi huo ulifanywa na Kampuni ya Ernst & Young katika kipindi cha siku 60, kuanzia Septemba na kukabidhi ripoti yake kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wiki iliyopita.
Hata hivyo, ikiwa ni wiki moja tangu CAG kukabidhiwa ripoti hiyo, taarifa za awali kutoka vyanzo mbalimbali vya habari ndani na nje ya serikali, zinaeleza kwamba baadhi ya vigogo ndani ya BoT wanatajwa kuhusika na malipo hayo yenye utata.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, vigogo hao wanahusishwa na ama kuidhinisha au kuhusika kwa namna moja au nyingine katika malipo hayo.
Vyanzo hivyo vilifafanua kwamba, maamuzi kuhusu ripoti hiyo yanatarajiwa kuchukuliwa kabla ya mwaka mpya.
"Watu watapata zawadi ya mwaka mpya, uchambuzi unaendelea kufanyika, lakini taarifa za awali zinaonyesha hivyo," kilisema chanzo cha habari kutoka serikalini.
Vyanzo hivyo vilifafanua kwamba, kuna baadhi ya stakabadhi za malipo ambazo zimeanza kuchambuliwa na zinaonyesha kuwa zimejaa utata.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, uchambuzi huo umezingatia kwa kina nyaraka za msingi za malipo ili kuona utata huo unasababishwa na nini.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, ukaguzi huo ambao uliingia kwa ndani na kuhoji watu mbalimbali akiwemo Waziri wa Fedha, Zakia Meghji unaweza kubadili hali ya kisiasa nchini katika kipindi cha kuingia mwaka mpya wa 2007/08.
Meghji alipoulizwa ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana kuhusu ripoti hiyo, alisema hadi sasa bado iko kwa CAG.
Alisema hafahamu lolote kuhusu kilichomo ndani ya ripoti hiyo kwani hajaiona na wala hawezi kuzungumza yaliyomo kwa sasa.
"Hadi sasa ripoti iko kwa CAG, sijaipata kama ni suala la maamuzi na nini kilichomo ni hadi ichambuliwe, nikiipata, nitaipitia, atapewa Rais na maamuzi yatatangazwa kwa umma," alisema Meghji.
Kauli hiyo ya Meghji ni ya pili ambapo ya kwanza ilitolewa na CAG ambaye wiki iliyopita alisema ofisi yake inafanyia kazi mambo yaliyomo katika ripoti hiyo, lakini hakufafanua.
Ernst & Young, awali ilipaswa kuikabidhi ripoti yake serikalini Novemba 10 ikiwa ni kumalizika kwa siku 60 za kufanya ukaguzi huo, lakini haikufanya hivyo na kuiomba serikali wiki tatu kwa ajili ya kuandaa ripoti ambayo ilifanyikia London, Uingereza.
Ripoti hiyo inasubiriwa kwa hamu na Watanzania kuona ukweli wa tuhuma za ufisadi ambazo zinadaiwa kufanywa katika EPA kwa ajili ya malipo ya vocha mbalimbali.
Nchi wafadhili pia zimesema zinasubiri kwa hamu matokeo ya uchunguzi huo kwani ni kipimo cha kuona mwelekeo wao wa kuongeza misaada kwa Tanzania katika bajeti ya mwaka 2008/09.
Kampuni hiyo ilipitia mahesabu katika kumbukumbu za vocha za malipo yaliyofanywa na BoT katika kipindi cha mwaka 2005/6, kubaini kama kuna ukweli juu ya madai ya ubadhirifu wa fedha katika benki hiyo katika kipindi hicho.
Agizo la kutafuta kampuni ya kukagua vocha hizo na mahesabu ya BoT, lilitolewa na Waziri Meghji Desemba 3, mwaka jana akimtaka CAG kuteua kampuni huru ya wakaguzi wazoefu wenye sifa za kimataifa kupitia baadhi ya kumbukumbu za matumizi ya fedha za benki za mwaka 2005/2006 ili kuondoa utata.