Akizungumza na Mwanaspoti jana,
kocha Robertinho alisema ameiona
hali ya mashabiki wa klabu hiyo
kutomkubali Bocco, ila kwa
mtazamo wake bado ni
mshambuliaji bora anayeweza
kucheza kwa maelekezo na
kuisaidia timu, hivyo hawezi
kumuacha nje kizembe.
Mbrazili huyo alisema Bocco pekee
amekuwa akifanikiwa kucheza kwa
maelekezo yake kwa kutumia muda
mwingi kukaa ndani ya eneo la
wapinzani faida ambayo imewapa
nafasi ya timu hiyo kufunga mabao.
"Sikiliza, ni kweli naiona hiyo hali,
mashabiki waje uwanjani kuangalia
Simba inacheza mpira vizuri.
Kwangu Bocco bado ni
mshambuliaji mzuri kwani
anakwenda kufanya kile
ninachokitaka afanye,” alisema
Robertinho na kuongeza;
"Hata katika mechi dhidi ya
Dynamos (Power) aliingia akafanya
nilichotaka tukapata bao lililosaidia
kutuvusha makundi na leo (juzi)
nimempa nafasi ya kuanza
amefunga tena, lakini akawafanya
mabeki wa Prisons kwa muda
mwingi kubaki nyuma, nataka
mshambuliaji wa aina hii anayekaa
muda mrefu eneo la hatari la
wapinzani na hili ndicho anafanya
Bocco huyu bado ni bora kwangu.”
Kocha huyo alisema anao
washambuliaji wengine kama Jean
Baleke na Moses Phiri ambao nao ni
wazuri kwa kukimbia pembeni
lakini wamekuwa hawajaweza
kucheza kwa nidhamu kama
anavyofanya Bocco.
"Nimezungumza na Bocco
nimemwambia aachane na mambo
ya mashabiki anisikilize mimi kama
kocha wake, mashabiki wanataka
ushindi hesabu zetu ndio
zitakazowapa furaha, unaona
amefunga wamenyamaza nataka
aendelee kufanya hivyo hivyo kila
mara kwani nitaendelea kumtumia,”
alisisitiza Robertinho aliyefikisha
jumla ya mechi 15 bila kupoteza
katika Ligi Kuu Bara.