BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 525
- 1,257
Siku chache kabla ya siku ya uteuzi wa wagombea wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara wa chama kikuu cha upinzani nchini yaani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu alinukuliwa akisema kuwa chama hicho kinakabiliwa na changamoto ya wagombea katika uchaguzi unaoendelea wa serikali za mitaa
Lakini kama hiyo haitoshi, licha ya tambo zao na kujipiga kifua viongozi wa ACT Wazalendo sirini nao pia wanakiri kuwa hawana wagombea wa kutosha katika uchaguzi huu, hiyo ndio sawa na kusema kwamba ushindani wa vyama vya upinzani kwa chama tawala yaani Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa namna yoyote ile kwenye uchaguzi huu haiwezi kulandana kwa kuwa kitendo cha kuwa na wagombea wachache tu ni dhahiri kuwa kinatoa mianya ya CCM kukosa ushindani kwenye maeneo mengi jambo ambalo ni faida kwao kama chama tawala
Jambo Online TV imefanya uchunguzi wake kwa kutumia sampuli ya baadhi ya maeneo ya nchi kwa kuzungumza na viongozi wa vyama tofauti vya siasa kuanzia CCM, CHADEMA, ACT Wazalendo, CUF nk sambamba na wasimamizi wa uchaguzi, ambapo matokeo ya uchunguzi huo kwa kiasi kikubwa yanashabihiana kabisa na kile kilichosemwa hadharani na Tundu Lissu, na kile wanachokiri sirini baadhi ya viongozi wa ACT Wazalendo
Kwa mfano, wakati Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani Boniface Jacob (Boni Yai) alipokutanisha wagombea wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam alieleza kuwa CHADEMA ina wagombea 95% ya mitaa yote ya jiji la Dar es Salaam, lakini uchunguzi wetu umeonyesha kuwa ilikuwa ni tambo za siasa tu, ndio tuna ujasiri wa kusema tambo za siasa kwa kuwa jimbo la Kigamboni kwa mfano chama hicho kimeweka wagombea chini ya nusu ya mitaa yote, kata ya Manzese katika jimbo analotoka Boni Yai mwenyewe yaani Ubungo yenye mitaa 10 CHADEMA ina wagombea mitaa mitano (5) tu, na katika jimbo la Kawe hususani mtaa wa Masaki chama hicho hakina hata mgombea wa ujumbe wa kamati ya mtaa
Hayo ni tofauti na taarifa zilizotolewa na viongozi wa CHADEMA Kanda ya Pwani, kwani kwa mujibu wa katibu wa kanda hiyo Jerry Kerenge alidai kuwa katika mkoa wa Dar es Salaam wenye mitaa 564, CHADEMA ilikuwa imesimamisha wagombea kwenye mitaa 547 ambapo ni sawa na asilimia 95 ya mitaa yote
Hali ni hiyo hiyo kwa Chama cha ACT Wazalendo, ambacho bila kumung'unya maneno hiki ndicho chama cha pili kwa ukubwa katika vyama vya upinzani hapa nchini, majimbo ya Temeke na Mbagala ambayo ni majimbo ya hakika ya chama hicho wagombea wa chama hicho ni 30% tu ya mitaa yote inayogombewa
Hali ni mbaya zaidi kwenye majimbo ya vijijini na mikoa ya pembezoni kwa vyama vyote 2 vikuu vya upinzani hapa nchini, na hapa nieleweke kuwa natambua mchango na nafasi ya vyama vingine vya upinzani nje ya CHADEMA na ACT Wazalendo lakini kila mmoja atakubaliana nami kuwa kama tunataka kuona au kujadili taswira ya upinzani nchini ni lazima macho na masikio yetu yajielekeze kwenye vyama hivyo viwili (2)
Licha ya 'udhaifu' huo wa vyama vya upinzani nilioueleza kwa uchache hapo juu lakini kilichotokea siku ya uteuzi tarehe 8/11/2024 ni kama imewapa nguvu vyama hivi viwili (2), kitendo cha wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuwaengua wagombea wa upinzani licha ya uchache wao kumewapa nguvu ya kueneza propaganda ya vyama hivi kiasi cha kuficha udhaifu wao wa kutokuwa na wagombea
Hata bila kuwaengua wagombea wao tayari CCM walikuwa wanabaki peke yao kwenye 70-75% ya vitongoji, vijiji na mitaa yote ya Tanzania Bara ambako uchaguzi huo ndiko unakofanyika, kwenye nafasi ya Wenyeviti wa vitongoji, vijiji na wajumbe wa Halmashauri ya kijiji CCM inagombea peke yake katika zaidi ya 80% ya nafasi hizo, vivyo hivyo kwenye mitaa
Sasa swali la kujiuliza hapa, kwa nini mfumo unavumilia vitendo vya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kama hali ni hii?, mfumo hauoni kuwa unawapa wapinzani wao sifa ambazo hawana na wakati huo huo kujiharibia ushindi wa halali kabisa kwa chama tawala (CCM)?...