Josephat Gwajima akana utajiri wake

Josephat Gwajima akana utajiri wake

Magazetini

JF-Expert Member
Joined
Aug 16, 2014
Posts
593
Reaction score
1,712
gwajima12_300_172.jpg


ASKOFU Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, amesema yeye si tajiri kama inavyodhaniwa, bali alichonacho ikiwa ni pamoja na nyumba, magari na helikopta ni baraka tu za Mungu, lakini kama ni utajiri, anatarajia siku moja utamshukia.

Aliyasema hayo jana wakati akihubiri kanisani kwake Kawe, Dar es Salaam, ambako alisema anawashangaa watu wanaomfuatilia maisha yake huku wakisema yeye ni tajiri mkubwa.

"Wanaodai mimi ni tajiri wana wivu tu na wananionea, mimi si tajiri, bali ni masikini kama walivyo masikini wengine. Natarajia kutajirika hapo baadaye waumini wangu wakiwa matajiri, siwezi kutajirika kama waumini wangu bado ni masikini, nitatajirika pamoja nao," alisema Gwajima.

Kuhusu mgogoro unaoendelea baina yake na Jeshi la Polisi, Askofu Gwajima alisema yeye anauona kama ni vita vya kiroho na hivyo ataendelea kumwomba Mungu ili amsaidie kupambana na kilichopo mbele yake na anaamini kuwa atashinda vita hiyo kwa uweza wa Mungu anayemtegemea.
"Mungu wangu na awasamehe wote wanaonituhumu kuwa mimi ni tajiri na kuamua kudhoofisha huduma, nasema huduma yangu haitakufa kamwe na wala hatutayumba katika mipango yetu ya kuhubiri injili. Tutapigana kwa uweza wa Mungu na tutashinda kama alivyosema kuwa tutapigana pamoja naye na tutashinda," alisema Gwajima.

Akizungumzia afya yake, Askofu Gwajima alisema kwa sasa anaendelea vizuri na anaweza kusimama na kutembea, kuhubiri kama ilivyokuwa hapo awali na hatarajii kurejea tena kwenye kiti cha baiskeli ya magurudumu matatu bali atasimama imara daima.

Kuhusu kupeleka nyaraka kadhaa anazotakiwa aziwasilishe polisi siku ya mahojiano Aprili 16, mwaka huu, Askofu Gwajima alisema suala hilo bado wanasheria wake wanalishughulikia na wataendelea kufuata taratibu zote zinazotakiwa na jeshi hilo.

Gwajima anatakiwa kuwasilisha nyaraka muhimu za hati ya usajili wa kanisa lake, namba ya usajili wa kanisa, hati ya umiliki wa helikopta, hati ya nyumba anazomiliki, idadi ya makanisa yaliyopo chini yake pamoja na hesabu za fedha za kanisani kwake zinazohusu mapato na matumizi.

Nyaraka zingine ni majina ya Bodi ya Udhamini wa kanisa, mpiga picha za video kanisani kwake siku ya ibada na shughuli zingine za kanisani hapo pamoja na waraka wa Maaskofu uliosomwa makanisani ambao Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo alioupinga na kusababisha yeye kumkashifu kiongozi mwenzake huyo wa dini.

Akionekana kuwa makini sana na lugha anayotumia wakati wa kuhubiri, Gwajima aliwaomba waumini wake waendelee kufuatilia kila sehemu na kuchunguza mambo yote mabaya yanayosemwa juu yake na kanisa lake na kuyaripoti kwake au kwa uongozi wa kanisa ili wayafanyie kazi mara moja kabla hayajaleta madhara.

"Nawaombeni sana mfuatilie kila chanzo cha habari na kuchunguza mambo yote yanayosemwa juu yangu au kuhusu kanisa na kuyaleta mara moja hapa kanisani ili tuyafanyie kazi kabla hayajaleta madhara makubwa," alisema Gwajima.

Aliongeza kuwa, "tuendelee kuwa na umoja katika kipindi hiki ambapo shetani anataka kupigana nasi ili tuweze kushinda. Tukifarakana hatutaweza bali tukiwa kitu kimoja tutasonga mbele na kuwa huru".

Utajiri wake
Wakati akikana kuwa tajiri, mwanzoni mwa mwaka jana alifanya mahojiano na gazeti hili na kukiri Mungu anambariki, ndiyo maana mambo yake yanamnyookea.
Aliyasema hayo alipokuwa anazungumzia mpango wake wa kununua helikopta kwa ajili ya huduma za injili ndani na nje ya nchi.

Alikiri kutokana na utajiri anaosema unatokana na baraka za Mungu, anamiliki jumba la ghorofa nne eneo la Mbezi Beach katika Manispaa ya Kinondoni.

Pia amewanunulia wachungaji wake 40 magari ya kutembelea kwa bei tofauti, yakiwemo ya chini ya Sh milioni 10 na mengine ya zaidi ya Sh milioni 20.

"Ni kweli nimewanunulia magari, unajua moja ya misingi yangu ya maisha ni kwamba, mimi siwezi kuishi maisha mazuri, wakati wachungaji wangu wanadhalilika, nimewanunulia magari karibia 40. Lakini nina wachungaji wa ngazi mbalimbali, hawa ni wale wa juu, wengine wachungaji wadogo wapo zaidi ya 670, hawa ni watenda kazi muhimu na wanatofautiana kwa ngazi zao, ndio maana kazi ya Mungu inasonga mbele hata nisipokuwepo," alisema Gwajima.

CHANZO: Habari Leo
 
duh. haya masikini ana 'hedikopta' na jumba la ghorofa nne! nchi hii hii
 
Inakuwaje mambo ya polisi yanakuja kuhubiriwa kanisani hivi huwa ni sehemu ya ibada, kwa nini injili isihubiriwe kama injili bila kuleta mambo ya polisi.

utaratibu wa ibaada huwa ukoje huko?
 
Hata mimi niliukana utajiri wangu kumbe gwajima ameniiga aiseeee
 
Inakuwaje mambo ya polisi yanakuja kuhubiriwa kanisani hivi huwa ni sehemu ya ibada, kwa nini injili isihubiriwe kama injili bila kuleta mambo ya polisi.

utaratibu wa ibaada huwa ukoje huko?
kweli . kwanini makanisani,misikitini kusiwe ni ibada tu,
 
Asema, JK atoe tamko juu ya polisi wanaomwandama. Adai kama hajatoa tamko basi yeye ndio aliowatuma.

Aeleza siri ya utajiri wake, waumini wamchangia mamilioni papo hapo.

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemwomba Rais Jakaya Kikwete kuvikemea vyombo vya dola vinavyomfuatafuata vikihoji mambo binafsi na kwamba akishindwa kufanya hivyo itakuwa wazi kwamba yeye ndiye anawatuma.

Akihubiri mamia ya waumini wa kanisa hilo jana, Gwajima alisema amekuwa akifuatwafuatwa na vyombo vya Serikali utadhani yeye si raia wakati ni Mtanzania halisi.

"Rais Kikwete tafadhali namuomba awakemee watu hawa... asipowakemea, basi kanisa langu litajua kwamba yeye ndiye anayewatuma," alisema Gwajima huku akishangiliwa na waumini waliokuwa wakimsikiliza.

Huku wakinyeshewa na mvua, waumini hao walikuwa wakimsikiliza Askofu Gwajima, siku tatu baada ya kiongozi huyo kuhojiwa kwa mara ya pili na polisi na kutakiwa awasilishe mambo 10 yanayohusiana na usajili wa kanisa, uongozi na mali zake.

Uraia wake

"Mimi ni Mtanzania halisi acheni nifanye kazi ya Mungu, kama mnadhani mimi si Mtanzania, basi mmepotoka kwani kwa hilo mtashindwa," alisema.

Alisema makundi ya jamii yamekuwa yakitoa kauli mbalimbali lakini hayabughudhiwi anavyofanyiwa.

"Madaktari, wanasiasa, wafanyabiashara wamekuwa wakitoa misimamo yao lakini hawabughudhiwi iweje Gwajima tu? Nitaendelea kuwapa vidonge vyenu kila mtakapopotoka, nafanya kazi ya bwana," alisema.

Kuhusu utajiri wake

Gwajima alisema amekuwa akishangazwa na vyombo vya Serikali vinavyohoji utajiri alionao bila kujua anaongoza idadi gani ya waumini. Alisema anaongoza kanisa lenye waumini zaidi ya 70,000 ambao ni kama watoto wake na kwamba yeye ni baba yao wa kiroho.

"Waumini hawa mimi ni baba yao wa kiroho, nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 tu nitakuwa na Sh70 milioni, halafu mnahoji utajiri ninaupata wapi?" alisema na kisha kuwauliza waumini hao... "Hivi baba yenu nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 mtanipa au mtaninyima?"

Alijibiwa, "Tutakupaaaa!" Baada ya majibu hayo waumini hao walianza kupeleka fedha katika jukwaa kuu huku wakiimba nyimbo za kumtukuza Mungu.

Waumini hao, wengi wao wakiwa wameshikilia noti za Sh10,000 na Sh5,000 walianza kusonga mbele na kutumbukiza kwenye maboksi.

Mchango huo ulichukua dakika 25 kuanzia saa 6.30 hadi saa 6.55 mchana na ulisimama pale Askofu Gwajima kuwaambia... "Basi basi naomba muache kuleta fedha, zinatosha, kaeni msikilize mahubiri, tukiendelea kupokea fedha hapa tutakesha. Watu wa idara ya fedha kusanyeni maboksi yenye fedha na pelekeni kunakohusika, hizi ni fedha za kanisa ambazo zitatumika katika mambo mbalimbali ikiwamo kununua mafuta ya kuendesha jenereta la kuzalisha umeme."

Gwajima alisema kutokana na idadi ya waumini wake kama kila mmoja atampa Sh10,000 basi atakuwa na Sh700 milioni.

"Wakinipa Sh100,000 kila mmoja ina maana nitakuwa na Sh7 bilioni, nawashangaa wanaohoji kuwa huu ni utajiri, watu hawalali usingizi wanajiuliza Gwajima anapata wapi utajiri huu, nawaambia mimi siyo tajiri hizi ni fedha za kanisa," alisema.

Idadi ya waumini

Askofu huyo alisema mbali na utajiri, watu wanahoji anapata wapi waumini wengi namna hiyo.

"Shida si kumkashifu Askofu Pengo, bali sasa wanahoji waumini wengi wanafuata nini hapa," alisema na kuongeza," nao wakija kunisikiliza watafahamu nini mnachokifuata kwani nao watabaki hapahapa hawatatoka."

Alisema baada ya kuandamwa na vyombo vya Serikali, maaskofu walitaka kutoa tamko lakini aliwakataza kwa sababu aliona anafanyiwa hivyo kwa sababu binafsi. Alisema katika kipindi ambacho amekuwa akiandamwa na polisi, waumini wameongezeka kanisani kwake.

"Walokole wakiwa katika tabu, ndiyo kwanza wanashikamana, ukitaka kuwasambaratisha wape neema utafanikiwa. Wakipata nyumba nzuri, gari zuri, kazi nzuri na safari katika nchi mbalimbali wanaacha kuja kanisani lakini wakiwa katika matatizo wanashikamana, hamuwezi kuwasambaratisha," alisema.

Ilivyokuwa awali

Gwajima amehojiwa mara mbili na polisi kutokana na matamshi yake ya kashfa dhidi ya Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, lakini mara ya pili mwelekeo wa mahojiano ulibadilika ukalenga zaidi kanisa na mali zake.

Mara ya kwanza kuhojiwa ilikuwa Machi 27, siku ambayo alizimia na kupelekwa katika Hospitali ya TMJ alikolazwa kwa siku nne huku taarifa zikieleza-

Baada ya kutoka Polisi, Gwajima amekuwa akitembea kwa kutumia kiti cha magurudumu mawili hadi Aprili 6, Siku ya Pasaka baada ya kuombewa na wachungaji kutoka Japan.

Alhamisi iliyopita, alihojiwa kwa mara ya pili na kutakiwa kurudi tena Polisi Aprili 16 akiwa na mambo 10 yakiwamo hati ya usajili wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini, idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia, nyaraka za helikopta ya kanisa, muundo wa uongozi wa kanisa, waraka wa maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za kanisa na nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi leo.
 
mara anadai mungu kambariki utajiri,mara anadai yeye maskini,huku ni kuwakejeli masikini bana.
 
Eti yeye si Tajiri anasubiri neema ya Mungu....

mweeeeh..... alichonacho chatoka kwa mungu kweli au???
 
gwajima amwambia rais kikwete asimfuatilie fuatilie ama sivyo........
 
Lumumba mpo biz kuanzisha thread za Gwajima kupotezea mnavotoa sadaka watu kwenye ajali!
Na leo tena mmefanya! Baada ya kustukiwa kwenye albino sasa mmehamia barabarani!
Kwani damu haijatosha tu?
 
Waumini wake hawajaushtukia utajiri qa bishop wao? Kama yeye wamemwezesha kumiliki vyote hivyo alivyo navyo wao watakuwa mara kumi yake kwani wanachomtolea ni fungu la kumi eti eeh! Maskini waumini hawa, hebu mjitambue basi kuwa Mungu aliyehai hahitaji sadaka ya fedha wala dhahabu!
 
...ni rahisi ngamia kupenya ktk tundu la sindano kuliko tajiri kurithi ufalme wa mbinguni...

.,wana macho lkn hawaoni..
 
Rais wetu kikwete maliza hilo sakata katika waumini wa Gwajima wapo makada wa ccm mule na wapiga kura wako wengi tuu wape furaha wanaoitegemea kwa sasa macho yote kwako mh.
 
Rais wetu kikwete maliza hilo sakata katika waumini wa Gwajima wapo makada wa ccm mule na wapiga kura wako wengi tuu wape furaha wanaoitegemea kwa sasa macho yote kwako mh.

Mi sipendi mtu anaye qoute habari ndeefu kama hii alafu anaandika uharoo, wengine tunatumia vitochi bana haaa
 
Back
Top Bottom