Jumba la elimu ya watu wazima na historia ya Gerezani, new street na wazalendo wake

Jumba la elimu ya watu wazima na historia ya Gerezani, new street na wazalendo wake

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
1564207580457.png


Kiwanja palipojengwa hili jumba la Elimu ya Watu Wazima kilinunuliwa na John Rupia wakati wa harakati za TANU kudai uhuru wa Tanganyika kati ya mwaka wa 1954 hadi 1961.

Mbele ya kiwanja hiki mtaa huu ukijulikana kama New Street ambao ulikuwa unaanza si mbali na hapo, unaanzia Arab Street (sasa Mtaa wa Nkrumah).

New Stret unakwenda moja kwa moja unakatiza Kitchele hadi kugota Morogoro Road.

Kwa mkono wa kushoto ukianza hapo kwenye hicho kiwanja mtaa wa kwanza utakaokutananao ni Somali Street (sasa Omari Londo) na mwanzo tu wa Mtaa kulikuwa na nyumba ya baba yake Zuberi Mtemvu, Mzee Mwinshehe Mmanga Mtemvu, Mluguru kutoka Morogoro.

Kupandisha na huo Mtaa wa Somali utakutana, nyumba ya Omari Londo.

Turudi New Street tunaelekea Morogoro Road tuko bado kushoto kwenye makutano ya Somali na New Street, hapo kulikuwa na nyumba ya Bi. Mruguru bint Mussa mama yao akina Abdul, Ally na Abbas Sykes pamoja na nyumba nyingine kadhaa hadi kufika Kirk Street (sasa Mtaa wa Lindi).

Watu wa Dar es Salaam kwa kushindwa kutamka jina la Kiingereza, ''Kirk,'' walikuwa wakitamka, ''Kiriki.'

Huyu Kirk jina lake kamili ni Dr. John Kirk historia yake ni ndefu yeye alikuwa Mwingereza kutoka Scotland aliyesafiri na Dr. David Livingstone hadi Zanzibar na akafanya kazi katika utawala wa Uingereza hapo visiwani.

Dr. John Kirk na Dr. David Livingstone wote wawili walikuwa na mitaa Gerezani.

Mtaa wa John Kirk umefutwa lakini wa David Livingstone bado uko hadi leo.

Mmoja wa wakati wa Mtaa huu wa Kirk alikuwa Mwalimu Bakari watu walipenda kumwita Mwalimu Bakari Seti Khabar kwa kuwa alikuwa bingwa wa ilm ya majini.

Katika Mtaa wa Livingstone ilikuwapo studio ya Mzee Shebe aliiyenipiga mimi picha yangu ya kwanza mwaka wa 1953 na pia akaja kuwa mpiga picha wa mwanzo wa TANU na Julius Nyerere na kuhifadhi historia yote ya uhuru.

Baada ya Kirk Street mtaa unaofuatia ni Mtaa wa Kipata ambako akina Sykes walikuwa na nyumba nyingine.

Mtaa huu huu Kirk ukiufuatia kwa juu kulikuwa na nyumba nyingine ya akina Sykes na kabla ya kuvuka barabara ya Sikukuu kulia kulikuwa na kinyozi Muingereza na kulikuwa na Barza ya wana TANU hapo wakikutana kupeana taarifa za siku.

Leo hapo alipokuwa kinyozi Mwingereza leo ipo ofisi ya CAN ya Gerezani.

Sina hakika kama chanzo cha TANU kuhodhi kiwanja hiki na baadae CCM kujenga ofisi hapo inatokana na historia ya kinyozi Muingereza.

Sasa ukivuka barabara hiyo kwenye kona ya Kirk na Mtaa wa Nyamwezi ipo nyumba ya ghorofa moja ya Muhsin Mende.

Muhsin Nende historia yake imefungana na historia ya Zuberi Mtemvu kwani wote walikuwa TANU kisha wote wakatoka TANU mwaka wa 1958 kuunda African National Congress (ANC) kuipinga TANU.

Ukivuka Mtaa wa Nyamwezi upande wa kushoto unakutana na nyumba ya Ramadhani Mashado Plantan.

Mashado Plantan yeye alitoka TANU na wenzake wengine mwaka huo huo wa 1958 kuunda All Muslim National Union (AMNUT) pia kupinga TANU.

Mbele kidogo ya nyumba ya Mashado Plantan ilkuwapo nyumba ya Bi. Tatu bint Mzee.

Kamateni haya majina kwani hawa wote walikuwa wana TANU ingawa walikuja kugombana na wengine wakaihama TANU lakini hawa wote wameacha alama katika historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika.

Nyumba hizi kadhaa kati ya Somali na Kipata zilivunjwa na serikali kupisha ujenzi wa Jumba la Ushirika lakini katika hawa wote wenye nyumba hizi ni Bi. Mruguru peke yake aliyeandikiwa barua binafsi na Mwalimu Julius Nyerere akimuomba nyumba yake ivunjwe.

Kwa nini Bi. Mruguru peke yake ndiye apokee barua kutoka kwa Mwalimu Nyerere na hao wengine waandikiwe na Waziri wa Ardhi?

Bi. Mruguru alikuwa mama yake Abdul Sykes kwa hiyo ni mama yake Mwalimu Nyerere vilevile.

Wakati wa harakati za kudai uhuru Mwalimu akifika nyumba ile na Abdul Sykes kumsalimia mama yao na hata pale Bi. Mruguru alipohamia Kirk Street nyumba no. 56 Nyerere na Abdul wakienda sana pale.

Abdul alikuwa ikiwa atasimama barazani kwa nyumba hiyo ya mama yake angeweza kuzungumza na mtu aliye pale barazani kwa Muingereza.

Mikutano ya TANU ya mwanzo ilikuwa ikifanyika mbele ya sehemu hiyo TANU ilipojenga Jengo la Elimu ya Watu Wazima ndani ya Viwanja Vya Mnazi Mmoja.

Bi. Mruguru aliweza kukaa uani kwake siku ya mkutano wa TANU na akasikiliza hotuba yote ya Nyerere bila ya shida yoyote.

Ukitoka Kirk Street unaingia Mtaa wa Kipata alikozaliwa Mwandishi.

Ukiwa kama unapandisha juu na nasema kupandisha juu kwa sababu ukiwa New Street baada ya barabara ni Viwanja vya Mnazi Mmoja kulia hakuna nyumba hadi uivuke Kitchwele ndiyo unakutana na nyumba pande zote mbili za barabara kuanzia Mtaa wa Stanley (baadae Aggrey na sasa Max Mbwana).

Hapa Kipata kushoto kulikuwa na nyumba ya zamani ya akina Sykes sasa ni ghorofa na hapa ndipo walipokulia na wakati wa harakati za TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika Ally Sykes akiishi nyumba hii na katika nyumba hii alificha mashine ya kuchapa makaratasi ya ''uchochezi,'' dhidi ya serikali.

Mkabala na nyumba hii ya Kleist Sykes ilikuwa nyumba ya Sheikh Abdallah Simba Liwali wa Songea.

Nyumba hii ya Abdallah Simba sasa haipo imejengwa Petrol Station.

Babu yangu akiishi nyumba hii ya kupanga na wanae.

Yeye nyumba yake alijenga Mtaa wa Mbaruku jirani na nyumba ya Aziz Ali kabla hajahamia Mtoni.

Ikiwa uko Mtaa wa Uhuru umeshavuka Mtaa wa Lumumba angalia kushoto utakiona hicho kituo cha mafuta.

Hii ni miaka ya 1930 na babu yangu Salum Abdallah akifanya kazi Tanganyika Railways Idara ya Kufua Vyuma (Foundry) na Kleist alikuwa Accounts Clerk, akienda kazini kapanda baiskeli.

Siku hizo waliokuwa na uwezo kama huo wa kununua baiskeli walikuwa Wahindi.

Tupandishe juu Kipata tunaelekea Msimbazi.

Mtaa wa Kipata na Congo kulikuwa na nyumba ya Abdallah Hamisi kabila Mnubi baba yake aliingia Tanganyika na jeshi la Wajerumani akitokea Sudan na ni mmoja katika waasisi wa African Assocaition mwaka wa 1929.

Mwisho wa Mtaa wa Kipata kabla ya Barabara ya Msimbazi kulikuwa na nyumba ya Abdallah Matimbwa.

Hivi sasa hii nyumba haipo na badala yake mwanae Salum Abdallah Matimbwa kajenga ghorofa.

Mkabala na nyumba hii palikuwa na uwanja mtupu ambao jina la Kitchweli ndipo lilipotokea.

Ilikuwa katika uwanja huu watu wakileta biashara zao kuuza kuanzia asubuhi hadi kiza kuuingia wakati wa Maghrib.

Wafanyabiashara wa uwanja walikuwa hawarudi na bidhaa nyumbani ila wameuza zote kwa barka iliyokuwapo mahali pale na ndipo likaja jina ''kitchwele,'' yaani hadi jua lichwe ndiyo wanafungasha kurudi nyumbani na hapo wameshauza kila kitu chao kabla ya kutua jua.

Hapo kwenye uwanja huo palikuwa na madras akisomesha Sheikh Omari Mtiro na inaaminika ni kutokana na Qur'an iliyokuwa ikisomeshwa pale ndipo Allah akatia baraka mahali pale.

Sheikh Hassan bin Amir na yeye alipata pia kusomesha pale katika miaka ya 1940.

Hivi ndivyo hii barabara mbele ya uwanja huu ilivyopata jina na kuitwa Kitchwele.

Turudi nyuma Kitchwele na New Street tunaelekea Morogoro Road kwenye ofisi ya Tanganyika African Association.

Kama nilivyotangulia kusema ni kuanzia hapa Kitchwele na New Street ndipo unaanza kukutana na nyumba pande zote mbili za Barabara kuanzia Mtaa wa Aggrey.

Kwenye kona ya Kitcwele na New Street kushoto sisi tunapata akili tumekuta pale kuna hoteli ya Muhindi anaitwa Mamu na hoteli hii ikawa inajulikana kwa jina la Kwa Mamu,

Hii hoteli ilikuwa kwa watu wa hali ya chini ikipika ugali kwa utumbo na ilikuwa hoteli maarufu sana kwani utumbo ule ulikuwa ukipikwa kwa ustadi mkubwa ukiwa mchuzi chukuchuku uliokolea ndimi na pilipili.

Sasa ilipokuwa hoteli hii ikajengwa ofisi ya NUTA mwanzoni au katikati ya miaka ya 1960 baada ya serikali kupiga marufuku vyama huru cha wafanyakazi na kuwaweka kizuizini viongozi wake mwaka wa 1964.

Mmoja wa viongozi hao alikuwa babu yangu Rais wa Tanganyika Railways African Union (TRAU) Katibu akiwa Kassanga Tumbo.

Mbele ya Kwa Mamu ndipo lilipo jengo la Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Jumuiya ya Waislam wa Tanganyika) iliyoasisiwa mwaka wa 1933 na Kleist Sykes na wenzake akina Ali Jumbe Kiro, Iddi Tosiri, Shariff Salim bin Omar Attas, Sheikh Ali Saleh, Mzee bin Sudi kwa kuwataja wachache.

Endeleeni kukamata haya majina kwani ni muhimu sana katika historia ya Tanganyika.

Pamoja na ofisi ya Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ilikuwapo shule ambayo wazee wetu walianza kusoma hapo miaka ya 1930 elimu ya dini na sekula.

Al Jamiattul Islamiyya Fi Tanganyika ilikuja kupigwa marufuku mwaka wa 1968 serikali ilipounda BAKWATA.

Hapo jengo la Al Jamiatul Islamiyya mlango wa pembeni yake uko Stanley Street kupandisha juu utakutana na Mtaa wa Sikukuu ilipokuwa nyumba ya Kleist Sykes na baada ya kufariki Abdul Sykes akawa hapo.

Nyuma hii ina historia kubwa sana kwani hapa ndipo mipango yote ya kuunda TANU ilipokuwa ikifanyika ukiachilia mbali kuwa Nyerere aliishi hapo baada ya kujiuzulu kazi ya ualimu Pugu mwaka wa 1955.

Mbele ukielekea mtaa wa Swahili kushoto alikuwa akiishi Tewa Said Tewa na mbele kabisa Stanley inapokutana na Congo ilikuwa nyumba ya Max Mbwana.

Mbele ya Stanley ni Mtaa wa Mchikichi ambako kulikuwa na nyumba ya Mama Sakina Bi. Chiku bint Said Kisusa, mke wa Shariff Abdallah Attas.

Tunaingia Mtaa wa Mkunguni na New Street kushoto ilikuwapo nyumba akikaa Bi. Hawa bint Maftah (mmoja wa akina mama wahamasishaji wananchi kujiunga na TANU kwa nyimbo za lelemama akiwa na Bi. Titi Mohamed) na jirani ya hapo nyumba ya Iddi Tosiri mwanachama wa African Association baadae (TAA) na pia mwanachama wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika na mwanachama shupavu wa TANU na TAPA (Tanganyika African Parents Association).

Tumefika mtaa wa Kariakoo na Sikukuu hapo ndipo ilipokuwa ofisi kuu ya TAA na ndipo ilipokuja kuundwa TANU mwaka wa 1954.

Ofisi hii ilijengwa kati ya mwaka wa 1929 na 1933 ikawa imekamilika na kufunguliwa na Gavana Ronald Cameron.

Kwa mkono wa kulia baada ya ofisi ya TAA kwa mbele kidogo Abbas Sykes siku hizo kijana mdogo alikuwa na nyumba inaangalia Mtaa wa Amani.

Sasa turejee pale tulipoanza kwenye Jumba la Elimu ya Watu Wazima.

Mimi na watu wengi tukiamini kuwa kiwanja kile ilipojengwa nyumba ile kilikuwa cha John Rupia na yeye akawapa TANU baada ya uhuru ili pajengwe chuo kikuu.

Siku moja niko katika mazungumzo na mmoja wa watoto wa Mzee Rupia nikaleta historia hii.

Kwa mshangao mkubwa akaniambia kuwa kile kiwanja TANU walikitaka lakini waliona ikiwa wakatakiomba wao kama chama cha siasa wakoloni hawatawapa kwa hiyo wakamuomba John Rupia akiombe yeye na TANU wakatoa fedha za kiwanja.

Mzee Rupia alipewa kiwanja kile ambacha baada ya uhuru akarejesha amana kwa wenyewe na baada ya uhuru TANU ikaanzisha Chuo Kikuu katika jengo hili.


********************************************************************
Msomaji utasoma jina la mtu lakini hujui nini mchango wake kwa uhakika katika historia ya TANU na kudai uhuru.

Ingia hapo chini na nenda kwenye ''tafuta,'' na andiika jina lake utasoma historia yake hapo:

mohamedsaidsalum.blogspot.com
 
Kitandu,
Hutaka sana kuandika wastani lakini hii historia ni ndefu sana.
Mtaniwia radhi wasomaji wangu.
usijali ni nzuri sana kwa sababu ukiwa unasoma unakumbukia mitaa ile unajikuta kuwa unahitaji muda wa kuisoma vizuri
Hiyo mitaa nimekatiza sana nilivyokuwa nakula nauli halafu natembea kukatiza hiyo mitaa
 
Unamkumbuka Sheikh Makwa alikuwa mwana tariqa na imam wa msikti wa kipata street, mbona watu wa dini hamuwakumbuki
Tafadhali tungependa picha zaidi za zamani za hhiyo mitaa uliyoisema, sababu niliishi kipat nikiwa mdogo karbu na mzee Mwamba Seif miaka ya 70
 
Kama mzee una picha za mtaa wa kipata wa zamani zipost please au hata mitaa mingine k. Lindi, Kiungani (gogo vivu) Somali kwa kina Marijani Rajabu, Mbaruku..n.k. We need old photos pls
 
Kama mzee una picha za mtaa wa kipata wa zamani zipost please au hata mitaa mingine k. Lindi, Kiungani (gogo vivu) Somali kwa kina Marijani Rajabu, Mbaruku..n.k. We need old photos pls
Dalla...
Nimezaliwa nyumba ya pili baada ya hiyo nyumba nyeupe kushoto mwaka wa 1952 lakini haikuwa kama hivyo nyumba imepboreshwa kidogo.

1727363236264.jpeg

Mtaa wa Kipata (sasa Kleist Sykes) 1970s​
 
Back
Top Bottom