Mdukuzi,
Soma makala hii hapo chini inayohusu ugaidi:
''Sheikh Rajab Ramadhani Chambuso ni katika vijana wadogo wa Tanga niliopata kusubiana naye kwa kipindi cha miaka 15 niliyoishi Tanga.
Nilifahamiana pia na mwenzake Ahmada Kidege ambao wote wakishughulika na kusomesha Uislam.
Sheikh Chambuso yeye ndiye alikuwa karibu na mimi zaidi.
Nilimjua kama mwalimu wa Islamic Knowledge akipita shule za sekondari akisomesha wanafunzi wa Kiislam elimu ya dini yao.
Kabla hatujafahamiana vizuri tulikuwa tukipishana alfajr tukifanya mazoezi ya kukimbia Barabara ya Bombo.
Nakumbuka kumuona akitembea kwa miguu shule moja baada ya nyingine jasho likimtoka kwenda kuwahi kipindi mimi nikiwa katika gari yangu na kiyoyozi kinaunguruma.
Wakati ule sikuwa sana karibu na yeye lakini nilipokuja kumzoea nikajafahamu kuwa anasomesha kote mjini na nje ya mji kwa kujitolea.
Haukupita muda alinunuliwa baiskeli na muhisani aliyeguswa na juhudi ile ya kijana mdogo kujitolea kuwasomesha watoto dini ya Allah bila ya malipo yoyote yeye akitegemea radhi za Allah.
Huu ukawa pia ni mwanzo wa uhusiano wangu na Sheikh Chambuso ikawa na mimi kwa namna yangu nasoma kwake kila tunapokuwa pamoja katika mazungumzo ya kawaida tu.
Ukiwa karibu ya waridi hukosi kunukia.
Sheikh Chambuso akanisoemsha historia ya Tanga na taasisi zake kubwa za Uislam kama Shamsiyya, Zahrau na Maawal Islam na baadae Shamsi Maarif ilipokuja kuanzishwa wakati mimi bado nipo Tanga.
Sheikh Chambuso ni kijana maarufu mjini kwa ile heshima yake ya kumtumika Allah na waja wake.
Wanafunzi waliopita mikononi mwake kuwasomeshsa hawana idadi.
Kupitia Sheikh Chambuso na mimi rafiki na nduguye nikawa nasafiria nyota yake nikifahamika kama ‘’rafiki yake Chambuso.’’
Sheikh Chambuso hakutosheka na kuwa anapita kwenye shule kusomesha akawa sasa anaingia hadi kufanya ushauri kwa wanafunzi wa Kiislam katika wale aliokuwa akiwasomesha dini masomo gani wachukue kwa ajili ya mstakbali wao wa baadae.
Hapa ikawa sasa Sheikh Chambuso anaingia katika anga ambayo kwa hakika ilikuja kuwanufaisha vijana wengi na wengi wao wakafanikiwa.
Lakini kubwa lililokuja kunifurahisha ni pale alipoamua yeye na wenzake kuanzisha shule ya chekechea ya Kiislam na kuanza shule ya msingi.
Sasa tena Sheikh Chambuso akawa anaongeza ulezi juu ya kusomesha.
Madrasa yake na shule ya chekechea ikawa imejaa pomoni.
Mimi binafsi furaha yangu ilikuwa haina kifani.
Sheikh Chambuso akaongeza na ‘’idara,’’ nyingine siyo rasmi akawa anapita kwa Waislam kuwaomba kuwasomesha katika shule yake watoto mayatima na wale ambao wazazi wao Allah amewapa mtihani wa kipato.
Haikuwa ajabu kumuona Sheikh Chambuso amafatana na daktari kumpeleka katika nyumba ili amtie suna mwanafunzi wake ambae kwa shida za umasikini kapita umri wa kutiwa suna.
Huwezi kummaliza Sheikh Chambuso.
Siku moja baada ya kutoka Tanga kwa kustaafu kazi nilirudi Tanga na nikenda kumtembelea Sheikh Chambuso shuleni kwake. Ile kuniona tu na baada ya kusalimiana ghafla akasimamisha masomo katika madarasa akawatoa wanafunzi wote nje ya wakapanga mstari ili wanisalimie.
Sheikh Chambuso alikuwa anazugumza na ule mkusanyiko kwa Kiarabu.
Niliyoshuhudia pale niliinamisha kichwa changu chini sikuweza kujizuia.
Machozi yalinilengalenga.
Kumbe mambo haya yanawezekana…
Lakini kuutumikia Uislam una changamoto zake hasa nyakati hizi za ''siasa za ugaidi.''
Haukupita muda Sheikh Chambuso akakamatwa na kuwekwa rumande kwa kesi ya ‘’kushawishi mauaji,’’ akawekwa ndani rumande Handeni majuma mawili.
Kapelekwa Handeni kafungwa kitambaa cheusi usoni huku yuko chini ya ulinzi mkali.
Sheikh Chambuso hana sifa ya uovu mimi binafsi na kila aliyesikia habari hizi alisikitika na kushangaa.
Hii ilikuwa kesi ya kubambikizwa kama ilivyokuja kudhihirika hapo baadae.
Siku ya pili yake zilipopatikana taarifa kuwa Sheikh Chambuso kakamatwa mji mzima wa Tanga ulizizima kwani ni nani asiyemjua Sheikh Chambuso mwalimu na mlezi wa watoto wao?
Ule msururu wa ingia toka nyumbani kwake kuanzia alfajir kuna baadhi ya watu walidhani nyumbani kwake kuna msiba kafa mtu.
Sheikh Chambuso alihangaishwa sana na kesi hii ambayo alinifahamisha kuwa polisi wanaiita, ''kumfunga mtu paka mweusi shingoni.''
Sheikh Chambuso mwenyewe alikuja kunambia kuwa ile kesi imemfunza mengi na imemuongezea elimu ambayo asingeweza kuipata popote.
Kwangu mimi ikawa sasa Sheikh Chambuso kawa shule na mwalimu pia na mimi nasoma kwake na kujifunza.
Hii ilipelekea mimi kuandika mengi kuhusu madhila mengi yanayowakabili Waislam kiasi nilimakaribisha msikiti kwetu aje kuzungumza na Waislam na nilimwekea ukurasa makhsusi kwa ajili yake katika kipindi chote alichokuwa mahakamani kujibu tuhuma za ''kushawishi mauaji:''
Ukurasa huu wa Sheikh Chambuso ulisomwa na watu wengi sana na ulikuwa na taarifa nyingi za uchunguzi kwa kuhusu ukweli wa tuhuma za ugaidi dhidi ya Waislam.
Huwa kila akija Dar es Salaam basi Sheikh Chambuso atanipitia kwangu kunijulia hali na kunieleza shule inavyokwenda na taarifa nyingine za vijana wa Kiislam Mkoani Tanga.
Mara ya mwisho nilipokutananae nilimuuliza kuhusu mwanafunzi wake mmoja bint nillitaka kujua maendeleo yake.
Sheikh Chambuso akaniambia, ‘’Yule bint anamaliza shahada yake ya Udaktari.’’
Kama nilivyotahadharisha hapo awali.
Kabla hatujaagana Sheikh Chambuso akanifahamisha kuwa wamefungua shule ya ushoni kwa wasichana inayoongozwa na Sheikh Khamisi Shemtoi ambae yeye mwenyewe licha ya kuwa sheikh ni fundi cherahani bingwa.
Huwezi kummaliza Sheikh Chambuso na wenzake kila unapokutananao basi watakuwa na jema la kukueleza kukufurahisha.
Kubwa ninalofaidi kwa Shekh Chambuso ni kule kunifunza misemo ya Kiarabu ambayo imekuwa silaha yangu kubwa katika mijadala.
Mathalan siku moja tunazungumza jambo akanipa jibu kwanza kwa Kiarabu kisha akanifanyia tafasiri akasema, '' Ukiijua sababu inaondoa ajabu.''
Kuna mfano mmoja alinipa kueleza jambo lililovurugika na watu kujaribu kulirejesha kama lilivyokuwa hapa mwanzo.
Akanambia, ''Sheikh Mohamed chukua mfano wa kioo kishavunjika na wewe ukajaribu kukiunga, hakiwezi kuwa kama kilivyokuwa hapo mwanzoni. Ukijitazama na kioo hicho utaiona tofauti.''
Sheikh Chambuso anasema yeye misemo hii kafundishwa na Sheikh wake Marehemu Sheikh Mohamed Ayub.
Siku moja tulikuwa katika gari yangu nikaweka CD ya Sheikh Mohamed Ayub anadarsisha tafsir ya Qur'an darsa za L'Asr Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Msomaji kasoma aya mbili tatu kamaliza Sheikh Mohamed Ayub anaanza kusomesha.
Nikamuona Sheikh Chambuso ghafla uso umembadilika kajiinamia akanambia, ''Sheikh Mohamed mimi hapo nipo sisi wanafunzi wadogo tuko safa ya nyuma mbele pale namuona sheikh mwenyewe kazungukwa na wanafunzi wake wakubwa ambao ndiyo walikuwa walimu wetu sisi, Sheikh Mohamed Bakari, Sharif Sayydid Hussein, Sheikh Zuher bin Ali bin Hemed bin Al Buhry...''
Sheikh Chambuso hakika ni kijana hazina kwa watu wa Tanga kwa usomi wake makini na jinsi anavyojibiidisha kutumikia jamii.
Ijaza yake katika haya yote ilikuwa kufunguliwa kesi ya kubambikizwa kuwa ''anashawishi mauaji.''
View attachment 2111918
| Sheikh Ramadhani Rajab Chambuso akigawa mashafu tafasiri ya Sheikh Ali Muhsin Barwani kwa wanafunzi wake St. Christina Secondary School Tanga Picha ilipigwa 2006 wakati akiwa Sheikh na Mwalimu ''mtoto.'' |