MKATABA WA UJENZI KIWANDA KIKUBWA CHA SUKARI WASAINIWA SONGEA
MKATABA wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha sukari chenye thamani ya shilingi bilioni 500 ambacho kinajengwa katika Kijiji cha Magwamila Kata ya Lilai Muhukuru wilayani Songea mkoani Ruvuma umesainiwa kwenye ukumbi wa Mkuu wa Wilaya Songea Januari 23,2024.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile amesema mkataba huo ni makubaliano ya awali baina ya viongozi wa Kijiji cha Magwamila na wawakilishi wa Songea Sugar Limited ambayo ni tawi la kiwanda cha Kagera Sugar ambao hivi sasa wamewekeza nchini Uganda na wameamua kuanzisha tawi la kiwanda hicho mkoani Ruvuma .
βMkataba umeshuhudiwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na wawakilishi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania Kanda ya Nyanda za Juu Kusini chenye makao makuu yake jijini Mbeyaββ.alisisitiza DC Ndile.
Ndile amewataka wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kujiandaa kuupokea uwekezaji wa kiwanda kikubwa cha sukari katika Katika Kijiji cha Magwamila.
Amesisitiza kuwa wawekezaji hao wanatarajia kuweka zaidi ya bilioni 500 katika kiwanda hicho, ambapo kiwanda kitazalisha tani zaidi ya laki moja kwa mwaka.
Ameongeza kuwa kiwanda hicho kitaweza kuzalisha umeme ambao utaweza kuuzwa kwenye grid ya Taifa, pia kitazalisha mafuta aina ya ethane ambapo amesema kuwepo kwa kiwanda hicho kitaleta manufaa makubwa katika wilaya ya Songe ana Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Kwa upande wake Mchumi Mwandamizi wa Bodi ya Sukari Tanzania Joshua Mhando ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.