Kama gari ina tairi mbovu, gia zisizofanya kazi vizuri, breki zisizo madhubuti, taa haziwaki, je haya ni makosa tofauti?

figganigga

JF-Expert Member
Joined
Oct 17, 2010
Posts
25,724
Reaction score
55,906
IWAPO GARI IMEKUTWA NA TAIRI MBOVU, GIA ZISIZOFANYA KAZI VIZURI, BREKI ZISIZO MADHUBUTI, TAA HAZIWAKI NA BODI LIMECHAKAA, JE HAYA NI MAKOSA MATANO (5) TOFAUTI, KIASI KWAMBA ANATAKIWA KULIPA 150,000*?

Kisheria, jibu ni Hapana. Ila kipolisipolisi linaweza kuwa Ndio.

Sheria ya Usalama Barabarani, yaani The Road Traffic Act, sura ya 168 inajibu swali hili kupitia kifungu cha 39(1) (a) &(b) na 39(5) kinajibu swali hili.

*Kifungu cha 39(1): Hali ya gari kwa matumizi ya barabarani*

Kwa mujibu wa kifungu cha 39(1) ni marufuku kwa gari lolote kutumika barabarani, iwapo gari au tela hilo na sehemu zake na vifaa vyake, ikiwemo chesesi yake, injini, mfumo wa gia, mfumo wa breki, bodi au sehemu za bodi, tairi na taa zake,

(a) Havipo katika hali nzuri na vinafanya kazi vizuri, na vipo katika hali ambayo uendeshaji wa gari barabarani mchana au usiku, hauwezi kuwa hatari kwa watu wanaosafiri na gari au tela hilo au kwa watumiaji wengine wa barabara;

(b) Vinazingatia matakwa yote na maelekezo kadiri yalivyo kwenye kanuni.

*Kifungu cha 39(5)*: Adhabu kwa makosa ya ubovu wa gari

Mtu yeyote takayetumia gari barabarani kinyume na matakwa ya kifungu kidogo cha 1,2, au 3 atakuwa anatenda kosa na akitiwa hatiani, kwa mara ya kwanza atalipa faini isiyopungua shilingi 20,000, na kwa mara ya pili faini isiyopungua shilingi 30,000 na kwa mara ya tatu na nyingine zinazofuata, faini isiyopungua shilingi 50,000 au kifungu cha miaka 3 jela au vyote kwa pamoja.

*Maana yake ni nini?*
Maana yake ni kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 39(1) kosa linalohusisha tairi mbovu, gia kutofanya kazi, breki, taa, na bodi, ni kosa moja tu linaloitwa *hali ya gari kutumika barabarani* au kwa lugha nyepesi ni *kosa la ubovu wa gari*. Hivyo ndio kusema, vitu vyote vilivyoorodheshwa hapo juu kwenye kifungu cha 39(1) ni viashiria au ushahidi tu wa ubovu wa gari au gari kutofaa kwa matumizi ya barabarani.

Na ndio sababu kifungu cha 39(5) hakisemi “Any person who uses on a road a motor vehicle or trailer in contravention of the provisions of subsections (1), (2) or (3) shall *for each item listed in subsection 1 above, be guilty of an offence…* bali kinasema *Any person who uses on a road a motor vehicle or trailer in contravention of the provisions of subsections (1), (2) or (3) shall be guilty of an offence*.

*Kwa hiyo basi*, kisheria sio sahihi kumuandikia mhusika makosa matano kwa ubovu wa vitu vilivyoainishwa chini ya kifungu cha 39(1) cha sheria ya usalama barabarani. Makosa yote hayo yatahesabika kama kosa moja tu la ubovu wa gari na mtu atatakiwa kulipa adhabu ya papo kwa papo ya shilingi 30,000. Faini hii haijalishi una ubovu wa kitu kimoja au vitu vitano ni hiyo hiyo tu, hata ingekuwa bulb tu. Wakati kama mtu huyo huyo atapelekwa mahakamani basi akitiwa hatiani kama ndio kosa lake la kwanza atalipa shilingi 20,000; kosa la pili 30,000 na kosa la tatu shilingi 50,000.

*Kwa kuongezea*
Iwapo askari ataona gari husika lina ubovu wa zaidi ya kitu kimoja, basi (kwakuwa yeye si mtaalamu) hapo ndipo anapotakiwa kuchukua hatuza Zaidi kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 81(a),(b) na (i), yaani *kuamuru gari liende lipelekwe alipo mkaguzi wa magari (Vehicle Inspector) kwa ukaguzi Zaidi wa kina*. Ambapo gari likishafikishwa kwa VI, VI naye atatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kifungu cha 83 cha RTA, ambapo akijiridhisha na ubovu anaweza kuondoa namba za usajili na kulizuia kutembea barabarani hadi litakaporekebishwa.

Ni matumaini yangu umeongeza uelewa kuhusu makosa ya ubovu wa gari chini ya kifungu cha 39(1)

USALAMA BARABARANI NI JUKUMU LETU SOTE.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…