SoC01 Kama jukumu la kuitunza ndoa sio la mke peke yake, kwanini wanaume hawafanyiwi “kitchen party”?

SoC01 Kama jukumu la kuitunza ndoa sio la mke peke yake, kwanini wanaume hawafanyiwi “kitchen party”?

Stories of Change - 2021 Competition

Madamboss

Member
Joined
Sep 7, 2021
Posts
5
Reaction score
193
Habari zenu wanajamii forum? Leo nataka nigusie swala la ndoa hususani matayarisho yanayofanywa kabla ya kuingia huko.

Ndoa ni muungano wa mume na mke katika mwili na roho. Wawili hawa wanapokaa pamoja huunda familia. Lengo kuu kwenye ndoa huwa ni kuunda familia iliyo bora lakini changamoto nyingi hutokea katika kujaribu kufanikisha ilo. Ilikujiandaa kuzikabili changamoto hizi matayarisho hufanyika kabla ya kubeba jukumu hili. Imezoeleka kwenye jamii zetu kabla binti hajaolewa sherehe moja anayofanyiwa ni "kitchen party ".

Hii ni hafla iliyoandaliwa kwa ajili ya bi harusi. Mama wa bi harusi, na wanafamilia wa karibu wa kike ndo huusika katika kuandaa shughuli nzima. Wanawake hukusanyika na kumletea zawadi bi harusi. Na hii imekuwepo kwa kusudi la kumuelimisha na kumpa mwanga bibi harusi kabla hajayaanza maisha ya ndoa. Hii huwa siku maalumu kwa bi harusi mtarajiwa kuambiwa na kukumbushwa baadhi ya mambo ya msingi yatakayo mfanya kuwa mke bora na pia mama bora. Na mafunzo hayo hutoka kwa wanawake wenzie waliokwisha ingia kwenye ndoa.

Kitchen party imekuwa hafla maarufu kwa ajili ya bi harusi miaka ya hivi sasa. Lakini tokea zamani ilikuwa ikifanywa majumbani tofauti na hivi sasa ambapo inafanywa kwenye kumbi. Wanawake wanaoalikwa ni wajuzi katika swala zima la ndoa. Hivyo hutoa uzoefu wao wa ndoa na kumshauri bi harusi. Baadhi ya mambo ambayo bi harusi hukumbushwa au kufundishwa ni kujiheshimu, kuheshimu wengine, usafi wa mwili na nyumba, kutunza familia, kumridhisha mume chumbani, upishi bora, kuwa mnyenyekevu kwa mume, kujipendezesha na mengine kadhalika.

Zamani kulikuwa na jando na unyago katika jamii nyingi za kiafrika. Hizi zilikuwa ni shule ya malezi bora kwa vijana ambao walikuwa wanahama toka rika ya watoto kuwa watu wazima. Vijana walifundishwa maadili bora, kuwa wakamavu na kuwajibika katika majukumu ya kuitunza na kuilinda familia. Mabinti walifundishwa namna ya kujitunza, kutunza nyumba, watoto na pia walifundwa jinsi ya kufanya mapenzi na kumridhisha mume wakishaolewa. Jadi hizi zimeenda zinasahaulika pengine sababu ya mapungufu yaliokuwepo kama ukeketaji kwa watoto wa kike.

Je, mabwana harusi wa miaka ya sasa wanajifunza wapi mambo kama haya ya kuwa mume na baba bora katika familia?

Ustawi wa familia hutegemea pande zote mbili kufanya vizuri yaani mume na mke. Na kwenye jamii zetu ambapo kuna mfumo dume, mume akipewa jukumu la kuwa kichwa cha familia ni vizuri tukahakikisha anajiandaa vyema kwa ajili ya hilo. Kuwa kiongozi wa familia ni jambo kubwa kwani jamii yoyote huundwa na mkusanyiko wa familia nyingi. Hivyo familia bora , hutengeneza jamii iliyo bora. Na uwezo wa kuwa kiongozi bora kuna baadhi ya watu wanakuwa nao bila hata kufundishwa lakini sio wote wenye hii kalama. Na kwa sababu mume kwenye familia anakuwa moja kwa moja kiongozi mkuu wa familia ni muhimu akafahamu namna ya kuwa kiongozi bora. Kiongozi anatakiwa angaze mwanga ili kuonesha wafuasi wake wapi wapite kufikia malengo.

Baadhi ya mambo ambayo wanaume wanaokaribia kuingia kwenye ndoa wangeweza kukumbushwa.

Kuwa mume bora kwa mkewe
. Upendo wa hali ya juu unahitajika ili kuweza kuyavumilia mapungufu ya mwenza wako wa maisha. Pengine unaweza ukahisi unayajua mapungufu yake yote lakini jinsi unavyozidi kuishi na mtu ndo unazidi kujua mapungufu yake. Mfano halisi ni kugundulika kwa magonjwa sugu kwa mmoja ya wanandoa. Hili ni jambo zito ambalo linawakuta wengi lakini mapokezi yanatofautiana. Ni vizuri kujiandaa kimawazo kukabiliana na changamoto kama hizi kabla ya kuingia kwenye ndoa.

Migogoro katika ndoa haiepukiki. Lazima itatokea mpishane na mwenza wako katika kauli au vitendo. Lazima kuwe na namna bora ya utatuzi migogoro. Ni vyema kuhakikisha hakuna mwenye hasira kabla ya kutafuta jinsi ya kusuluhisha . Hii itasaidia kupunguza ukatili kwa wanawake na watoto unaofanywa majumbani. Mahusiano kati ya mume na mke huathiri tabia na maendeleo ya watoto. Watoto waliopo ndani ya familia ambazo wazazi hugombana mara kwa mara huishi na wasiwasi katika maisha yao ya kila siku. Hivyo wanakuwa hatarini kupata msongo wa mawazo na hata kupelekea kutofanya vizuri shuleni.

Kumtunza mke wake. Kuna tabia ya baadhi ya wanaume kuvutiwa na binti kisha wakaamua kuoa. Lakini wanashindwa kujituma ili mkeo huyo aendelea kupendeza kama walivyomkuta. Miili ya wanawake ni rahisi kubadilika na kuzeeka hasahasa kutokana na maswala ya uzazi. Hivyo ni muhimu kuweka juhudi zaidi katika muonekano mwanamke anapokwishaolewa. Ajabu ni kwamba utakuta mume anamnyima mke wake hela ya kujitengeneza ili avutie lakini atatoa hela na kumpa mchepuko. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba mwanandoa anapopendeza akasifiwa na mtu wa nje, sifa kuu hurudi kwa mwenza wake.

Tatizo la ukosefu wa watoto kwenye ndoa. Kuna wanaume wengi ambao hawatoi ushirikiano katika kutafuta utatuzi na badala yake huweka hitaji la kuoa mwanamke mwingine haraka. Pia kwa baadhi inakuwa changamoto pindi watoto wa jinsia moja tu ndo wakipatikana. Utulivu katika ndoa hukosekana panapokuwa na watoto wakike tu katika familia. Hii ni kutokana na dhana potofu kwa baadhii kuwa mtoto wa kiume ni bora kuliko wa kike. Hata hivyo wanaume wengine wanakuwa hawajui kuwa kibaiolojia jinsi ya mtoto hutambulika kutokana na aina ya mbegu kutoka kwao. Lakini swala la msingi ni utambuzi kwamba hakuna jinsia moja iliyo bora kuliko nyingine, na kwamba wanaume na wanawake wanapaswa kupewa fursa sawa.

Kuwa baba bora kwa wanawe. Ukibarikiwa kuwa mzazi ni jambo la kumshukuru muumba. Maana sio wote waopata hio nafasi. Lakini baraka hii inakuja na majukumu mengi. Kuwa baba bora sio tu kuhakikisha umeacha hela nyumbani kwa ajili ya mahitaji ya wanao. Baba bora anashiriki katika malezi ya mwanawe toka ikiwa mimba. Wababa wengine hawapo karibu na wanawe kufatilia maendeleo na mienendo yao. Jukumu lote wanambebesha mama. Na tatizo linapotokea msalaba unakuwa wa mama. Hio sio kitu vizuri. Inapendeza baba atakama ndo mtafutaji akatenga muda wakuwa na wanawe baada ya miangaiko yake. Na kuna muda inatokea mume anapata mtoto wa nje ya ndoa. Wahenga walisema kitanda hakizai haramu. Sio sawa kutelekeza au kukana damu yako. Mwanaume anatakiwa awe tayari kifikra kwamba jambo kama hili litakapo tokea atawajibika kama mzazi wa huyu mtoto. Pia baadhi ya wababa wanakuwa wakali kupitiliza mpaka ukaribu mzuri na watoto unakosekana. Hisia za ukaribu na mshikamano unaundwa katika familia wanapotumia muda kuwa pamoja na kufanya mambo yanayowaleta karibu.

Kumpa bwana harusi zawadi zitakazomsaidia katika kutengeneza vitega uchumi. Pesa ni kitu muhimu kwenye maisha na kuwa mtafutaji mkuu wa familia sio kitu chepesi ukizingatia na gharama za maisha zilivyoongezeka ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Mfano mzuri ni ada za shule za watoto. Ukitaka watoto wapate elimu bora lazima upambane kama unakipato cha chini au wastani. Ingependeza bwana harusi akapewa zawadi za kumuwezesha kubeba hili jukumu kama anavyopewa bi harusi zawadi tofauti. Mfano wa zawadi ambazo bwana harusi angeweza kupewa ni mifugo ya biashara kama vifaranga vya kuku, frame ya duka, trekta na kadhalika. Haipendezi pesa nyingi ikitumika kwenye maandalizi ya harusi halafu baadae vyanzo vya mapato kwa wanandoa vikakosekana.

Kwa kuhitimisha, ukweli ni kwamba ndoa ni jukumu la mume na mke. Hivyo basi hamasa inayokuwepo katika kujiandaa na jambo hili inatakiwa iwe sawa kwa pande zote mbili. Hili jukumu la kuwaanda wanandoa watarajiwa halitakiwi kuachwa kwa kizazi chetu cha sasa au vijavyo. Na halitakiwi kufanywa na mitandao ya kijamii kama Instagram na Facebook. Hiki ni kitu muhimu sana kwa sababu kuna watu wamelelewa kwenye familia isiyo na misingi bora. Familia ambazo hazina amani, upendo, heshima, uvumilivu na mawasiliano. Kwahiyo, inakuwa ngumu kwenda kuyaishi yale ambayo hawajayazoea. Hivyo basi kuna umuhimu wa kukumbushia hata walau kwa uchache namna ya kulibeba jukumu la kuwa mume na baba bora kabla ya kuingia kwenye ndoa.
 
Upvote 8
Kama mwanaume anahitaji kufundishwa jinsi ya kuwa mume basi huyo bado hana sifa za kuwa mume. Mwanaume anayetaka kuoa inatakiwa awe ameshajijenga yeye mwenyewe. Katika kujijenga huko atakuwa amepitia mengi ya kutosha ya kumuwezesha kujenga na kuusimamia mji wake.

Mwanaume ndo sheria ya mji wake. Kwa hiyo hahitaji kufundishwa chochote. Kile anachoamua yeye ndo sheria ya mji wake. Kumfundisha ni kuanza kumpangia Halmashauri ya Mji wake aiendeshe vipi, jambo ambalo ni kasoro kubwa sana kwa mtu anayetaka kuitwa "Mume" kupangiwa na watu wengine aendeshe vipi mji wake.

Mwanamke wewe jukumu lako ni kuchagua mji upi unakufaa, sio kujaribu kubadilisha kichwa cha mwenye mji.

Kama mwenye mji ni mbabe, basi ndo uende ukashike adabu na kuwa mpole na mnyenyekevu.

Kama ni zezeta, mtoto wa mama, au kizazi kipya cha wanaojiita wanaume lakini kila kitu kapewa na wazazi wake, hadi kazi katafutiwa, gari kanunuliwa, nyumba kajengewa au ya urithi, basi ndo ujiandae kwa mabadiliko makubwa huko mbeleni maana huyo bado ni mwanafunzi wa uanaume. Kwa hiyo unaweza ukajikuta unaishi katika mabadiliko makubwa kama akizinduka na kuamua kuwa mwanaume.

Wanaume hata wale zezeta au wale walioolewa na majimama mara nyingi mwisho wa siku huzinduka na kujitambua.
 
Back
Top Bottom