Ojuolegbha
JF-Expert Member
- Sep 6, 2020
- 1,278
- 797
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imehitimisha ziara muhimu nchini Comoro kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu juu ya mifumo bora ya ushirikishaji wa Diaspora katika maendeleo ya taifa. Katika ziara hiyo, Kamati ilikutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Visiwa vya Comoro ambapo walijadili masuala ya kidiplomasia, nafasi ya Diaspora katika kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, na umuhimu wa sera madhubuti zinazolenga kushirikisha Diaspora katika maendeleo ya taifa.
Mazungumzo muhimu pia yalifanyika na Kamisheni ya Diaspora ya Comoro, ambapo Kamati ilijifunza kuhusu majukumu ya kamisheni hiyo, mafanikio yake katika kuimarisha mchango wa Diaspora kwa uchumi wa taifa hilo, na namna mifano hiyo inaweza kutumika kuboresha mfumo wa Tanzania. Uzoefu huu unatoa msingi imara kwa maboresho ya kitaasisi, sera, na sheria nchini Tanzania, ikiwemo hatua za kuleta Hadhi Maalum kwa Watanzania wenye uraia wa nchi nyingine.
Kamati pia ilikutana na Kampuni ya Aden, inayomilikiwa na Diaspora mwenye asili ya Tanzania. Kampuni hiyo imekuwa mfano wa mafanikio, ikichangia ajira, huduma za kijamii, na uwekezaji unaochochea maendeleo. Mafanikio haya yanaonesha umuhimu wa kuwawezesha Diaspora kupitia sera na sheria zinazotambua mchango wao kwa taifa.
Ziara hii ni hatua muhimu kuelekea kutolewa Hadhi Maalum kwa Raia wa Nchi nyingine wenye Asili ya Tanzania, kwa kupitia maboresho ya sheria kama vile Sheria ya Ardhi Sura ya 113 na Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54. Hatua hizi zitasaidia kuimarisha mchango wa Diaspora katika uchumi wa taifa, uwekezaji, na maendeleo ya kijamii kupitia mifumo inayowezesha ushiriki wao kikamilifu.
Tanzania inajifunza, kuboresha, na kuimarisha mahusiano ya kimataifa kupitia uzoefu wa nchi rafiki kwa maslahi ya taifa.