simaye
JF-Expert Member
- Nov 5, 2010
- 426
- 214
kuundwa kwa kamati kwa ajili ya kuchunguza sababu za wanafunzi wengi kufeli ni kama upeo mdogo wa kufikiri na kutoona mbali kwa serikali yetu. Ukweli wa kufeli kwa wanafunzi uko wazi kabisa na wala hauhitaji elimu ya digrii ili ujue kama wanavyotaka kutwaminisha hawa viongozi wetu. Licha ya mgomo wa walimu kutajwa kuwa ndio sababu nafikiri hayo ni mawazo mepesi kabisa ambayo kiuhalisia huwa na majibu mepesi(majawabu kama alivyowahi kusema rais wa chama cha walimu Tanzania).Tanzani hapa tulipofikia ni pabaya zaidi kwa sababu masuala muhimu na ya msingi tumekuwa tukiyajibu kisiasa.Kati ya mambo magumu ambayo hayahitaji kjibiwa kisiasa ni mustakabali wa Taifa la Tanzania kwa miaka mingi ijayo ambao unaweza kujengwa tu endapo elimu itapewa kipaumbele., Zipo sababu nyingi za wanafunzi kufeli, kwa kusaidia baadhi na kubwa na hizi hapa; 1. mfumo wa utungaji wa maswali na usahihishaji wake una walakini kwa sababa kwa muda wa miaka yote minne mwanafunzi anatakiwa kupimwa na maendeleo ya ujifunzaji wake hupelekwa baraza( necta) kwa ajili ya kuunganishwa na matokeo yake ya mitihani ambayo kwa kawaida ni 50% na mtihani wa mwisho ni 50% . Sasa swali hapa ni je, baraza huwa linaunganisha na matokeo hayo au huwa wanampima kwa mtihani tu huo anaoufanya mimi sijui na kama tume inaenda kuchunguz hili nitaiunga mkono 2.Mitaala na maswali ya mtihani. Kwanza niweke wazi kuwa hakuna mtaala rasmi wa elimu nchini japo wapo wanaodai kuwa ipo. Mimi najua tu mihtasari kwa hiyo walimu wengi wnatumia mihtasari ambayo ndio maelekezo ya nini wanapaswa kufundisha katika kipindi chote cha ujifunzaji wa wanafunzi katika ngazi husika ya elimu;awali, msingi, sekondari na vyuo. 3 Maudhui ya mihtasari na vitabu vya kufundishia na kujifunzia. Hili ni tatizo kubwa kwani miongozo iliyotolewa na vitabu haviendani kabisa. kwa hili baadhi ya walimu wanatumia uzoefu katika ufundishaji kwa sababu vitabu vya kufundishia hakuna kwa hivyo wanafundisha kwa sababu wanaingia madarasani. 4. Lugha ya kufundishia na kujifunzia . Katika elimu ya sekondari lugha inachangia kwa asilimia kubwa sana kwa sababu maswali yanatungwa kwa kutumia kiingereza kigumu mno na hili hufanywa makusudi kwa ajili ya kuwakomoa watahininiwa .Misamiati mingi inayotumika katika utungaji wa mitihani ni migumu kiasi cha kuwafanya wanafunzi hasa wanasoma katika shule za kata ambao muda mwingi wanajifunza kwa kutafsiri kutoka lugha mama kwenda kiswahili na baadaye kuandika kwa kiingereza kupata tabu kugundua maudhui ya maswali katika lugha ya kiingereza. Ni muhimu kujua kuwa lugha ya kiingereza ni ngumu kwani wengi wetu hatuitumii kila siku kwa hiyo kuandika swali kwa kiingereza kigumu ili mwanafunzi ashindwe ni kutomtendea haki maana katika mtihani hawaruhusiwi kuingia na kamusi. 5. Madai ya walimu. Walimu wengi sasa hivi hawafanyi kazi kwa moyo wa kujituma kwa sababu kazi hii haiwalipi kabisa. Maslahi wanayopata walimu kwa kaweli hayalingani na kazi wanayofanya ya kuandaa watu makini kwa ajili ya kulitumikia Taifa kwa nidhamu, uadilifu na uaminifu wa hali ya juu kabisa.Walimu wanaingia kazini saa 12.00 asubuhi na anatakiwa kurudi saa 9.30 alasiri. Kwa mazingira ya shule zote za serikali muda wote huu anakaa bila hata chai wala chakula cha mchana na afundishe, nguvu atakuwa nazo toka wapi. Baya zaidi wengi wa walimu wanaishi katika nyumba za kupanga zilizo mbali na shule, hivyo kuwasukuma kuondoka kazini kuanzia saa 5;00 kwa ajili ya kwenda kupata angalau chai na huko yanayotokea mengi maana akikuta hakuna hawezi kurudi inabidi aendelee kukaa nyumbani ili kutafuta uwezekano wa kula yake ya siku. 6. Mazingira ya kazi ya ualimu. mazingira ya shule nyingi za serikali nchini Tanzania hayanaa mvuto kulinganisha na kazi yenyewe. Mwalimu anatakiwa kuwa na meza, kiti, ofisi nzuri na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kumwezesha kufundisha kwa utulivu. Bahati mbaya haya hayapo maana walimu wengi na hasa shule za serikali hawana hata meza za kukali na wakipata ni mbovu na muda mwingine anakaa kwenye madawati ya kukalia wanafunzi, hii inamvunja moyo sana maana hawezi kukaa katika hali hii kwa muda mrefu. Mwalimu anahitaji kiti na meza nzuri ili aweze kukaa bila kuumiza mgongo wakati wa maandalizi na mapitio ya kazi za wanafunzi. 7. kazi ya ualimu kuwa wito. Hii ni sababu nyingine inayofanya hata baadhi ya walimu kutofanya kazi kwa moyo. Wanasiasa wengi na pengine baadhi ya wasomi wanataka kuaminisha umma kuwa kazi ya ualimu ni wito. Hakuna kazi ya wito hapa duniani labda iwe umeamua kuifanya kwa ajili ya kutoa msaada. Waalimu wote wamesomea ualimu kwa muda wa miaka miwili , mitatu, miinne na kuendelea.wamesomea kwa ajili ya kuifanya ili iwalipe na wafanye shughuli zao za kujiendeleza kimaisha na familia zao .Sasa Taifa linapoamua kuja na nadharia ya wito hapa watakaoingia ni watu ambao wamekosa kazi za kufanya na hivyo wanaingia katika kazi ya ualimu kama njia ya kupitia kwa ajili ya kutimiza malengo yao na wakiingia tu wanatumia muda mwinigi kutafuta njia nyingine ya kupata kazi nzuri na wakipata wanaachana na ualimu mara moja na ndio maana walimu hawaji kutosha nchi hii. Sekta ya elimu kiukweli inahitaji mabadiliko makubwa ili kuweza kuifanya muhimu na kiwanda pekee cha kuzalisha wataalamu watakaokuwa na ujuzi wa kutosha wa kuliendesha Taifa hili ili lifanane na mataifa mengine yaliyoendelea. Hakuna taifa lililoendelea kwa kuwekeza katika siasa kama tanzania inavyojaribu kujengwa. Marupurupu makubwa wapewe walimu ili waweze hata kununulia nyenzo za kufundishia kama kompyuta na vitabu na kama haya hayatafanyiwa kazi basi tusitegemee mabadiliko yoyote katika elimu!!
...................Tafakuri njema.......................
mwalimu wa walimu.
...................Tafakuri njema.......................
mwalimu wa walimu.