The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Katika maeneo mengi, changamoto ya ukusanyaji wa taka imeendelea kuwa kilio cha wananchi. Magari ya kukusanya taka ama hayafiki kabisa au hufika mara chache sana, huku wakazi wakilazimika kutoa michango kwa huduma ambazo hazitolewi ipasavyo. Hali hii si tu inahatarisha afya za watu bali pia inavuruga imani ya wananchi kwa viongozi wao wa mtaa.
Suala lingine ni kwamba, unapokosekana utaratibu mzuri wa kushughulikia taka, huwa zinaishia kujaa mitaani, kuziba mitaro, na kuharibu mandhari za mitaa na wakati mwingine kuleta magonjwa ya mlipuko. Lakini pia, uchomaji holela wa taka huongeza hewa chafu yenye sumu ambayo inahatarisha afya za wakazi kwa magonjwa kama pumu na saratani. Kuna baadhi ya mitaa majalala yanafuka moshi masaa 24. Kuna mitaa watu wanachoma matairi kuvuna nyaya na moshi unaathiri watu.
Je, haudhani kuwa kiongozi anayewania nafasi katika mtaa wako anapaswa kujua changamoto hizi na namna ya kuzitatua?
Lakini pia, unapaswa kujiuliza na kuona kama mtaa/eneo lako lina miti ya kutosha na kiongozi unayeenda kumpigia kura Novemba 27 ana mikakati gani kuhusu upandaji wa miti na utunzaji wake katika eneo hilo. Ni vema kujua kuhusu mipango yake ya katua changamoto ya kukata miti kiholela au kuvamia misitu. Haya yote ni muhimu kufuatilia kwani miti ni uhai wa mazingira yetu. Inaongeza hewa safi, inapunguza joto, inazuia mmomonyoko wa udongo, na inaboresha mandhari za maeneo yetu.
Haya ni machache tu ambayo yanamgusa kila mmoja kwenye suala zima la mazingira. Kwahivyo basi, kabla haijafika Novemba 27, ni vema ukawa na majibu kutoka kwa wagombea wa eneo lako. Namna bora ni kuhudhuria mikutano kila unapoweza na kuhoji maswali ya msingi.
Kila la kheri!