Katiba Mpya huenda ikawa tiba ya magonjwa mengi yanayoikabili nchi

Katiba Mpya huenda ikawa tiba ya magonjwa mengi yanayoikabili nchi

drclark

Member
Joined
Feb 10, 2016
Posts
57
Reaction score
12
Novemba 4 mwaka huu Rais John Pombe Magufuli alikutana na wahariri Ikulu jijini Dar es Salaam. Miongoni mwa maswali aliyoulizwa lilikuwamo la mchakato wa kupatikana Katiba Mpya. Rais alijibu kwamba hakuna pahali alipoahidi kuwa atauendeleza mchakato huo.

Pengine Rais alisahau, lakini wachunguzi wa mambo wamebainisha kuwa ahadi hiyo imo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 ibara ya 144 kifungu (e) ambayo inaeleza kuwa CCM itakapoingia madarakani itamalizia mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.

Aidha, Juni mwaka huu Rais Magufuli alipopokea taarifa ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana aliahidi kuendeleza mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya na kwamba atahakikisha inapatikana Katiba inayotakiwa na wananchi. Aliwaeleza wananchi kwamba kama wanayo maoni mengine yakifikishwa serikalini, yataongezewa kwenye mchakato huo.

Kutokana na kauli hiyo, wadau wakajipanga upya na kutoa mapendekezo kadhaa ya maboresho wanayotaka yaingizwe kwenye Katiba inayopendekezwa. Mapendekezo hayo ni mawaziri wasitokane na wabunge ili kuondoa mgongano wa kimaslahi, Jaji Mkuu athibitishwe na Bunge ili kupunguza madaraka ya Rais na mambo mengine mbalimbali.

Wadau waliona kwamba kama mchakato utaruhusu kuongezwa maoni ya wananchi ina maana kwamba mchakato huo utarudi katika hatua ya kuratibu maoni ya wananchi na kuijadili upya Rasimu ya Kwanza iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Hivyo ndiyo kusema kuwa mchakato huo utaanzia mahali pazuri na huenda maoni ya wananchi yakapata nafasi.

Tunaamini kwamba kama Katiba Mpya itapatikana, kazi ya kusafisha nchi aliyoianza Rais itakuwa rahisi kwa sababu itakuwa imeiweka sawa mifumo ya uendeshaji nchi kwa ajili ya kukabiliana na mazingira ya sasa na ya baadaye.

Katiba hiyo inayopendekezwa inakadiriwa kuwa itaweza kuiongoza Tanzania kwa miaka 50 ijayo, hivyo itaweka misingi bora ya uongozi na mfumo imara wa utawala.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliwahi kusema kuwa nchi haiwezi kuwa na mabadiliko ya kweli kama miiko na maadili ya viongozi havitaingizwa kwenye Katiba Mpya na kwamba kero nyingi zilizopo zitapungua iwapo Katiba Inayopendekezwa itapigiwa kura na wananchi na kuzaa Katiba Mpya.

Serikali ilitumia zaidi ya Sh100 bilioni katika mchakato wa Katiba, hizo ni fedha za walipa kodi wa taifa hili hivyo si vyema kuweka pembeni jitihada zile. Tunaamini kuwa sasa ni muda mwafaka wa kurejea tena kwenye mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.

Wadau wanaona kuwa ni vyema mchakato huo ukaendelea sasa wakati ambapo kuna utulivu wa kutosha badala ya kusubiri kipindi ambapo taifa litakuwa linaelekea kwenye uchaguzi. Mwaka 2019 kutakuwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2020 kutakuwa na uchaguzi mkuu, hivyo muda mwafaka wa kurejesha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ni kati ya mwaka 2017 hadi 2018.

Tunaunga mkono jitihada za Rais za kusafisha nchi, ila suala la kuhakikisha nchi inapata Katiba Mpya nalo ni muhimu na tunamshauri Rais aliingize katika vipaumbele vyake, kwani ni wazi kuwa kuwapo kwa Katiba Inayopendekezwa imeweka mazingira mazuri kwa Rais kufanya kazi yake aliyoidhamiria ya kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati.


Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom