Katiba mpya iwe hivi

Katiba mpya iwe hivi

Rule of LAW

New Member
Joined
Jan 2, 2013
Posts
4
Reaction score
1
MAONI YA KATIBA MPYA
Tanzania ifuate muundo wa Katiba iliyoandikwa ya Ki-sekula na inayofuata mfumo wademokrasia. (A secular written and democratic constitution).
Katika muundo wa Ki-sekula, serikali na dini ni vitu visivyo changamana. Yaani serikali haipaswi kushabikia dini moja au nyingine bali maswala yote ya dini na imani ya wananchi wake ni maswala binafsi na yasiyoingizwa katika taratibu za utendaji wa serikali wala Katiba ya Nchi. Muundo huu ni muundo unaozingatia kuwa, ukiondoa ile dhana ya utamaduni wa jumla katika jamii, jamii imeundwa na tamaduni tofauti-tofauti na kila mtu ana uhuru wa kuamua aamini nini na atekeleze vipi imani yake bila kuvunja sheria halali za nchi. Kwa hali hiyo hujenga utamaduni wa kuvumiliana na kuchukuliana (religious tolerance) katika jamii bila kulazimishana kufuata dini au imani fulani. Muundo huu ndio unaoleta misingi ya amani na utulivu katika Taifa. Hivyo unafaa kufuatwa na katiba mpya ya Tanzania.
1. UHUSIANO WA SERIKALI, DINI NA MASHIRIKA YAKIDINI.
(a) Hoja iliyopo ni kuwa Katiba ya Sasa haitambui uwepo wa Mungu na Mamlaka yake.
(i) Katiba Mpya: Isiingize kwa namna yoyote ile masuala ya Imani ya Mtu au Watu. Masuala ya kuwepo au kutokuwepo kwa Mungu ni Masuala ya Imani kulingana na dini anayoamini mtu mwenyewe na sio Masuala ya KIkatiba.
(ii) Katiba Mpya: Itamke waziwazi kuwa Tanzania ni Nchi inayofuata mfumo wa Kisekula na wa kidemokrasia na kwa sababu hiyo, serikali haitafungamana wala kujihusisha na mambo ya kidini au kutumia sheria yoyote ya kidini katika kuendesha majukumu yake yote.

KWAMBA KATIBA ILIYOPO INASEMA SERIKALI HAINA DINI NA HIVYO KUTOTAMBUA SHERIA ZA KIDINI.
(iii) Katiba Mpya iendeleze Msimamo huu uliopo wa Serikali kutokuwa na Dini na uwe ni moja ya nguzo dhahiri na madhubuti zisizotenguka au kutenguliwa na chombo au mtu yeyote.
(iv) Katiba Mpya iweke wazi kuwa inaheshimu uwepo wa dini na taratibu zake lakini taratibu hizo hazitaingiliana kwa namna yoyote na sheria na taratibu za Serikali na uendeshaji wa taasisi za serikali.
(v)Katiba mpya iweke dhahiri kuwa sheria na taratibu za uendeshwaji wa taasisi za kidini ni jukumu la dini husika na kwa namna yoyote sio jukumu la serikali. Katiba itake sheria za nchi zifuatwe hata pale zinapokwenda kinyume na imani ya raia kulingana na dini yake.
(vi) Katiba mpya iweke bayana kuwa sheria zote za nchi zitatungwa kwa kuzingatia misingi ya Katiba na haki za binadamu na uhuru wa mtu au raia yeyote anayezingatia sheria na taratibu zilizokubaliwa nakupitishwa na bunge halali la watanzania utalindwa kikamilifu.
(vii)
Katiba mpya iweke bayana kuwa mambo yanayohusu 'Ibada' au 'dini' yako nje ya misingi ya Katiba isipokuwa tu pale mambo hayo yanapogusia suala la kulinda uhuru wa kuabudu wa mtu binafsi au kikundi cha watu litalindwa kikatiba.
(viii) Katiba Mpya Kamwe isithubutu kuchanganya mamlaka ya kidini na ile ya kiserikali bali isisitize kuwa mamlaka ya nchi yametenganishwa mbali na mamlaka ya dini na mifumo yote ya kidini

(B) KUHUSU MATUMIZI YA MANENO AU MISAMIATI INAYOFUNGAMANA NA DINI KATIKA KATIBA
(i) Katiba Mpya iepuke kuingiza maneno au misamiati ya kidini ndani ya Katiba na kama ilivyo katiba ya sasa ihakikishe kuwa maneno yanayotumika hayafungamani na misamiati ya kidini au imani fulana ya watu au kundi la watu katika nchi bali ni huru.

(c) KUHUSU SIKU ZA IBADA ZA KIDINI.
Katiba Mpya iepuke kuingiza siku za mambo ya Ibada katika Katiba. Mambo ya Ibada na siku za Ibada za mapumziko si swala la Kikatiba bali ni mambo yanayoweza kuangaliwa kupitia sheria ya bunge inayohusu siku rasmi za mapumziko katika nchi.

(d) KUHUSU MAHAKAMA ZA KIDINI KATIBA MPYA:
(i) isiingize kwa namna yoyote taasisi au mahakama za kidini au kikabila katika Katiba. Suala la Mahakama za kidini ni swala la kidini kwani ni taasisi iliyo kwa mujibu wa taratibu za ki-dini na hivyo haipaswi kuwepo katika katiba ambayo si ya kidini.
(ii) Isisitizwe bayana kuwa kwa vile serikali inafuata mfumo wa kisekula serikali haitahusika Na kuanzishwa au kugharamia taasisi za kidini, kama vile mahakama za kidini bali itahusika tu na mahakama za kiraia zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi zilizotungwa na Bunge. Hii itasaidia kujenga ukuta wa matengano kati ya serikali na mahakama za kidini.

UTAMBUZI WA SHARIA NA UFUATWAJI WA SHERIA ZA KIDINI Katiba Mpya:

(i) Iweke bayana kuwa Serikali haitojihusisha kwa namna yoyote ile na matumizi ya sheria za kidini na ipige marufuku taasisi za kiserikali kutumia matumizi ya sheria za kidini katika nchi au eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (ii)Katiba mpya: Iweke wazi kwamba shughuli zote za mahakama zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania zitafuata na kuzingatia taratibu na miongozo iliyokwekwa kwa mujibu wa sheria za Bunge na Katiba na sio sheria za kidini.

UHUSIANO WA SERIKALI NA MASHIRIKA YA DINI.
Katiba Mpya:
Iweke dhahiri kuwa Serikali itajihusisha au kushirikiana na taasisi za kidini katika mazingira ya uwazi na bila upendeleo wowote hususani pale tu taasisi husika zinapojihusisha na shughuli za maendeleo ya ki-jamii: mfano Afya, elimu, maji, n.k.

UHUSIANO WA DINI NA VYAMA VYA SIASA.
Katiba Mpya; (i) Ipige marufuku kwa dini zote kujihusisha na vyama vya kisiasa au shughuli za kisiasa. Hii ni muhimu ili kuhakikisha dini au taasisi za dini hazifungamani na makundi ya kisiasa katika nchi.
(ii)Ipige marufuku uanzishwaji wa vyama vya kisiasa vyenye mrengo wa kidini au kikabila katika Jamhuri ya (Muungano) wa Tanzania (yaani Zanibar na Tanzania Bara) Hili ni muhimu ili kuhakikisha kuwa vyama vinavyoshinda chaguzi na kuunda serikali havikiuki dhana na msingi wa kutenganisha dini na serikali.

UHURU WA KUABUDU NA KUJIUNGA NA DINI.
Iendelee kuhakikisha kuwa ibara ya 19(1), (2) na (3) ya Katiba ya sasa inabakia katika Katiba Mpya na pia iweke wazi kuwa uhuru wa kutangaza au kuhubiri dini hautaingiliwa na vyombo vya usalama, vyombo hivyo havitahusika kutoa vibali vyovyote ila tu vitatoa ulinzi pale stahili kwa makusanyiko kuhakikisha usalama wa raia wanapokusanyika.

KUHUSU UTEUZI WA VIONGOZI KATIKA NYADHIFA MALIMBALI SERIKALINI NA KATIKA TAASISI ZA KISERIKALI, BUNGE AU MAHAKAMA. Katiba Mpya:
Iweke dhahiri kuwa uteuzi wa viongozi katika serikali, taasisisi za serikali au idara hautazingatia misingi ya dini, jinsia, wala ukabila wa mteuliwa bali utazingatia usawa, sifa za kiuweledi, uwezo (ikiwemo elimu) na uwajibikaji wa mhusika. Hii ni kuondoa dhana ya kuteua watu kwa misingi ya kugawana nafasi kiudini udini hali ambayo haileti ufanisi katika maendeleo ya nchi bali huleta na kuendekeza umaskini na kutokuwajibika ipasavyo kutokana na kuwa na viongozi wasio na uwezo kielimu au wasio na sifa za kiuweledi.

UMILIKI WA RASILIMALI NA MUSTAKABALI WA WANANCHI KATIKA UMILIKI HUO.
Hili ni muhimu. Rasilimali zitumike kwa namna ambayo asilimia Fulani ina nufaisha eneo rasilimali husika ilipo. (Benefit sharing concept). Mwekezaji aliye mahali lazima aingie mkataba na serikali ya kijiji ya kukubali kuacha 1% hadi 2% ya faida ya kila mwaka katika account ya maendeleo ya kijiji au eneo husika. Kwa lugha nyingine wananchi wa eneo wawe na hisa yao ambayo ni ardhi zitokako rasilimali husika kama ni madini au rasilimali nyingine.

UMILIKI WA ARDHI NA ULINZI WA MAZINGIRA.
Suala laumulikishwaji ardi kwa mtu binafsi kama mali yake na kuondoa dhana ya serikal (RAIS) kuwa mmiliki kwa niaba ya wananchi lisiondolewe kwani mfumo tulionao umetusaidia kilamtazani kuweza kuwa na ardhi. Kuuondoa mfumo wetu na kuiga mifumo kama ya Kenya "absolute ownership" kutawafanya watanzania kuwa maskini kuliko kwani ardhi yetu itanunuliwa na kumilikiwa na wachache wenye fedha kiasi kwamba mtu mmoja aweza kununua mkoa mzima nakuwa mali yake binafsi!

BUNGE NA UCHAGUZI WA WABUNGE, MADIWANI NA RAIS NA CHAGUZI NDOGO.
Suala la CHAGUZI NDOGO liangaliwe upya kwani linamatumizi makubwa ya fedha za maendeleo. Kama Mbunge akifarika au vinginevyo basi chama alikotoka kimteue mtu atakaye shika nafasi iliyoachwa wazi kwani ndicho kilichopata ridhaa ya kuliongozi eneo bunge (jimbo) husika kwa miaka mitano!

BARAZA LA MAWAZIRI NA UTEUZI WA MAWAZIRI. Baraza la Mawaziri lisiundwe kutokana na Wabunge ili kuimarisha utengano wa Bunge na Serikali (Separation of Powers to prevent dictatorship or absolutism). Mawaziri wateuliwe toka kwa wataalamu wasio wabunge. Mbunge awe mbunge basi. Pia wabunge wasifanywe wajumbe wa Bodi, au kupewa kazi tofauti na ubuge. Kazi yao iwe moja ya uwakilishi. Hii itawapa nafasi nzuri ya kuihoji serikali na kuibana inapovurunda mambo ikiwemo nafasi ya kupiga kura ya kutokuwa na Imani na Baraza/Serikali.

KINGA DHIDI YA MASHITAKA YA JINAI NA MADAI KWA RAIS.
Katiba mpya ifute kinga dhidi ya mashitaka ya jinai na madai kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anayopewa na ibara ya 46 (1) na (2). Kwa hiyo katiba mpya iweke wazi kuwa Rais ashitakiwe kwa makosa ya jinai, makosa dhidi ya binadamu na madai.
 
Back
Top Bottom