Kutoka Ilani ya NCCR-Mageuzi 2010, uk. 8-11
4.0 AJENDA ZETU KATIKA UCHAGUZI WA 2010
4.1 AJENDA ZA KIUTAWALA
4.1.1 KATIBA MPYA
Katiba ya nchi ndiyo sheria kuu ya nchi. Sera za Serikali na Sheria za nchi lazima zitokane na kufungamana na katiba ya nchi. Kama taifa lina katiba mbaya isiyolinda haki za wananchi, basi sheria na mfumo wa utoaji wa haki utakuwa mbaya na usiotenda haki. Kama katiba ya nchi na sheria zake havilindi haki, basi watendaji wa vyombo vya dola hawatatenda haki kwa kuwa haki haipo kisheria.
Pia, Taifa ambalo katiba yake ni mali ya viongozi, kwa maana kwamba imetungwa na viongozi kwa ajili ya kujiweka madarakani na kulinda masilahi yao, halina demokrasia ya kweli. Katiba ya Tanzania ni ya aina hiyo, Ni katiba iliyotungwa na viongozi kupitia Bunge Jamhuri. Sote tutatambua kuwa kwa mujibu wa taaluma ya katiba, Bunge ni chombo cha kutunga sheria za kawaida za nchi lakini si chombo cha kutunga katiba. Katiba ya nchi hutungwa na Baraza la Taifa la Kutunga katiba.
Chama cha NCCR – Mageuzi kinatambua ukweli kwamba baraza la Taifa la Kutunga Katiba ndicho chombo halali cha kutunga katiba ya nchi. Chama chetu kinatambua pia kuwa tangu Taifa letu kuundwa, hatujawa na chombo hiki kwa mujibu wa katiba na sheria zetu za nchi.
Baraza la Taifa la Kutunga Katiba hujumuisha wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, na wawakilishi wa sekta muhimu, vyama vya siasa, taasisi za kijamii, mashirika ya dini, vyama vya wafanyakazi, wakulima, taasisi mbalimbali za serikali na kadhalika.
Chama cha NCCR-mageuzi kitahakikisha kuwa Baraza la Taifa la Kutunga Katiba litaundwa na litatekeleza mchakato wa kutungwa katiba mpya. Kwa mujibu wa mageuzi haya, lengo letu ni kuwa na katiba mpya ya nchi itakayofanya mambo yafuatavyo:
i) Itaainisha misingi na maadili ya utaifa kutokana na muafaka wa kitaifa, misingi ambayo itadumisha haki, maelewano, amani na umoja.
ii) Itaweka mfumo mpya wa uchaguzi utakaowawezesha wananchi kuwachagua viongozi wao katika uchaguzi huru na wa haki. Mfumo huo utaanzisha uwakilishi wa uwiano sambamba na uwakilishi wa majimbo ulioko hivi sasa.
iii)Itaamuru kuwepo na tume huru ya uchaguzi na itaweka masharti ya uundwaji wake;
iv) Italiamuru Bunge la Jamhuri kutunga sheria mpya ya uchaguzi inayoweka mazingira huru na sawa kwa wote kushiriki na kushindana katika uwanja ulio sawa.
v) Itaweka misingi ya mgawano wa mamlaka katika mihimili ya dola itakayoondoa utaratibu wa hivi sasa wa mihimili hii kuingiliana katika utendaji wa wajukumu yake na itaondoa utaratibu usiofaa wa kuwapa watumishi wa mihimili hii kofia zaidi ya moja, matharani mbunge kuwa pia waziri au mkuu wa mkoa, jaji kuwa mwenyekiti wa Tume ya serikali, na kadhalika.
vi) Itaweka usawa wa kijinsia katika kutekeleza mfumo mpya wa uchaguzi.
vii) Itatangaza rasmi utaifa wa Watanzania, kuweka vigezo vya uraia na kutaja wazi haki ya kila raia kupewa kitambulisho cha uraia.
viii) Itaanzisha mahakama ya kudumu ya katiba itakayopokea na kusikiliza masharti ya kikatiba, raia binafsi au taasisi.
ix) Italipa bunge nguvu ya kuwa chombo cha kutetea maslahi ya wananchi na kuwa na uamuzi wa mwisho katika utungaji wa sheria, uridhiaji ya mikataba na kuwa na mamlaka ya kupitisha au kukataa uteuzi wa viongozi muhimu wa dola.
x) Itaainisha wizara na idadi ya kudumu ya wizara za Jamhuri ya Muungano.
xi) Itapunguza baadhi ya madaraka ya rais kwa kuyaweka kwenye vyombo vingine vya maamuzi.
xii) Italinda haki ya raia wa Jamhuri ya Muungano kumiliki ardhi na kulipwa fidia ya haki inayoendana na bei za soko ardhi inapochukuliwa na serikali kwa miradi ya umma.
xiii) Itaweka muundo wa muungano wenye dola la shirikisho baina ya Tanganyika na Zanzibar.
xiv) Itaainisha haki za binadamu kwa viwango vinavyokubalika kimataifa ikizingatia utu wa mwafrika na utamaduni wake.
xv) Itaruhusu wagombea huru wa nafasi za uongozi (udiwani, ubunge, na urais).
xvi) Itatambua sekta ya habari kama muhimili muhimu wa demokrasia yetu na kuliamuru Bunge litunge sheria ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari na haki ya raia kupata, kutumia na kutuma habari;
xvii) Itaimarisha uhuru wa mahakama na kuamuru Bunge litunge sheria itakayorahisisha utoaji na upatikanaji wa haki kwenye vyombo vya maamuzi nchini;
xviii) Itahakikisha kuwa ardhi na maliasili vinaendelezwa, vinamilikiwa na vinawanufaisha Watanzania.