SI KWELI Katika muhula wa kwanza wa Hayati Rais Magufuli Tanzania haikuwahi kupokea msaada wa kifedha kutoka kwa nchi yoyote

SI KWELI Katika muhula wa kwanza wa Hayati Rais Magufuli Tanzania haikuwahi kupokea msaada wa kifedha kutoka kwa nchi yoyote

Baada ya kuitathmini taarifa hii, tumebaini kuwa si ya kweli.
1691435263640.png

Ni kipindi nakumbuka Mwamba aliibatiza jina nchi kuwa donor country (nchi inayotoa misaada) na kuna usemi kwamba Tanzania tulijihudumia bila misaada ya wazungu tulijibana bana tule kwa urefu wa kamba ndio maana hata vyuma ilibidi vikazwe.

Palikuwa pana ukweli?
 
Tunachokijua
Tangu kuingia kwake madarakani mnamo mwaka 2015, Rais Magufuli alijitambulisha kama kiongozi aliyehimiza umuhimu na ulazima wa nchi ya Tanzania na bara zima la Afrika kujitegemea. Mara nyingi alijitolea kufikisha ujumbe wa kutokubaliana na misaada ya kigeni na kutoa wito kwa kila Mtanzania kuchapa kazi kwa juhudi ili nchi iondokane na utegemezi wa misaada ya wafadhili ambayo huambatana na masharti.

Hii iliweka wazi msimamo wake wa nia ya kujenga uwezo wa kifedha wa ndani na kutotegemea misaada kutoka nje. Lakini pia, alieleza wazi mtazamo wa kuwezesha bara la Afrika kuwekeza katika rasilimali zake za ndani na kusimamia uchumi wake, huku akiamini kuwa bara hilo lina uwezo wa kugharamia miradi yake bila kutegemea wageni.

Baadhi ya viongozi barani Afrika wakati fulani pia walieleza kuunga mkono msimamo wa Magufuli kwa umuhimu wa bara la Afrika kujitegemea kiuchumi na kuwa na uwezo wa kugharamia miradi yake kutokana na mapato ya ndani. Kwa mfano, ukifuatilia hotuba za marais karibu wote waliohudhuria mazishi ya kitaifa ya Rais Magufuli Jijini Dodoma Machi, 2021, walimsifu kwamba walau alionesha kwa vitendo kwamba Afrika inaweza kuondokana na utegemezi wa mataifa ya nje.

Rais Kenyatta, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati ule, alisema Dkt. Magufuli alikuwa amedhihirisha kwamba bara la Afrika linaweza kuinua kichwa chake kwa heshima na kugharamia sehemu kubwa ya miradi yake kutokana na mapato yaliyokusanywa ndani bila kutegemea wageni, ambao misaada yao mara nyingi huja na masharti mengi.

Hata hivyo, licha ya Rais Magufuli kusisitiza msimamo wa kujitegemea, Tanzania iliendelea kupokea misaada ya kifedha kutoka kwa mashirika na nchi mbalimbali duniani ili kutekeleza miradi yake ya maendeleo, ikielezwa kuongeza uwezo wa nchi katika kuboresha maisha ya wananchi wake na kukuza sekta tofauti za kiuchumi na kijamii.

Kwa mfano, mnamo Februari mwaka 2020, Umoja wa Ulaya (EU) ulikubali kuruhusu kutoa Sh132 bilioni kwa ajili ya kuchangia bajeti ya maendeleo ulizokuwa umezizuia mwezi Desemba 2018. EU ilisimamisha kutoa msaada wa Euro 80 milioni (Sh 203 bilioni) baada ya kutokea mgogoro wa kidiplomasia. Uamuzi huo ulitangazwa baada ya Rais John Magufuli kufanya mazungumzo na balozi wa umoja huo nchini Tanzania, Manfred Fanti, Ikulu jijini Dar es Salaam. Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu wakati huo, Bw. Gerson Msigwa ilieleza kuwa mazungumzo ya Rais Magufuli na Fanti yaliruhusu kuendelea kwa mpango wa Umoja wa Ulaya kuchangia bajeti ya maendeleo ya Tanzania, na kwamba walikuwa wakiandaa mpango mwingine wa miaka saba uliotarajiwa kuanza baadaye mwaka huo.

Pamoja na hayo, baadhi ya kauli pia zilionesha kwamba Tanzania haikuwa ikikataa kupokea mikopo kabisa, bali ilikuwa ikikataa mikopo yenye masharti magumu. Mnamo mwezi Novemba mwaka 2018, wakati wa uzinduzi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyojengwa kwa msaada wa China, Magufuli aliwasifu Wachina kuwa wanatoa misaada isiyokuwa na masharti. Alieleza kuwa China ni marafiki wazuri kwani walitoa fedha za walipa kodi wao zaidi ya shilingi bilioni 90 bila masharti. "Jambo la kufurahisha ni kwamba misaada yao haiambatani na masharti. Wenyewe wakiamua kukupa wanakupa, walitujengea TAZARA, URAFIKI na pia wametusaidia katika maeneo mengine ya maendeleo," alisema Rais Magufuli na kumhakikishia Balozi Wang Ke kuwa serikali ya Tanzania itahakikisha kila msaada unaotolewa unatumiwa vizuri.

Lakini pia, Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), uliipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 30 (Shilingi bilioni 84) kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kujenga miundombinu ya kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia. Mkataba wa sehemu ya fedha hizo, kiasi cha Euro milioni 26 (shilingi bilioni 72) ulisainiwa tarehe 15 Desemba, 2020 kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Frederic Clavier na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) Bi. Stephanie Mouen Essombe.

Mnamo mwezi Februari 2020, Serikali ya Tanzania pia ilitiliana saini mikataba miwili ya msaada na serikali ya Sweden kwa kupatiwa fedha kiasi cha dola milioni 90 sawa na shilingi Bilioni 240.95 kutoka mfuko wa ushirikiano wa Elimu Duniani GPE. Mkataba huo unatokana na mfuko ambao unachangiwa na washirika wa maendeleo wengine wakiwemo UNICEF, UNESCO, Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya, Australia, Canada, Denmark, Ufaransa, Korea, Uholanzi, Norway, Hispania, Uswisi, Marekani pamoja na Uingereza.

Hivyo basi, mifano hiyo michache inakinzana na madai ya Tanzania kutopokea misaada kabisa kutokana na ukweli wa matukio na mikataba ya kifedha iliyofanyika wakati wa uongozi wa Rais Magufuli.
Back
Top Bottom