Kauli ya Kutaka Kulipia Barabara ya Mabasi ya Mwendokasi Inapaswa Kupingwa Mara Moja

Kauli ya Kutaka Kulipia Barabara ya Mabasi ya Mwendokasi Inapaswa Kupingwa Mara Moja

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
Joined
May 5, 2014
Posts
631
Reaction score
1,577
ACT Wazalendo tunapinga vikali kauli iliyotolewa jana Februari 14, 2025 na Waziri wa Ujenzi, Ndg. Abdallah Ulega, akipendekeza kuwekwa utaratibu wa kulipia matumizi ya barabara ya mwendokasi kwa wale wanaotaka kuepuka foleni. Kauli hii haipaswi kupuuzwa ni ushahidi mwingine wa jinsi serikali inavyokosa huruma kwa wananchi wake na kukosa uwajibikaji kwa maslahi ya wananchi.

Mradi wa mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam ulijengwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania na hivyo ni haki ya kila mwananchi kuutumia bila vikwazo vya gharama. Kuweka ada kwa huduma ambayo ilikusudiwa kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri wa umma ni kinyume na malengo. Huu ni ubaguzi wa wazi ambapo sasa wananchi maskini watalazimika kubaki kwenye foleni kwa sababu hawawezi kumudu gharama mpya.
WhatsApp Image 2025-02-15 at 16.50.08_219e367b.jpg

Aidha, mfano uliotolewa na Waziri Ulega kuhusu Daraja la Mwalimu Nyerere Kigamboni kama jambo la mafaniko ni dhihaka kwa wananchi. Inashangaza, licha ya malalamiko ya muda mrefu kuhusu ada kubwa za daraja hilo na serikali kutoonesha nia ya kushughulikia changamoto hiyo. Sasa Waziri anapendekeza mfumo huo wa uonevu uendelezwe kwenye barabara za mwendokasi. Huu ni uthibitisho kwamba serikali ya CCM haina ajenda ya maendeleo yanayowalenga wananchi bali inaendeleza siasa za kutengeneza vikwazo vya kiuchumi kwa wananchi.

ACT Wazalendo tunasisitiza kwamba:
i. Barabara ya mwendokasi ni mali ya umma na haitakiwi kuwa biashara ya kuwanufaisha wachache.

ii. Waziri Ulega angejikita kuchukua hatua madhubuti za kutatua changamoto za uendeshaji wa mabasi ya mwendokasi ili kuleta ufanisi na kumaliza tatizo la msongamano, uhaba wa magari na uchakavu.

iii. Serikali ina wajibu wa kuhakikisha huduma za usafiri wa umma zinabaki kuwa nafuu na kupatikana kwa wananchi wote bila ubaguzi wa kiuchumi.

iv. Kama serikali inaona kuna haja ya kuwa na barabara ya haraka ya kulipia (Express toll road) ijenge au iruhusu sekta binafsi ijenge kwa ajili hiyo badala ya kutumia miradi iliyojengwa kwa fedha za umma au mikopo itakayolipwa na fedha za umma ili kuwanufaisha watu wachache tu (vibopa).

Tunaitaka serikali kuacha mara moja mawazo haya dhalimu na badala yake kuelekeza juhudi katika kuboresha miundombinu kwa ajili ya wote.
Aidha, tunatoa wito kwa Serikali kutafakari ujenzi wa barabara za mzunguko (ring roads) kuzunguka Mji wa Dar es Salaam ili kuyaondoa Malori kutumia barabara za katikati ya mji yanapobeba mizigo kutoka bandari ya Dar e s Salaam.


Imetolewa na;
Eng. Mohammed Mtambo
Waziri Kivuli wa Miundombinu
ACT Wazalendo.
Februari 15, 2025.
 
Back
Top Bottom