Askari 11 wa Usalama Barabarani wa mikoa ya Iringa, Morogoro na Pwani wameondolewa kwenye vitengo vyao vya kazi baada ya kuonyeshwa kwenye televisheni wakipokea rushwa, imeelezwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkuu wa Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema, alisema kufuatia tukio hilo, amewaagiza makamanda wa Polisi wa mikoa kuwachukulia pia hatua za nidhamu zinazostahili.
Alisema askari hao 11 walioonekana kwenye mkanda wa uchunguzi uliofanywa na kituo cha televisheni cha ITV, watahojiwa na kuchunguzwa na ikithibitika kuhusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na kanuni za Polisi.
"Kipindi kile nilikiona na kimenifurahisha sana, nachukua fursa hii kuvipongeza vyombo vya habari kwa kutuunga mkono katika vita dhidi ya rushwa hasa kipindi maalumu kilichorushwa na ITV kwa kweli kimetufundisha," alisema Mwema.
Alisema lengo la Polisi ni kujidhihirisha katika jamii ya Watanzania kwa kuwa na utumishi ulio bora, hivyo imejipanga kutafuta miundombinu ya kisasa katika kuongeza ufanisi katika utendaji wake badala ya kutumia askari zaidi ya 1,000 barabarani.
"Tutashirikiana na Wizara za Miundombinu na Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha kuwa tunakuwa na mfumo na miundombinu ya kisasa, ili makosa ya barabarani, ajali na uvunjifu wowote wa sheria uonekane kwa urahisi kupitia kamera za CCTV," alisema.
Pamoja na hayo, Mwema alisema katika tathmini ya hali ya uhalifu ya kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu, imeonyesha upungufu wa matukio ya uhalifu kutokana na sababu mbalimbali lakini kubwa zaidi ni kuimarika kwa ushirikiano kati ya wananchi na Polisi, (Polisi Jamii).
Hata hivyo alisema chombo hicho bado kinakabiliwa na wakati mgumu hasa katika miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba ambako matukio ya uhalifu hujitokeza kwa kiwango cha juu kama vile mauaji na unyang'anyi wa kutumia silaha hali ambayo hata hivyo Polisi imejipanga kukabiliana nayo