Ninachukulia Kenya kama nyumbani kwangu, kwa sababu niliishi na kufanya kazi huko mara mbili kwa miaka mitano na nusu. Kwa zaidi ya miaka kumi kati ya mara hizo mbili, nimejionea mabadiliko makubwa yaliyotokea nchini humo, haswa uboreshaji wa miundombinu.
Mwaka 2004, wakati nilipofanya kazi nchini Kenya kwa mara ya kwanza, nilitembelea Mbuga inayojulikana zaidi duniani ya Wanyamapori ya Masai Mara. Barabara kutoka Narok hadi Masai Mara iliniachia kumbukumbu kubwa sana. Barabara hiyo yenye urefu wa takriban kilomita 100 ilikuwa mbovu sana, na ilituchukua karibu saa 6 njiani. Watu wengi walisema, Masai Mara ni kama Peponi, lakini barabara ya kuelekea huko ni kama Motoni. Mwaka 2017, wakati nilipokaribia kumaliza muhula wangu wa pili wa kufanya kazi nchini Kenya, ujenzi wa barabara kuu ya C12 kati ya Narok na Masai Mara ulikamilika, na muda wa kusafiri kati ya sehemu hizo mbili ulipungua hadi saa mbili.
Miundombinu ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi, imeboreshwa zaidi. Wakati nilipofika mji huo kwa mara ya kwanza, kulikuwa na barabara kuu moja tu, ambayo ni Mombasa Highway. Ingawa iliitwa Highway, lakini kasi ya magari haikuweza kuzidi kilomita 60 kwa saa kutokana na ubovu wake. Wakati wa asubuhi na jioni, msongamano wa magari ulikuwa mkubwa kiasi cha kuwafanya watu kuchanganyikiwa. Lakini sasa mji wa Nairobi una mtandao mzuri wa barabara.
Niliposimama kituoni kwa mara ya pili, Nairobi tayari ilikuwa na idadi kubwa ya barabara kuu kama vile Thika Road, Ring Road, na Nairobi Expressway. Uboreshaji wa barabara ni upande mmoja tu, mabadiliko ya Nairobi yametokea katika nyanja zote. Ujenzi wa Kituo cha Biashara cha Kimataifa (GTC) ulikamilika mwaka jana, na hilo ni jengo refu zaidi katika Afrika Mashariki. GTC si kama tu imeongeza nuru kwa mji wa Nairobi, bali pia imeleta manufaa halisi kwa wakazi wa jiji hilo, kwani imeweza kutoa zaidi ya ajira 4,000 kwa Wakenya.
Jambo lililonifurahisha zaidi ni kwamba, miradi mingi ya ujenzi wa miundombinu hiyo, ikiwa ni pamoja na barabara ya C12, ilijengwa na kampuni za China. Katika miaka ya hivi karibuni, ushirikiano kati ya China na Kenya katika ujenzi wa miundombinu umestawi, na kupata matokeo makubwa.
Tukitaja ushirikiano wa ujenzi wa miundombinu kati ya China na Kenya, hatuwezi kusahau Reli ya SGR. Reli hiyo iliyozinduliwa mwaka 2017 imepunguza muda wa safari kati ya Nairobi na Mombasa kutoka zaidi ya saa kumi hadi zaidi ya saa nne tu, na nauli pia imeshuka kwa zaidi ya nusu. Sasa watu wa Nairobi wanaweza kwenda Mombasa kwa mapumziko ya mwisho wa wiki kwa treni. Aidha, reli hiyo imetoa nafasi za ajira zaidi ya 50,000 kwa Wakenya.
Muhula wangu wa pili wa kazi nchini Kenya uliishia kwenye hafla ya uzinduzi wa Reli ya SGR. Siku hiyo, niliimba na kucheza ngoma pamoja na Wakenya, nikiwa na furaha kwamba nchi hii hatimaye imekuwa na reli ya kisasa, na pia nafurahia zaidi urafiki mkubwa na ushirikiano mzuri kati ya China na Kenya.