Wizara ya Afya nchini Kenya imethibitisha kurekodiwa kwa visa vipya vinne vya virusi vya Ebola, na kufanya jumla ya wagonjwa nchini humo kufikia saba, ikiwa ni pamoja na kisa cha kwanza cha aliyefariki.
Nchi hiyo haikuwa imewahi kuripoti kisa chochote cha Ebola hadi Oktoba 6, kufuatia kifo cha mfanyabiashara Mkenya mwenye umri wa miaka 40 aliyekuwa akiishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Marehemu alisafiri kwa njia ya nchi kavu hadi Kampala, Uganda, kabla ya kupanda ndege kuelekea Nairobi mnamo Oktoba 3 na kufariki dunia tarehe 5 Oktoba akiwa kwenye matibabu.
Miongoni mwa visa hivyo vipya ni ndugu wa kiume wa karibu wa marehemu aliyekuwa karantini tangu Oktoba 6, pamoja na wafanyakazi watatu wa afya (wanaume wawili wenye umri wa miaka 29 na 35, na mwanamke wa miaka 32) waliomhudumia mgonjwa huyo wa kwanza.
Wote walionyesha dalili za homa na kuwekwa karantini mara moja kabla ya vipimo kurejesha majibu chanya.
Visa vingine vilivyothibitishwa awali vinajumuisha mwanamke wa miaka 65 na mwanamume wa miaka 39, ambao wote ni ndugu wa mwathiriwa wa kwanza. Wizara imeeleza kuwa kati ya watu 130 waliochangamana na waathiriwa, watu 128 wamefuatiliwa na kuwekwa karantini, huku ikisisitiza kuwa hatari kwa umma bado ni ndogo kwani hakuna ushahidi wa maambukizi katika jamii.
Mlipuko huu unahusishwa na mlipuko wa 17 wa Ebola nchini DRC unaotokana na aina ya virusi vya Bundibugyo ambavyo havina chanjo wala matibabu maalum ambapo zaidi ya watu 9,066 wameambukizwa na 4,381 kufariki tangu Mei. Uganda pia ilirekodi visa 20 na vifo viwili kabla ya kutangazwa kuwa huru dhidi ya Ebola mnamo Agosti.
Source: France 24