SoC02 "Kesho Isiyofika" - Bruno D. Sakalani

SoC02 "Kesho Isiyofika" - Bruno D. Sakalani

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Jul 29, 2022
Posts
5
Reaction score
4
KESHO ISIYOFIKA
“Unasikia midundo iyoo Chris!!? Yule Shayo mgombea wa PMP amekuja bwana!” Madokola, alimshtua Chris kwa kelele maana kwake yeye alidhani Chris alikwishazama katika ndoto na usingizi mzito.

“Naamka aisee!” alijibu Chris kwa sauti ya chini “Kwani watu wamekwisha jaajaa uwanjani?” Madokola akanyanyuka kutoka kwenye jiwe alilokuwa amekalia, akatupa macho uwanjani huku akimwambia Chris,

“Ndiyo, wamefurika bwana!” Madokola akainama karibu na sikio la Chris akamkonyeza

“Na Shani namuona kwa mbaali”

Chris akanyanyuka huku akitabasamu kwani alikuwa hajamuona Shani kwa takribani wiki mbili sasa tangu baba yake Chris – Mzee James Kapembwa alipofariki dunia. Kwa binadamu wengine wiki mbili hizi zilikuwa ni siku kumi na nne tu, lakini kwa Chris kilikuwa ni kipindi cha majonzi ya kumpoteza baba yake sambamba na upweke wa kumkosa Shani kipenzi chake.

Shani alipomuona Chris uso wake ulijawa na furaha tele. Chris naye alivyomuona Shani alitabasamu....
......................................................................................
Ramani ya nchi ya Kachemwa



Kwa sasa hali za kimaisha za wakazi wengi wa Kanyanza hazikuwa kama miezi saba iliyopita kabla serikali ya Kachemwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kanyanza hawajaifunga bahari ya Johe Magharibi wakidai kuwa sababu ni uvuvi haramu, licha ya kutokuwa na vithibitisho vyovyote vilivyoainishwa. Wachache waliojaribu kuvua nyakati za usiku waliishia rumande. Wapo wengine ambao katika harakati zao walidai wamekutana na meli kubwa za uvuvi kutoka ughaibuni; hakuna mkazi wa Kanyanza hakuna aliyeujua ukweli kama katazo za kutovua ni kwa ajili ya “kutunza mazingira” au ilikuwa ni njama za kutoa wigo kwa mabepari wa kunyonya rasilimali za Kachemwa.

Alfajiri ya leo Mzee Kapembwa aliamka kwa kuchelewa akihisi kupungukiwa nguvu lakini kwa kuwa alitakiwa akamalizie kuvuna mahindi na kuyaacha leo kungepelekea mahindi yaharibike kwa mvua au wezi wangeweza kuyashambulia. Katika kipindi hiki ambacho bahari imefungwa na uvuvi hauruhusiwi mahindi yamekuwa tegemeo pekee kwa wakazi wa Kanyanza. Mzee Kapembwa alimuamsha kijana wake, Christian, wakanawa nyuso zao na kila mmoja akakwea kwenye baiskeli yake na wakaelekea shamba. Njiani walikutana na kina mama waliovalia mavazi ya njano wakikiwakilisha chama tawala cha Kachemwa Democrati Party (KDP) na wengine walipeperusha bendera za buluu za chama pinzani cha Kachemwa Movement Party (KMP). Kwenye kinyang’anyiro hiki cha urais, chama cha KDP kilikuwa kikiwakilishwa na Mheshimiwa Balili Emmanuel aliyekuwa rais wa Kachemwa anayemaliza muda wake na Mafole Shayo aliiwakilisha KMP

Iliwachukua masaa manne kwa Christian na baba yake kukusanya takribani magunia matatu kila mmoja,katika hekari nne zao ilibaki hekari moja tu kuvuna.

Mzee Kapembwa alishusha pumzi akaenda kunywa maji,Christian akaendelea kuvuna.Baada ya muda Christian aligeu akamuona babaye amejilaza chini, kuona vile akamuita kwa sauti ya chini “Baba!!?” alipoona haitiki alimkimbilia akamkuta hajiwezi huku ameshika tumbo akilalama kwa maumivu makali.Christian akampakia babaye kwenye baskeli huku akitetemeka mikono akamkimbiza kituo cha afya cha Mkatezi, alipokuwa njiani Christian aliwaza sana kwa kuwa baba yake ndiyo ilikuwa nguzo pekee aliyokuwa amebakiwa nayo, mamaye alitangulia mbele za haki wakati Christian akiwa na miaka kumi tu... miaka kumi na miwili iliyopita.

Christian alipokaribia karibu na makazi ya watu alikutana na rafiki yake, Madokola aliyemsaidia kusukuma baiskeli hadi kituo cha afya cha Mkatezi.Makorongo ya barabarani yalipelekea wakafika kituoni wakiwa hoi, macho ya Chris yalikwishagubikwa na machozi maana baba yake alikuwa anakoroma tu.

Kituoni walipokelewa na Daktari Mnyazi ambaye baada ya muda alimuita Christian,

“Uliyemleta ni baba yako?” Christian alitingisha kichwa, Daktari Mnyazi akaendelea “Imeonekana alikuwa na taifodi na malaria kali tumboni. Na alifariki wakati mpo njiani. Pole sana Christian.” Kusikia hivi mwili wa Christian uliingiwa na baridi, akashusha pumzi, akaenda nje kukaa kwenye benchi huku akijifuta machozi. Madokola akamsogelea Christian akamshika bega kumpa pole

“Pole sana mzee!!”, Christian akashusha pumzi kwa nguvu mno, akanyanyuka pamoja na Madokola kuelekea chumba cha daktari ili kwenda kufatilia taratibu nyingine kwani Mkatezi haikuwa na mochwari.

Mzee Kapembwa alikwa maarufu miongoni mwa wanaoswali Ijumaa na waumini wenzake wa Parokia ya Kanyanza hivyo kwa pamoja walishirikiana kuhakikisha mzee wao anahifadhiwa ipasavyo kwenye nyumba yake ya milele.
Kaburi la Mzee James Kapembwa
......................................................................................

Chris alimkumbatia Shani akampa mabusu kadhaa, wakageukia uelekeo wa mziki unaosindikiza kampeni,

“Kweli watu wamejaa mzee!!” Chris alimwambia Madokola.

Muda huohuo ndipo mgombea Mafole Shayo aliwasili kuanza kampeni, alizungumzia sana jinsi uongozi wa Rais Balili Emmanuel ulivyoizamisha Kachemwa kwenye dimbwi la umaskini ilhali viongozi wa juu wa kiserikali wakifurahia maisha kwenye majumba yao ya kifahari, aligusia jinsi katazo la kutovua kwenye bahari ya Johe lilivyokuwa linaendelea kuwaumiza fukara wa Kanyanza na kuwafaidisha mabepari. Aliongea vingi mno kiasi kwamba Chris aliwabeba Shani na Madokola wakaanza kuondoka taratibu,

“Kachemwa sio nchi masikini. Ni uongozi mbovu ndio unaopelekea hadi leo bado mkoa tajiri kama Kanyanza unashindwa kuwa na hospitali inayoweza kuokoa maisha ya wananchi....”

Chris alivosikia hivi mwili wake ukasisimka mno kama kapigwa na baridi kali, Mafole akaendelea,

“Kanyanza yenye barabara za kiwango cha lami, huduma nzuri za afya. Kanyanza ambayo watu watakuwa wanafanya shughuli ya kiuchumi iliyowalea, shughuli ya uvuvi. Hii ndiyo kesho ambayo kila mkazi wa Kanyanza anaitamani. Kesho ambayo mnaiota na kuiwaza. Kesho Isiyofika. Nawaahidi raia wenzangu wa Kanyanza na Kachemwa kwa ujumla, mimi ndiye ninayekuja na ile kesho isiyofika kwenu. Kesho yenye kutimiza ndoto zenu na matamanio yetu. Hii ndiyo kesho nitakayowaletea endapo mtanichagua” Mafole alimaliza akisindikizwa na shangwe, makofi na vigeregere kutoka kwa akina baba hadi akina mama wa Kanyanza.

“Ingekuwa anayoyasema ni rahisi kuyatimiza, ingekuwa raha sana!” Chris aliongea kwa uchungu akikumbuka matukio ya wiki mbili zilizopita. Madokola akawaambia Shani na Chris,

“Siasa za Kachemwa bwana! Apo unaweza ukakuta aidha uyo Mafole anapotezwa au akishapata madaraka hiyo kesho anayoizungumzia itakuwa ni kesho isiyofika kweli!”

“Haitashangaza 😒!” Shani aliongezea.

Chris na Madokola wakamsindikiza Shani kwao kisha wakarudi kwa kina Madokola wakaa kusikiliza redio,

“Habari zilizotufikia hivi punde ni kwamba mgombea wa urais kutoka chama cha Kachemwa Movement Party amefariki mara baada ya kuvamiwa na kikundi cha watu alipokuwa anaelekea Chanyanzu kukamilisha kampeni zake akitokea Kanyanza. Kamanda wa polisi mkoani humo Inspekta Madanda amesema polisi inaendelea na uchunguzi juu ya kifo cha mwansiasa uyo nguli..”

Kesho tunayoitaka.png


Kusikia hivi, Chris na Madokola walishtuka wakatazamana wasijue nini cha kusema , Mafole alikuwa mpinzani wa karibu wa rais Balili. Kesho aliyokuwa akiihubiri Mafole ndiyo kesho ambayo raia wengi wa Kachemwa walikuwa wanaikosa, kwao kesho aliyokuwa akiizungumzia Mafole ilikuwa ni Kesho Isiyofika!🤦‍♂️

Bruno D. Sakalani
 

Attachments

Upvote 3
Hongera sn kazi nzr, karibu pia kuvote kazi yang

 
Hongera sn kazi nzr, karibu pia kuvote kazi yang

Shukran sana, nitakaribia🤝🏾
 
Back
Top Bottom