SoC04 Kesho tuliyoiishi

SoC04 Kesho tuliyoiishi

Tanzania Tuitakayo competition threads

Faraja S

New Member
Joined
May 24, 2024
Posts
2
Reaction score
1
Watu wanasema "ukitaka kujua umepiga hatua basi simama na uangalie ulipotoka". Kwa sisi watanzania ambao tuna ujasiri wa kuhesabu miaka 62 tangu tupate uhuru wa kuijenga Tanzania tuliyoitaka wenyewe, Je tukisimama na kuangalia tulipotoka tunaona nini?

Naomba dakika kadhaa za siku yako niweze kukueleza vile ninavyoiona Tanzania kwenye macho yangu na kwanini ninaamini tumeshaiishi kesho yetu.

Nakala hii itazungumzia sekta ya elimu kwa sababu ninaamini hapo ndio palipobeba uchumi wa nchi yetu. Najua tunasema kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa letu lakini hata kuweza kuhamisha ujuzi kutoka kwa mkulima mmoja kwenda mwingine hiyo ni elimu.

Ninaamini uwezo wetu wa kujenga kizazi bora wakati huu ndio mwanzo wa kutengeneza taifa imara. Uwekezaji wetu wa sasa unaweza kuzaa matunda ambayo tunaweza tusiyafaidi sasa lakini yakaja kunufaisha vizazi elfu kutoka sasa.

Miaka kadhaa iliyopita zoezi la kujisajili kwa ajili ya vitambulisho vya taifa lizinduliwa na kwa wakati ule nilipata bahati ya kuona vyeti vya baba yangu. Nilistaajabu kuona vitu walivyojifunza kipindi kile Tanzania tumepata nafasi tu ya kuanza kujijenga, ninamaanisha miaka ya sabini.

Walisoma kuhusu siasa, walisoma ufundi na ujuzi mbalimbali ambao ungeweza kuwasaidia watakapoingia mtaani, binafsi ninaamini kama wazee wetu wangepata teknolojia na miundo mbinu tuliyonayo sasa basi sisi watoto wao tusingeikuta Tanzania hii.

Sasa tatizo liko wapi? Machoni mwangu ninaona tatizo kuanzia kwenye mzizi wa shina na kadiri siku zinavyozidi kwenda mti huu huzidi kuoza na kupoteza ubora wake.

Utakubaliana na mimi kundi kubwa la vijana wa sasa hata hawajui wakimaliza elimu yao ya sekondari watasoma nini elimu ya juu. Mimi nikiwa kama mmoja wa wahanga wa hili na katika kuchagua kutafuta maisha mtaani ndipo unapojua kuwa hauna ujuzi na huo ujuzi ambao ni sehemu ya elimu inabidi utoe pesa ili kuupata. Je elimu tunayoipata mashuleni inafanya kazi gani kama haitupi ujuzi wowote wa kutusaidia kupambana na maisha tunapoingia mtaani?

Naamini wote tuna ndugu au tunafahamu watu ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na elimu lakini wanatumia ule ujuzi mdogo walioupata shule na unawaingizia kipato hadi uzeeni. Kwangu mimi ni ndugu yangu aliyeishia elimu ya msingi ambaye ni seremala hadi sasa.

Najua utabishana kuwa muda hautoshi kusoma vitu vya darasani na kuwa na muda wa kujifunza ujuzi. Lakini tukitulia na kuchunguza vitu watoto wanasoma mashuleni na hii nikimaanisha kuanzia elimu ya msingi, utagundua kuna vitu vingi ambavyo havikuwa na umuhimu wa wao kuvisoma wakati huu ingali watavisoma tena wakienda sekondari.

Pamoja na hilo kuwa tatizo kubwa lakini hilo sio mzizi wa tatizo machoni mwangu.

Machoni mwangu mzizi wa hili tatizo ni walimu. Utakubaliana na mimi kuwa kadiri siku zinavyozidi kwenda walimu wanaozidi kuhitimu masomo hawana ubora kama walimu wa miaka ya nyuma.

Machoni mwangu, na ninaamini sipo peke yangu ninaeona mchakato wa mtu kuwa mwalimu unaanza pale mtu anapokuwa hana chaguzi nyingine. Ameshafeli na alama zake zinamruhusu tu kwenda kusoma ualimu ili angalau asiambulie patupu. Mtu huyu ambae alifundishwa na mwalimu ambae mwanzo wake ulikuwa hivi kama yeye na yeye pia anaingia kwenye huo mzunguko ili aweze kwenda kuendeleza mzunguko mwingine. Je hii ni sawa? Ingali walimu wanasimama kama mama kwenye familia, je ni sawa upatikanaji wao utokane na mtu kukata tamaa na sio kutokana na shauku ya mtu kujenga kizazi bora na chenye faida kwa taifa lake?

Kazi ya ualimu ni kazi ambayo haijaheshimiwa kuanzia mchakato wake wa kutafutwa walimu hadi kwenye kutunzwa na kulipwa kwao. Imefikia hatua mtu akijitambulisha kama mwalimu unajua kabisa huyu kuna mahali alikoroga kwenye maisha na kwa kipindi hiki hii dhana imeshaingia hadi kwa vijana wanaosoma hasa wa sekondari. Je tunadhani hawa vijana wanaweza kuwaheshimu walimu wao kiasi cha kutamani kujifunza kutoka kwao?

Naamini elimu nzuri ni ile inayotoka kwa mtu unayemtazamia. Na hicho kitu hakipo kwenye shule zetu hasa za sekondari, na hii ndio sababu matokeo yetu ya elimu za msingi ni bora sana kuliko sekondari kwa sababu watoto wakiwa wadogo wanawatazamia sana walimu wao.

Matokeo yake tuna wanafunzi wasioheshimu walimu wala hawatazamii kujifunza kutoka kwao kwa sababu wanajua walimu wao walishindwa mahali.

Na upande wa pili tuna walimu wanaofundisha ili tu waweze kupeleka mkono kinywani na si vinginevyo. Kutokana na hili tumekuwa tukiona kesi nyingi za walimu zikizidi kuibuka kila kukicha na upande wa pili tumekuwa tukiona matokeo yakizidi kuzorota kila kukicha.

Ukiniuliza mimi ninaona nini na tufanye nini ili kujikwamua hapa nitakuambia hivi..

Kwanza ninaona Tanzania ambayo imeshindwa kutengeneza walimu wakutazamiwa.

Na pili mitaala yetu wenyewe ni chanzo kikubwa cha watoto wetu kukata tamaa na shule. Na kwa namna fulani nimekuwa nikijihoji hii mitaala yetu imetoka wapi?

Cha kufanya kinaweza kisichukue miaka mitano au kumi lakini ninaamini kinaweza kuwa mwanzo wa kuirejesha Tanzania tuliyoipoteza. Tanzania ambayo mtoto wake anapata elimu na ujuzi kutoka shule.

Ninaitazamia Tanzania ambayo walimu wataheshimiwa sana, kuanzia mchakato wa kutafutwa, kupatikana hadi malipo. Badala ya wale walioshindwa na kukata tamaa kuishia kuwa walimu, natamani wale walioonekana wana uwezo mkubwa ndio waingie kwenye huu mchakato. Tutengeneze walimu ambao watoto wetu watatazamia kuwa kama wao na hapa ndipo hamasa ya kweli inapopatikana.

Ninatazamia kuona ujuzi ukifundishwa mashuleni, ujuzi kama ufundi, ushonaji, sanaa, ususi, upishi ikiwemo uhokaji, elimu kuhusu kilimo, biashara, ujuzi wa tehama n.k... Hivi ni vitu ambavyo mtu atavitafuta mwenyewe akimaliza shule na kuingia mtaani. Lakini naamini ni haki ya msingi kwa shule kutupa nafasi ya kujifunza hivi vitu mashuleni.

Tupewe nafasi ya mwanafunzi kuchagua ule ujuzi anaotamani ajifunze kama vile tunavyopewa nafasi za kuchagua kombi za kusoma. Shule iwe mahali pa kujua au kupata mwangaza wa kile tunachotamani kufanya mbeleni maishani.

Natambua tuna safari ndefu sana ya kuiboresha sekta ya Elimu lakini kama tusipotibu mzizi huu basi tutakuwa tukijenga nyumba juu ya mchanga.

Naitazamia Tanzania ambayo tutakapozungumzia sekta ya elimu basi tuwe tumegusa ujuzi ukiwa kama sehemu kuu ya elimu hii..

Wako katika ujenzi wa taifa letu kuu la Tanzania.
 
Upvote 1
Ninaitazamia Tanzania ambayo walimu wataheshimiwa sana, kuanzia mchakato wa kutafutwa, kupatikana hadi malipo. Badala ya wale walioshindwa na kukata tamaa kuishia kuwa walimu, natamani wale walioonekana wana uwezo mkubwa ndio waingie kwenye huu mchakato. Tutengeneze walimu ambao watoto wetu watatazamia kuwa kama wao na hapa ndipo hamasa ya kweli inapopatikana.
Nzuri hii point.
Ahsante Faraja S
 
Back
Top Bottom