Kesi ya Pinda yapigwa kalenda

Kesi ya Pinda yapigwa kalenda

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
pinda.png

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.PICHA |MAKTABA



KWA UFUPI
Ni kuhusu pingamizi lililowekwa na Serikali la ama iendelee kusikilizwa au itupwe.


Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana ilishindwa kutoa uamuzi wa pingamizi la Jamhuri katika kesi ya kikatiba inayomkabili Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa mara ya pili mfululizo na sasa imepanga kuutoa Juni 6, mwaka huu.

Kesi hiyo Namba 24 ya mwaka 2013, ilifunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu likiongozwa na Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu akisaidiana na Dk Fauz Twaib na Augustine Mwarija.

Katika kesi hiyo, walalamikaji wanadai kuwa Pinda alivunja Katiba kwa kauli aliyoitoa bungeni, Juni 20, 2013, wakidai kuwa ni amri kwa vyombo vya utekelezaji wa Sheria kuwapiga wananchi, wakati wa vurugu.

Pamoja na mambo mengine, wanaiomba Mahakama itamke kuwa kauli hiyo ni kinyume cha Katiba na imwamuru Pinda aifute hadharani.

Hata hivyo, walalamikiwa kupitia jopo la mawakili wanne wa Serikali likiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG), George Masaju waliweka pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo.

Awali, uamuzi wa pingamizi hilo ulitarajiwa kutolewa Aprili 17, mwaka huu lakini Mahakama ilishindwa na kupanga kuutoa jana. Kabla ya kushindwa tena na kupanga kuutoa Juni 6.

Hakuna sababu zozote zilizotolewa za Mahakama hiyo kushindwa kutoa uamuzi huo jana na wadaiwa waliofika mahakamani hapo kusikiliza uamuzi huo walipewa hati ya wito wa kufika mahakamani tarehe hiyo mpya kwa ajili ya uamuzi.

Uamuzi huo ndiyo utakaotoa hatima ya kesi hiyo. Ikiwa Mahakama itakubaliana na pingamizi hilo, basi kesi hiyo itatupiliwa mbali na iwapo italitupilia mbali, kesi hiyo itaingia katika hatua nyingine ya kupangiwa tarehe ya kusikilizwa.

Katika pingamizi hilo walalamikiwa wanadai kuwa kesi hiyo ni batili na iko mahakamani isivyo halali kwa kuwa inakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 na Sheria ya Mamlaka, Kinga na Haki za Wabunge ya mwaka 1988.

Mawakili hao wanadai kuwa Pinda analindwa na Katiba Ibara ya 100 (1) na (2), ambazo zinamkinga mbunge kushtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kwa jambo lolote alilolisema, alilolitenda au aliloliwasilisha bungeni kwa njia ya maombi, muswada au hoja.

Upande wa walalamikaji unaowakilishwa na mawakili Harold Sungusia na Fulgence Massawe (LHRC), Mpale Mpoki, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya (TLS), katika majibu yao wanadai kuwa walalamikaji wana haki ya kushtaki.

Wanadai kuwa kinga ya mbunge ina mpaka na inalindwa kwa shughuli za Bunge tu, huku wakidai kuwa hati hiyo haina dosari na kwamba hata kama zipo dosari za kisheria, zinaweza kurekebishwa.Pinda alitoa kauli hiyo inayolalamikiwa katika mkutano wa 11 wa Bunge, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu Bungeni.
Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, kuhusu msimamo wa Serikali, hususan malalamiko dhidi ya vyombo vya dola katika baadhi ya maeneo kama Mtwara, kuwapiga wananchi. "Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu... Eeh, hamna namna nyingine, eeh maana lazima tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria...

"Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine, eeh… maana tumechoka," inasomeka hati ya madai ikinukuu maneno ya Pinda.

Chanzo:
mwananchi.co.tz


 
Back
Top Bottom