Kifo cha Patrice Lumumba katika mswada wa kitabu "Under the shadow of british colonialism" Ally Sykes and Mohamed Said

Kifo cha Patrice Lumumba katika mswada wa kitabu "Under the shadow of british colonialism" Ally Sykes and Mohamed Said

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
1145059


Naweka hapo chini kipande kutoka katika mswada wa kitabu cha maisha ya Ally Sykes, ''Under the Shadow of British Colonialism,'' kipande ambacho Ally Sykes anaeleza mauaji ya Lumumba yalipotokea wao katika TANU pamoja na Mwalimu Nyerere walijisikiaje.

Pamoja na haya kudai uhuru wa Tanganyika Ally Sykes anaeleza pilikapilika alizokuwanazo katika kushughulika na biashara zake:

''Mwezi December 1960 tulimleta Eduardo Masengo Dar es Salaam kutoka Nairobi kuja kufanya maonesho.

Lakini Masengo hakuwa mwanamuziki pekee aliyekuja Dar es Salaam.

Kabla yake tulimleta Msafiri Mori Mori na band yake Sportsman Cha Cha Band iliyokuwa inatangaza sigara za Sportsman.

Rafiki yangu Julius Nyerere na mtu wangu wa karibu sana ndiye alikuwa Mgeni wa Heshima katika onesho lile pale Ukumbi wa Arnautoglo.

Peter Colmore alikuja kutoka Nairobi kwa shughuli hii na nikachukua fursa ile kumjulisha kwa Nyerere.

NilimpeIeka Colmore nyumbani kwa Nyerere Magomeni Majumba Sita alipokuwa anaishi.

Siku ile Nyerere hakuwa na raha kwa kuwa taarifa zilikuwa zimetufikia kuwa Lumumba alikuwa ameuawa.

Magazeti yalikuwa yameandika kuwa Lumumba alikuwa kakamatwa Port Francqui baada ya baada ya kutoroka alipokuwa amezuiwa katika nyumba mjini Leopoldville.

Siku chache kabla ya haya kutokea Wabelgiji walikuwa wametoa amri ya Lumumba kutafutwa na iliaminika kuwa Lumumba alikuwa anaelekea Stanleyville ambako wananchi waliokuwa wanamuunga mkono walipokuwa.

Magazeti yalichapa picha ambayo ilikuja kuwa mashuhuri sana ya Lumumba akiwa kafungwa kamba mikono nyumna yuko nyuma ya lori na askari wa Kibelgiji wakimlinda.

Lumumba wakati ule alikuwa tayari keshapoteza nafasi yake ya Waziri Mkuu wa Congo na alikuwa anarudishwa Leopoldville.

Sisi tukiwa wanachama wa TANU tunaosubiri kupata uhuru tulikuwa tukifuatilia mambo ya Congo kwa umakini mkubwa.

Hali ya mambo yalikvyokuwa yanakwenda yalikuwa yakitusikitisha sana.

Palikuwa na taarifa ya kuasi kwa Jeshi la Congo na askari wakiwakamata Wabelgiji wake kwa waume na watoto na wakiwapiga.

Mimi binafsi nilikuwa nayafuatilia haya mambo kwa karibu zaidi kwa kuwa kwa wakati ule naamini mimi nilikuwa mtu pekee niliyefika Congo na kushuhudia ubaya wa ukoloni wa Wabelgiji dhidi ya Wakongomani.

Masengo alisikitika sana kusikia taarifa kutoka Katanga nyumbani kwao kuwa jimbo hilo limejitenga kutoka Jamhuri ya Congo na liko chini ya Moise Tshombe..

Masengo alikuwa anatoka kabila la Bayeke kabila sawa na Tshombe.

Nyerere akimchukia Tshombe kupita kiasi.

Tukachukua nafasi hii kumpeleka Masengo Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC) kurekodi nyimbo zake za zamani.

Waliporudi Nairobi Colmore na Masengo wakaniandikia barua, Colmore akinishukuru kwa kumtambuisha kwa Nyerere na Masengo kwa kuiratibu vyema safari na maonyesho yake.

Colmore alinieleza kuwa alikuwa ameshukuru kwa Nyerere kuwa na msimamo thabiti katika suala la Congo.

Wakati ule Masengo alikuwa tayari keshaingizwa katika kampuni ya High Fidelity Productions kama mkurugenzi.

Colmore alikuwa mtu wa kuona mbali.

Alitambua kuwa tutahitaji msaada wa Nyerere ikiwa tutataka kupanua biashara yetu katika Tanganyika huru.

Ndiyo maana kule kumjulisha yeye kwa Nyerere lilikuwa jambo muhimu sana kwake.

Colmore alikuwa anajua urafiki mkubwa uliokuwapo baina yangu na Nyerere, kiongozi mkuu mtarajiwa wa Tanganyika.

Mimi na Colmore tulikuwa na matarajio makubwa katika uhuru wa Tanganyika kuwa tutapata mafanikio makubwa katika kampuni yetu.

Hadi hapa tuliona mafanikio katika ndoto iliyokuwa inaelekea kuwa kweli.

Biashara za Colmore zilikuwa zinapanuka na Tanganyika ilikuwa sehemu muhimu ya biashara hii kiasi alijenga nyumba Moshi na kila mwisho wa juma alikuwa akiendesha gari yake kutoka Nairobi kuja Moshi.

1145062


1145060


1145064


Picha: Lumumba, Ally Sykes na Julius Nyerere Magomeni Majumba Sita, 1958, Julius Nyerere na Eduardo Masengo Majumba Sita, 1960 na Peter Colmore kulia na mgeni wake nyumbani kwake Muthaiga Nairobi, 1995 picha hii nilipiga mimi zilizobakia ni kutoka Maktaba ya Ally Sykes.
 
Back
Top Bottom