Mzozo wa umilki wa BOT kutatuliwa kwa nyaraka kati ya Z'bar na Tanzania Bara
Na Salma Said, Zanzibar.
SAKATA la hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) sasa limechukua sura mpya, baada ya kikao cha kamati ya kero za Muungano kukubaliana kila upande uwasilishe ushahidi wa nyaraka ilizonazo kuhusina na suala hilo.
Akijibu swali katika baraza la Wawakilishi jana, Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, alisema katika kikao cha mwisho cha kamati hiyo kilichofanyika mwanzoni mwa
wiki hii, SMZ na Serikali ya Muungano walikubaliana kila upande uwasilisha nyaraka zinazohusiana na suala hilo kama ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.
Waziri Hamza alisema kwa upande wa Zanzibar wana nyaraka hizo ambazo zitatumika kama ushahidi jinsi benki hiyo ilivyoanzishwa na hati za kila mwanachama kwa pande zote za muungano.
''Napenda kueleza kwamba SMZ iko makini sana kufuatilia suala hili kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi, Ofisi ya Waziri Kiongozi na Uratibu wa Uchumi na Uhusiano wa Kimataifa,'' alisema waziri huyo.
Alisema mara baada ya kuthibitishwa kwa hisa za SMZ BoT, hatua nyengine zitafuata na kuwahakikishia wajumbe wa baraza kwamba SMZ inafuatilia suala hilo kwa makini.
Hamza aliwaahidi wajumbe kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi katika kikao kijacho cha kamati ya pamoja inayoshughulikia kero za muungano.
Alisema katika kikao kilichopita cha kuzipatia ufumbuzi kero za muungano wamekubaliana kwa pamoja kwamba Katibu Mkuu Kiongozi atoe kibali kwa Benki Kuu kutoa nyaraka zinazoonyesha mmiliki wa taasisi hiyo.
Swali la msingi liliulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Magogoni (CCM), Daud Hassan Daud aliyetaka kujuwa hatma ya suala la hisa za Zanzibar BOT.
''Tulikubaliana kwamba Katibu Mkuu Kiongozi atoe kibali cha kupatikana kwa nyaraka zinazoonyesha mmilikii wa taasisi hiyo,'' alisema Waziri Hamza.
Alithibitisha kwamba kuna mgogoro wa umiliki katika taasisi hiyo, huku Zanzibar ikidai kwamba ina hisa zake katika benki hiyo na kwamba wana uhakika SMZ imechangia uanzishaji wa benki hiyo.
Source: Mwananchi