Nimemjua Dr Slaa kwa muda mrefu sana na najua kuwa alikuwa mtendaji muhimu sana katika kamati mbalimbali nyeti ambazo Mwalimu Nyerere alimtumia kuweka mambo sawa. Naamini Dr Slaa ni mmoja wa mtu ambaye anamjua sana Mwalimu Nyerere lakini pia anajua vilivyo ni jinsi gani Mwalimu Nyerere alikuwa makini sana katika kushughulikia mambo nyeti kama hili la masuala ya mahusiano na mshikamano wa watanzania. Haswa suala hili la maslahi ya Wakristo Vs Maslahi ya Waislamu ambalo daima limekuwa likitokota chini kwa chini na sasa limeletwa katika majukwa ya kisiasa.
Kitendo cha yeye kutoka hadharani, katika nyakati zilizogubikwa na joto la ushabiki na hata chuki za kisiasa kutokana na uchaguzi nay eye kusema ama kushutumu kuwa Kikwete amekuwa akipendelea Waislamu ama hata kusema neon linaloleta maana kama hiyo ni kitendo ambacho kitatugharimu watanzania na zaidi CHADEMA kwa muda mrefu sana, iwe ameshinda uchaguzi ama ameshindwa.
Naamini Dr Slaa hajaropokwa ama kuingiwa na mdadi wa uwezekano wa kushindwa na umati wa watu aliokuwa nao wakati huo na hivyo kujisahau na kuongea hovyo kama ambavyo wanasiasa wengi hujikuta wakifanya. Naamini kuwa Dr Slaa amesema hayo huku akiwa na kitu maalum alichokilenga.
Hivi karibuni nilipata fununu kuwa CHADEMA wameamuru wagombea wao kuwasiliana na Maaskofu na viongozi wengine wa kanisa la katoliki kuangalia uwezekano wa kutumia mtandao wa kanisa kuhakikisha kuwa wanalinda kura zao. Msisitizo ulitolewa kwa zile sehemu ambazo CHADEMA kimeshindwa kujiwekeza vya kutosha na hivyo kutokuwa na uhakika wa kupata watu madhubuti wa kulinda kura zao. Nasikia kuwa tayari kuna Maaskofu ambao wamewaamuru wakuu wa vigango mbalimbali kuwahamasiaha vijana wao kujitolea kuisaidia CHADEMA katika zoezi hilo.
Nina wasiwasi moja ya malengo ya Dr Slaa kuongea hayo aliyoyasema katika viwanja vya kawe ni maandalizi ya kujilinda na makombora ya CCM yanayokuja hivi sasa kudai kuwa CHADEMA wamakuwa wakitumia mfumo wa kanisa kufanikisha ushindi ikiwemo hili la ulinzi wa kura.
Kwa kweli Dr Slaa amepotoka na sitashangaa kuona kuwa mara baada ya uchaguzi huu na endapo CHADEMA watashindwa kupata urais na kutofanikiwa kupata viti vya ubunge kufikia lengo lao la viti 100, basi chama hicho kitaingia katika mgogoro mkubwa ambao sidhani kama watatoka salama kama ilivyojionyesha hapo awali.
Nasema hivyo kwa kuwa naamini kuwa CHADEMA wanafanya makosa yaleyale ya CUF waliyoyafanya hapo nyuma na kuambulia kubaki kuwa ni chama cha asilimia 7 10 ya watanzania milele amina. CHADEMA inaweza kuwa chama cha asilimia 15 -20 milele amina kwani wakati CUF kinaendelea kuwa chama cha Waislamu wanaodhani kuwa serikali ya CCM ni adui wa maslahi yao, CHADEMA mara baada ya uchaguzi huu kitakuwa ni chama cha Wakristo wanaodhani kuwa serikali ya CCM ni adui wa maslahi yao pia.
Ubaya wa hili ni kuwa chama kinadumaa na kukosa uwezekano wa kutanuka na ukichukulia kuwa kuna kila uwezekano wa CCM kuwa na mgombea Urais Mkristo kama ilivyo utamduni waliojiwekea. Wale wote walioenda CHADEMA kutokana na hisia ama chuki za kudhani ama kuona kuwa CCM ya Kikwete inapendelea waislamu ni dhahiri watarudi nyumbani kujipanga upya na nyumbani huko kutakuwa CCM na sio CHADEMA.
Lakini pia matamshi kama haya nay ale ya kuwa CCM wameingiza kura kwa malori, jeshi lina nia mbaya na yeye na CHADEMA huku akijua wazi kuwa lile ni tamko la Kamati ya Ulinzi na Usalama ambayo anajua vilivyo uwezo na utendaji wake lakini pia lie la kuwa nusu ya maafisa wa usalama wanaripoti kwake akijua akuwa kuna ukweli wa kimazingira uliojengwa na historia yake, ni matamshi ambayo hata kama hayataleta machafuko wakati wa uchaguzi na baada ya hapo, lakin yatasumbua sana uendeshaji wan chi kwa yeyote Yule atakayekuwa madarakani huko tuendako.
Ni wazi kuwa kwa matamshi yake hayo, Dr Slaa ameshafukuza kura chache za waislamu ambao walikuwa tayari kuziba masikio ya propaganda za watu na mashehe hovyohovyo ambao wamekuwa wakipita mitaani na misikitini kudai kuwa Dr Slaa ni pandikizi la Kanisa na Kanisa linamchukia Kikwete sio kutokana na mapungufu yake kiutawala lakini chuki dhidi ya waislamu na maslahi ya waislamu.
Dr Slaa amejinasabisha na propaganda hizo kwani aliyoyasema ndiyo ambayo Waislamu hata wale ambao bado wamekuwa na moyo wa kumuunga mkono wamekuwa wakiyalalamikia.
Na katika hili, kuna wakati niliwahi kulifuatilia ili kujua kama kweli kuna ukweli wowote haswa pale nilipokutana na kuongea na Askofu mmoja ambaye alinihakikishia kabisa kuwa hivi sasa tuna wakuu wa mikoa wengi waislamu kuliko wakristo.
Nilipofuatilia nikakutana na hali hii hapa chini ambayo naamini bado haijabadilika.
- Katika ofisi binafsi ya rais kuna wateule 13 na kati yao 9 Wakristo 7 Waislamu
- Makamu wa Rais Muislamu na hili ni wazi linalazimika kutokana na matakwa ya muungano
- Waziri Mkuu ni Mkristo
- Kati ya Mawaziri 26, 16 ni wakristo na 10 Waislamu
- Kati ya manaibu mawaziri 21, Wakristo 13, Waislamu 8
- Makatibu Wakuu wapo 26 na kati yao Wakristo 15m Waislamu 8
- Manaibu makatibu wakuu wapo 23, kati yao 15 wakristo, 8 Waislamu
- Mwanasheria Mkuu ni Mkristo
- Mkaguzi Mkuu wa Serikali ni Mkristo
- Katibu Kiongozi ni Mkristo
- Taasisi ya Rushwa ni Mkristo
- Kati wa mabalozi 32, wakristo 14 na Waislamu 18
- Katika majeshi na vyombo vya ulinzi hali ni kama ifuatavyo;
- Jeshi la Ulinzi, Mkuu wa Majeshi ni Mkristo na Mnadhimu Mkuu ni Musilamu na Mkuu wa JKT ni Mkristo
- Usalama wa Taifa Mkureguzi Mkuu ni Muislamu na Msaidizi wake ni Mkristo
- Mkuu wa Polisi ni Muislamu na Mwendesha Mashtaka Mkuu ni Mkristo
- Kamishina Mkuu wa Magereza ni Mkristo
- Jaji Mkuu ni Mkristo na Jaji Kiongozi ni Muislamu
- Katika jumla ya wakuu wa mikoa 26, Wakristo ni 14, Waislamu ni 12 lakini kati yao watano ni kutoka Zanzibar ambako uwezekano kubwa ni kuwa watakuwa waislamu kama ilivyo suala la mgombea mwenza.
- Wakuu wa wilaya jumla yao ni 120 na kati yao Wakristo ni 77 na Waislamu ni 43 ambao 10 ni kutoka Zanzibar.
- Wakuregenzi wa Mikoa wapo 26 na kati yao 16 ni wakristo na 10 ni waislamu
- Katika makamishina wakuu hali ni kama ifuatavyo;
- Kamishana ya Utumishi wa Umma ni Mkristo, Kamishna ya Maadili ni Mkristo, Kamishna ya Haki za Binadamu na Utawala bora ni Mkristo, Kamishna ya Uchaguzi ni Mkristo,
- Ukija katika wakuregenzia wakuu hali ni kuwa kati ya 25 ambao nimeweza kuwapitia, 19 ni Wakristo na 5 ni Waislamu.
Bado teuzi zingine ambazo nazifanyia kazi ambazo ukweli hali ni kama inavyojionyesha hapo juu.
Sasa mtu kama Dr Slaa anapokuja na hoja kuwa Kikwete ni mdini kwa kweli nashindwa kumuelewa lakini zaidi ananifanya nijiulize kama ile kauli mbiu ya UMAKINI anaiamini ama ni kivutio kura tu. Ukosefu wa umakini wa hali ya juu alionyesha katika hili sidhani kama utamuwezesha kupata heshima anayostahili pale atakapokuwa mkuu wa vyombo vya dola ambavyo navyo kutokana na siasa hovyo kama hizi vimeaanza kugawanyika katika misingi hiyo.
Na kwa kweli katika picha tunayoipata hapo juu ni vigumu kuelewa mtu kama Dr Slaa na wengine ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiamini kuwa Kikwete ni mdini kwa kuwa napaendelea waislamu katika teuzi zake. Ni wazi kuwa Mzee wangu Dr Slaa ambaye niliwahi kumutmikia kwa imani kubwa wakati Fulani ama ameamua kufanya lolote ili mradi wake wa Urais ufanikiwe ama ni mmoja wale ambao wanaamini kuwa ni watu wa kundi fulani, dini fulani, kabila fulani ama kutoka katika maeneo fulani tu ndio wenye haki ama uwezo wa kuongoza taifa letu na sio wengineo.
Mitazamo kama hii si migeni katika dunia yetu na yote imepelekea maafa makubwa. Mitazamo ka hii ndiyo iliyopelekea machafuko ya Kenya mwaka 2007 kutokana na Wakikuyu kuamini kuwa na hodhi ya utawala,. Huko Uganda kati ya Banyankole ya Museveni na wengineo. Lakini hatari zaidi ni yale ya Burundi na Rwanda ambako kwa muda mrefu kundi moja kati ya Wahutu ama Watutsi wamekuwa wakiamini kuwa wao ndio wenye uwezo wa kuongoza na wengine watakuwa wamependelewa tu.
Mitazamo kama hii ndio chimbuko kubwa la vuguvugu la TEA PARTY ambalo limeibuka nchini Marekani mara baada ya mswahili Baraka Obama kupata nafasi ya kuongoza taifa hilo. Kama ilivyo hapa, mambo mengi ni ya uzushi , hisia potofu na yenye kulenga kuzusha mazingira ya chuki na hofu miongoni wa watu. Maneno kama haya ndiyo yamekuwa silaha kuhimu kwa wanavuguvugu hawa wakiongozwa na wanasiasa waliokosa umakini ama wale waliojitokeza wazi kama Sarah Palin ama wale wanaojifinya nyuma kama wengi katika chama cha kihafidhina cha Republican.
Ni wazi kuwa Dr Slaa amepotoka na maji yameshamwagika na sioni dalili za usalama katika chama nilichowahi kuwekeza imani yangu hapo kabla cha CHADEMA lakini zaidi kwa nchi yetu kwa ujumla.
Sikupenda kuleta masuala kama haya mtanadaoni lakini ukweli katika hali tuliyofikishwa na hawa viongozi ambazo wakati fulani tuliwahi kuwaamini kuwa ni wazalendo wa kweli, imenibidi kufanya hili ili kuweka wazi ukweli wa mambo badala ya kuacha wingu la siasa za fitina na majungu kutawala imani na mitizamo ya watanzania.