Prof. Kahigi: Tegemeo la Bukombe
Na NdimaraTegambwage - Imechapwa 22 September 2010
"NENDA upinzani, sisi tutakuunga mkono!" Hiyo ndiyo sauti ya umma iliyomwelekeza Prof. Kulikoyela Kanalwanda Kahigi kuvuka mstari – kutoka CCM kwenda CHADEMA.
Ni vyama viwili vikubwa vinavyofahamika katika jimbo la Bukombe – Chama cha Demokrasia na Maendeleo na Chama Cha Mapinduzi.
Yaliyompata Kahigi ndiyo yalimpata Dk. Willibrod Slaa wakati akitafuta ubunge wa Karatu miaka 15 iliyopita kupitia CCM. Jina lake, tena akiwa mshindi kwa mbali, lilitupwa.
Mafundi ujenzi wa CCM hawakujua kuwa walikuwa wanakataa jiwe muhimu ambalo lingeimarisha mihimili mikuu. Ndivyo ilivyotokea pia kwa Prof. Kahigi.
Historia imetufunza kukataa kukasirika; kwani kukasirika kunaleta jazba na maamuzi kengeza.
Tumefunzwa kuchukia na tumezingatia. Ukichukia unachukua hatua. Ndivyo alivyofanya Dk. Slaa ambaye leo hii anachora ramani ya ajenda kuu za uchaguzi mkuu mwaka huu.
Ndivyo alivyofanya pia Prof. Kahigi wa Bukombe. Hawakuhamaki. Hawakukasirika. Walichukia kilichotendeka. Wakauliza wazee na vijana. Wakashauriwa: "Nenda kule tutakufuata."
Kahigi alizaliwa Agosti 1950. Katika umri huo tayari amesoma hadi chuo kikuu na kujizolea shahada ya kwanza (1976), shahada ya pili – ya umahiri (1977) na shahada ya udaktari wa falsafa (1988).
Katika umri huo pia Kahigi amefanya ufundishaji, tathmini na utahini katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi.
"Nimeipenda kazi yangu na kuifanya kwa dhati kwa miaka yote," anasema Kahigi wakati akielezea familia yangu jijini Dar es Salaam juu ya uamuzi wake wa kugombea ubunge.
Huku akitabasamu aliongeza, "Lakini huku pia kuna kazi, tena nzito, ya kufanya kwa ushirikiano na wananchi ambao wamekuwa chimbuko la ‘raslimali' tunazotumia kufundishia na kuandika vitabu."
Kahigi ambaye ameandika na kuchapisha zaidi ya vitabu 10 na makala nyingi za kitaaluma katika majarida ya kitaifa na kimataifa, anabeba kauli ya ushirikiano kwa wakazi wa Bukombe. Anasema, "Maendeleo sahihi yanawezekana tukishirikiana."
Anaonyesha nia hiyo katika shairi lake la Mei – Juni 2005:
Wimbo wangu, sasa toka, leo kifupi eleza:
Shakawa ziloifika, wilaya zikaimeza
Watu wakahamanika, kwa shida za kuumiza
Kote wakazongomeka, utu wakaupoteza.
Mwambieje wanati, wenye uchungu wa dhati
Waiache atiati, waendeshe harakati
Umoja wauzatiti, kwa kiapo na kwa hati
Wainuke wasiketi, wajihami madhubuti.
Niwelezeje lukuki, wafikwao uonezi
Kwamba jambo lilobaki, ni kutenda ukombozi
Ni kwa dhati kudiriki, kuupindua uozi
Madhalimu kuwadhiki, na kuleta MAGEUZI.
Ni ndoto ya masafa? Ni dhamira? Ni utashi ndani ya kauli? Namfahamu Kulikoyela Kanalwanda Kahigi. Hutenda asemacho. Hufanana na kauli yake. Aweza kufanana pia na wananchi wa Bukombe au jinsi anavyotaka wawe kupitia utetezi wake.
Miaka ile nilipokuwa sekondari, wanafunzi waliokuwa wakiapa kuwa wakienda chuo kikuu watasomea sheria, wengi walikuwa na historia ya wao, wazazi au nduzu zao kunyang'anywa au kunyimwa haki. Walitaka kuwa watetezi na walinzi wa haki.
Kahigi anataka kuwa mtetezi wa wananchi katika mazingira ambamo anaona hawana mtetezi:
Wengi wamekuwa wezi, utajiri kuwania
Mbinu zao ziko wazi, kwa hakika twazijua
Fedha za sera azizi, kwa hila hujichotea
Na hutumia ghawazi, kuhonga kila njia.
"Nataka niwe karibu na wananchi. Tushirikiane. Inawezekana." Haya ndiyo maneno aliyokuwa akisema Kahigi mara kwa mara wakati tukipata chakula cha mchana alipokuja kueleza familia yangu kile alichodhamiria, wiki mbili zilizopita.
Bali anasikitikia sana CCM. Anasema hata wananchi wa Bukombe wanajua sasa kuwa chama hicho ni hatari ya kuepuka kwani "kilipora ushindi wao."
"Nilishiriki mchakato wa kura za maoni CCM. Niliongoza kwa ushindi wa kura za vituoni," anaeleza Kahingi na kuongeza kuwa wahusika walichelewesha kutangaza matokeo (toka Agosti 1 hadi 4) na hatimaye kutangaza mbunge anayemaliza muda wake, Emmanuel Luhahula kuwa ndiye mshindi.
Kahigi anasema akisimama na vyama vingine walishinikiza kurudia hesabu vituoni na kugundua kuwa Luhahula alikuwa na "kura hewa" kutoka matawi ya kata za Uyovu na Iyogelo ya Zamani. Bado CCM wilaya walimpitisha waliyetaka.
Pingamizi la Kahigi wilayani lilitupwa. Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Siasa, hata hivyo, walibaki upande wake. Kamati ya siasa mkoa ilijadili pia na kukubali kuwa mshindi ni Kahigi.
Kahigi anasimulia Kamati Kuu iliyokaa mjini Dodoma, ilivyompitisha lakini Halmashauri Kuu "ikapindua" uamuzi wa Kamati Kuu na ule wa wanachama na kumtangaza Luhahuka kuwa mgombea.
Kwa kauli yake, "Safari ya kugeuka ilikuwa imeanza. Sababu ilikuwa wazi. Haki za namna mbili zilikuwa zimebakwa: Haki ya mopigakura kumchagua mtu anayemtaka na haki ya mgombea kuchaguliwa na watu wanaomtaka. Baada ya uamuzi kufanyika hapakuwa na kurudi nyuma."
Profesa Kahigi siyo mgeni katika minyukano. Sisi tuliomwona katika uchanga wake na kufuatilia vitabu, makala, mashairi na mihadhara yake darasani, yeye ni mkondo usiozimwa – ama utavunja vizuizi au utatafuta upenyo mpya.
Haongei sana lakini kauli yake inapenya. Ana tabia ya kudadisi mkubwa kwa mdogo na kirafiki. Kwa njia hii hukusanya lililoko nyoyoni mwa wengi.
Makazi ya Prof. Kahigi – pale Kabuhima, Uyovu – ndiko chemchemi ya taarifa za kampeni. Kutoka hapa, siyo tu wanachama na viongozi wa Chadema, bali hata wanachama wa vyama vingine na wale wa CCM, wanapokea na kusambaza ujumbe wa anayeweza kuwa mbunge mpya kesho.
Prof. Kahigi amekuwa mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM); Mkuu wa Idara ya Kiswahili, Mwenyekiti Mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania, Mhariri Mkuu wa majarida ya UTAFITI na KIOO CHA LUGHA; mhariri mkuu wa Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania na Mradi wa Lugha za Tanzania.
Huyu ni mwandishi wa vitabu vipatavyo 10 vingi vikiwa vya fasishi na vinatumika katika shule na vyuo.
Moja ya kazi za heshima ambayo haiwezi kufutika haraka ni kuwa Msimamizi na Mratibu wa Mradi wa Kimataifa wa kutafsiri kwa Kiswahili, progamu za kampyuta (Microsoft: Office and Windows).
Hii ni kazi ya ukombozi iliyorahisisha matumizi ya kompyuta kwa wasiojua vema lugha nyingine isipokuwa Kiswahili.
Mbali na UDSM, Kahigi amefanya ufundishaji, tathmini na utahini Chuo Kikuu Huria (Tanzania), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Mt. Agustine, Mwanza.
Vyuo vikuu vya nje ni pamoja na Michigan na Kalamazoo (Marekani), Leiden (Uholanzi), INALCO (Ufaransa); vyuo vikuu vya Moi, Nairobi na Kenyatta (Kenya) na Makerere (Uganda).
Prof. Kahigi anasema, "Ndugu yangu, siendi kubahatisha. Nimesimama na walionita kugombe na walioniambia hama tutakufuata. Tunafanya kazi. Kama upepo hautabadilika, ushindi ni wetu." anasema kwa tabasamu.