Ngoma nzima hiyo:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jumatano, Februari 29, 2012
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amevialika vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, jumuiya za kidini, asasi za kiraia na makundi mengine ya watu wenye malengo yanayofanana kuwasilisha kwake orodha ya majina ya watu watakaoteuliwa kuwa Wajumbe wa Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba.
Mheshimiwa Rais ametoa mwaliko huo kupitia Tangazo la Serikali Na. 66 la tarehe 24 Februari, 2012 kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 6(6) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.
Kifungu cha 6(6) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011 kinamtaka Mheshimiwa Rais kualika vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, jumuiya za dini, asasi za kiraia, jumuiya, taasisi na makundi mengine ya watu wenye malengo yanayofanana kuwsilisha kwa Rais orodha ya majina ya watu kwa ajili ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume.
Kwa mujibu wa Tangazo hilo la Serikali, kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu, jumuiya ya kidini, asasi ya kiraia na kila kundi lenye watu wenye malengo yanayofanana itapaswa kuwasilisha orodha ya majina yasiyozidi matatu ambayo itaonyesha umri, jinsia, uzoefu, sifa na mahali anapoishi kila mtu aliyemo katika orodha.
Aidha, orodha hiyo inatakiwa iwasilishwe kwa Mheshimiwa Rais kwa maandishi ama moja kwa moja kwa mkono au kwa rejista ya posta kupitia anuani ifuatayo: Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu, S.L.P. 9120, DAR ES SALAAM Au Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Ofisi ya Rais, S.L.P. 4224, ZANZIBAR.
Mwisho wa kuwasilisha orodha ni tarehe 16 Machi, 2012.
Imetolewa na: Wizara ya Katiba na Sheria, Makutano ya barabara ya Sokoine na Mkwepu, S.L.P 70069,
DAR ES SALAAM,