RAISI WAJIBISHA WATENDAJI WAKO
Mheshimiwa Raisi Toka uingie madarakani kumekuwa na jitihada nyingi sana zinazofanywa na watendaji wako katika kuhakikisha unakuwa karibu zaidi na wananchi wako kwa njia rahisi zaidi za mawasiliano .
Toka umeingia madarakani watendaji wako wamekuwa wakitumia zaidi mitandao ya kimataifa yaani INTERNET kwa ajili ya kukuweka wewe karibu zaidi na wananchi wako , pamoja na jitihada hizi za kupongezwa kuna mengine yamefanyika inabidi sasa uwe macho na hawa watu .
Miaka miwili iliyopita mlianzisha tovuti maalumu kwa ajili ya wananchi kutoa maoni yao , kipindi hicho watu mbali mbali walilalamika kuhusu gharama za tovuti hiyo hakuna aliyejali kujali kwa maana ya kutoa ufafanuzi kwa wananchi hata hivyo tovuti hii mpaka leo iko kimya .
Baadaye mlianzisha tovuti zingine ambazo zilikuwa zinafanana na hizo za kutoa maoni , naona kuna moja bado iko lakini imeshindwa kupambana katika soko ili kuweza kutambulika itumike kiurahisi na watu wengi zaidi maana yake iko kimya .
Halafu likaja hili la ikulu kuanzisha blogu yake ya mawasiliano ambayo ilikuwa imesajiliwa katika Google , si unakumbuka raisi ulienda kutembelea makao makuu ya google mwaka huu na wasaidizi wako ? wale ndio mlisajili blogu kwao , pamoja na kusajili imeandikwa mara chache sana mtu akitaka habari zozote inabidi atembelee blogu na mitandao mengine na sio blogu hiyo .
Mheshimiwa hakukuwa na sababu za msururu wa tovuti zote hizi pamoja na blogu hizi zote kwa sababu raisi aliyekutangulia alikuwa na tovuti maalumu ya ikulu na nyingine iliyokuwa inaitwa statehouse ilibidi kuendeleza tovuti hizi na kuweka hivyo vyote .
Kumbuka Ikulu sio mali yako wewe wala ya mwingine wowote yule , kiongozi aliyetoka alitambua hilo sio mali yake ndio maana akaacha tovuti hizo zenye majina ya ikulu , ili wewe ukiingia mtumie hizo na muziendeleze tofauti yake mmeziacha zote na kuanzisha zetu wenyewe hii sio tabia nzuri mheshimiwa .
Baada ya yote hayo leo tena nimesoma Barua toka ikulu kwa vyombo vya habari inayohusu mkutano wako kesho moja ya kitu kilichonichekesha na kunihuzunisha ni hili la kuweka email ya yahoo ambayo ni
swalikwarais@yahoo.com , inahuzunisha sana kwa sababu watendaji wako wameshindwa kubuni njia nzuri zaidi na bora kwa ajili ya wananchi kutoa maoni yao kwenye karne hii .
Anuani ya barua pepe hiyo imesajiliwa leo na ninaamini wakati wanasajili hawakusoma maelezo ya ziada kabla ya kuendelea na usajili hivi ikatokea sasa mtu akafanikiwa kuingilia anuani hiyo akachukua maswali hayo pamoja na mawasiliano mengine mtafanya nini ? halafu akaamua kuifuta mtafanya nini ? na suala la usalama wako hapo umeliwekaje ? .
Mheshimiwa kila unapotaka kusoma Ujumbe kwenye Anuani hiyo kama kweli utakuwa unaisoma , kumbukumbu zinabaki yahoo kwenyewe , kila unapojaribu kujibu maswali kutumia anuani hiyo inapoenda itajulisha ilijibiwa akiwa wapi kwahiyo uhalifu unaweza kuanza hapo na kuendelea sipendi kuona hili likiendelea
Kwa maslahi ya usalama Wako wewe mwenyewe raisi , wasaidizi wako na wengine ambao watakuwa kwa njia moja au nyingine wanatumia anuani hiyo nawaomba kabisa muache kutumia anuani hiyo andaeni njia nzuri za mawasiliano kati ya raisi na wananchi wake na hivi vyote vinaweza kufanyika kwenye tovuti ya ikulu ikitengenezwa vizuri tu .
Kingine mnatakiwa mfungue channel zetu kwenye tovuti zingine kama youtube hii ni kwa ajili ya video muwe mnaweka video zenu na vingine humo , Raisi wa sasa wa Marekani alisaidiwa sana na youtube katika kufanikisha mambo yake mengi .
Mheshimiwa raisi ulizindua Mkonga wa mawasiliano siku chache tu zilizopita kwa sasa mtandao uko haraka sana hakuna matatizo kama zamani naamini wasaidizi wako wakitumia advantage hii utafika mbali hata kwenye kampeni zako za mwaka 2010 utatesa sana .
Mwisho ni kukuomba wewe na wasaidizi wako muwe karibu sana na wataalamu wenu wa ICT katika utendaji wa kazi inawezekana hata hii ANUANI iliyotengenezwa leo pamoja na hizo BLOGU zimetengenezwa bila ridhaa ya wataalamu wenu wa ICT nah ii ni mbaya sana , hawa watu wanasomeshwa kwa pesa nyingi sana lazima tuone tofauti yao katika jamii .