Kikwete: Sikusudii kumtwanga Kagame

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
Afichua fununu za nia ovu za Rwanda

Asema hatuziamini, lakini hatuzipuuzi

Rais Jakaya Kikwete



Rais Jakaya Kikwete, ameeleza kuhuzunishwa na jinsi serikali na viongozi wa Rwanda walivyomtukana na kumkejeli, akisisitiza kuwa Tanzania haina ugomvi wala nia mbaya dhidi ya nchi hiyo.

Kadhalika Rais Kikwete, amesema uhusiano kati ya nchi mbili hizo umetetereka na kwamba unapitia katika kipindi kigumu.

Kwa upande wangu, binafsi, sijasema lolote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu, alisema Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Julai kwa taifa. Alisema si kwamba hajaambiwa yanayosemwa au hajui kusema au hana la kusema, ila hajafanya hivyo kwa sababu haoni faida yake.

Aliongeza kuwa haoni kama kuna mgogoro wa aina yoyote na kwamba busara inaelekeza kuwa, hakuna sababu ya kukuza mgogoro usiokuwapo huku akinukuu msemo wa Kiingereza kuwa, two wrongs do not make a right.

Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa Rwanda, kuwa kwa upande wetu hakuna kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na ushirikiano wetu. Mambo yapo vile vile, alisema.

Rais Kikwete, alisisitiza kuwa angependa Tanzania iendelee kuwa na uhusiano mzuri na nchi hiyo.

Alisema katika kipindi cha miezi miwili kuanzia Mei hadi sasa, uhusiano baina ya nchi hizi unapitia katika wakati mgumu.
UHASAMA
Alisema kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yake na Tanzania kwa ujumla, ni ushahidi wa kuwapo hali hiyo na kwamba angependa kuwahakikishia Watanzania na raia wa Rwanda kuwa:

Mimi, serikali ninayoiongoza na wananchi wa Tanzania tunapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na Rwanda, kama ilivyo kwa nchi zote jirani.
Kama majirani, kila mmoja anamhitaji mwenzake, hivyo lazima tuwe na uhusiano mwema na ushirikiano mzuri, alisema.

KUICHOKOZA RWANDA
Alisema yeye na serikali yake watakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi yoyote jirani au duniani.
Hatuna sababu ya kufanya hivyo kwani ni mambo ambayo hayana tija wala maslahi kwetu, alisema.
Aliongeza kuwa wakati wote Tanzania imejihusisha na mambo ya kukuza na kujenga ujirani mwema, kusaidia kuimarisha uhusiano kwa maslahi ya nchi zote.

MTIKISIKO
Rais Kikwete, alisema uhusiano unaelekea kupata mtikisiko baada ya kutoa ushauri kwa serikali ya Rwanda, kuzungumza na mahasimu wao.

Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa, kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike. Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa serikali za Kongo na Uganda, alisema.

Alisema alizungumza hayo katika mkutano ambao Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli yake na kwamba Rais wa Rwanda, Paul Kagame hakusema chochote.
Rais Kikwete, alisema baada ya Rais Kagame kurudi Rwanda, alitamka maneno ambayo hakupendelea kuyasikia.

Kwa kweli nimestaajabu sana na jinsi walivyouchukulia ushauri wangu na wanayoyafanya. Havifanani kabisa mimi nilifanya vile kwa kuzingatia mila na desturi zetu za miaka mingi katika ukanda wetu, alisema.

Aliongeza kuwa viongozi wamekuwa wakikutana katika mikutano na vikao mbalimbali kuzungumza na kushauriana kwa uwazi juu ya njia za kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea.

Rais Kikwete, alisema wakati wote yamechukulia kuwa ni mambo yanayozihusu pande zote, hivyo kupeana ushauri ni wajibu wa wote na mara nyingi ushauri kwa wanaogombana kuzungumza unatumika sana.

Iweje leo mtu kutoa ushauri ule lionekane jambo baya na la ajabu. Jambo la kushutumiwa na kutukanwa! Siyo sawa hata kidogo!! Ushauri si shuruti, ushauri si amri. Una hiyari ya kuukubali au kuukataa. Muungwana hujibu: Siuafiki ushauri wako.
Hakuna haja ya kutukana wala kusema maneno yasiyostahili wala kusema yasiyokuwapo na ya uongo, alisema.

Rais Kikwete, alisema pengine Rwanda wanalo jambo dhidi ya Tanzania ambalo Watanzania hawalijui, kwa maana nao wanasikia mengi yanayozungumzwa na kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi ya Rais na nchi hii.

Hatupendi kuyaamini moja kwa moja tunayoyasikia, lakini hatuyapuuzi, alisema.

HOTUBA YA SIKU YA MASHUJAA
Kadhalika alizungumzia hotuba aliyoitoa mkoani Kagera siku ya kuwakumbuka mashujaa, kuwa atakayeichokoza Tanzania atakiona cha mtema kuni, kama ilivyokuwa kwa Iddi Amini wa Uganda, haikumlenga mtu wala haikutaja taifa.

Alielezea kushangazwa kwamba kauli hiyo, imetafsiriwa visivyo na kupotoshwa na baadhi vyombo vya habari na hata vya nchi majirani wa Tanzania. Alisema tafsiri hizo ni potofu kwani hakumtaja yeyote katika hotuba hiyo.

Sikumtaja mtu au nchi , nilikuwa nazungumzia wajibu wa majeshi yetu na raia wa nchi yetu kulinda uhuru na mipaka yetu na kwamba hatutamruhusu mtu au nchi yoyote kutupokonya wala kuichezea haki yetu hiyo ya msingi, alisema.

Tuko tayari kuitetea hata kama gharama yake ni maisha yetu kama walivyofanya mashujaa waliolala Kaboya, alisema.

Rais Kikwete alisema katika hotuba yake hiyo, aliwakumbusha Watanzania kuwakumbuka mashujaa kwa kutambua wajibu wa kuwa tayari kujitolea muhanga kulinda uhuru wa mipaka ya Tanzania.

Alisema alichosisitiza ni utayari wa nchi kulinda mipaka yake na kwamba mfano wa mashujaa hao, ni fundisho kwa mtu yeyote anayetamani kumega kipande cha ardhi ya nchi hii, kwamba atakiona cha mtema kuni.

Alisema ulikuwa uamuzi muafaka na wa busara kufanya sherehe hizo Kaboya, kwani ndipo walipolala mashujaa waliopoteza maisha kutetea mipaka na uhuru wa Tanzania dhidi ya Idd Amin.

Rais Kikwete, alisema ujumbe huo ulihusu kuwakumbuka mashujaa wa taifa, kama ilivyofanyika Naliendele mkoani Mtwara mwaka juzi, walipozikwa mashujaa waliopoteza maisha kuisaidia Msumbuji kutetea uhuru wake dhidi ya wakoloni, makaburu na vibaraka wa ndani ya taifa hilo.


CHANZO: NIPASHE
Pia, soma: Kagame tells Kikwete "I will hit you......"
 
Mkuu ulikuwa wapi haya mbona tumejadili sana juzi na jana,haya tumekupata mkuu.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…