SoC04 Kila kijana atambue wajibu wake kuwa ni mhusika mkubwa zaidi katika kuleta mabadiliko na maendeleo katika taifa

SoC04 Kila kijana atambue wajibu wake kuwa ni mhusika mkubwa zaidi katika kuleta mabadiliko na maendeleo katika taifa

Tanzania Tuitakayo competition threads
Joined
Jun 17, 2024
Posts
7
Reaction score
5
Kijana ni umri wa ukuaji wa mwanadamu unaokadiliwa ni kuanzia miaka 16-45.Huu ni umri ambao mwanadamu huwa anakuwa na uwezo zaidi wa mambo mbalimbali ukilinganisha na umri aliotoka nyuma yake yaani utoto na ule auendeao yaani uzee. (Ikumbukwe kijana inamhusisha yule wa kiume au mwanaume na wa kike au mwanamke).

Kijana ni nguvu kazi katikabutekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kutumia akili au nguvu pasipo kusukumwa na mtu yeyote. Kijana katika umri huu anapaswa kujitambua zaidi kwa kutimiza wajibu umpasao kuutimiza ili kuleta maendeleo au mabadiliko.

Mfano kushiriki kikamilifu katika matukio ya taifa kikatiba, pia kujifunza mambo mbalimbali na kuimarisha mahusiano yake na jamii ili aweze kushirikiana nayo katika kuleta tija ndani ya taifa.Taifa lolote lenye vijana chanya,wawajibikaji, imara na wenye uwenzo katika nyanja mbalimbali huwa taifa imara na lenye maendeleo.

WAJIBU NA NAFASI YA KIJANA KATIKA KULETA MABADILIKO NA MAENDELEO YA TAIFA.

1. Kujitambua na kujenga uwezo wa kukabiliana na mazingira na changamoto.

Uelewa anaokuwa nao kijana wa kujing'amua yeye ni nani,anapaswa kufanya nini wakati gani na kwa namna gani. Kijana anapaswa kuwa na ukomavu wa akili unaompa uwezo wa kujiamini na kuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu mbalimbali kikamilifu. Kuzielewa changamoto na kutafuta namna chanya ili kuzikabili na kuzitatua.

2. Kuijua katiba ya nchi na kutekeleza wajibu wake kikatiba.
Katiba ni mwongozo wa sheria zinazosimamia kundi fulani la watu mfano taifa. Kijana anapaswa kuijua katiba na sheria zake ili kujua wajibu wake na haki zake. Kijana mkomavu anauwezo wa kushiriki katika matukio muhimu ya kitaifa pasipo kukwepa. Kijana lazima ashiriki uchaguzi katika kuchagua viongozi walio na maono ya kulisaidia taifa kupata maendeleo na wazalendo. Vilevile ana haki ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya jamii hadi taifa alizo na sifa nazo. Hii itamjengea ushirikiano na jamii katika kuleta mabadiliko na maendeleo kwenye taifa.

3. Kushirikiana na jamii katika kujenga hoja na kujadili mwenendo wa taifa.
Ushiriki wa vijana katika masuala mbalimbali ya kitaifa huwezesha viongozi kutenda kwa ari na umakini ili kuleta matokeo chanya. Taifa licha ya kuwa na mikakati mbalimbali inayowekwa na serikali lakini kuna wakati serikali inaweza kwenda tofauti na mikakati yake hii hupelekea rushwa na ufisadi. Kijana anaowajibu wa kupinga rushwa kwa nguvu zake zote kwani rushwa hupindisha sheria. Ni wajibu wa vijana kuwapinga viongozi wala rushwa na mafisadi kwa nguvu zao zote kwani hurudisha nyuma maendeleo ya taifa.

4. Kushirikiana na serikali katika kupanga na kutekeleza mipango na maono ya taifa.
Taifa lenye shauku ya maendeleo lazima liwe na mipango na maono ya sasa na wakati ujao. Hii ni mikakati mathubuti au dira ya utendaji wa shughuli mbalimbali za kuleta mabadiliko na maendeleo kwa muda fulani mfano mwaka mmoja hadi miaka 25 ijayo. Kijana ashiriki katika kupanga na kutekeleza mikakati na maono hayo. Kwakuwa mipango na maono ya sasa yasipopangiliwa vema na kusimamiwa vema huweza kuathiri kizazi cha kesho.Pia maono ni muhimu sana mno kwa taifa kwani ni mambo ambayo hayajafikiwa lakini huwa na tija sana yanapopangiliwa kwa maandishi ili kuyateleleza. Kila kiongozi aingiaye madarakani anapaswa kupita katika mipango na maono hayo na kuyatekeleza kikamilifu.

5. Kuwa mzalendo na kusimamia rasilimali za Taifa
Tanzania ili isonge mbele inahitaji vijana wazalendo, wanaojali masilahi ya Tanzania kuliko ya kwao binafsi. Kuwa mwaminifu katika kidogo hupelekea uaminifu katika makubwa.Tanzania ina rasilimali nyingi sana kama madini, mbuga za wanyama, misitu,gesi asilia n.k . Yafaa kutumiwa kwa usahihi kama tunu muhimu za kukuza pato la taifa. Kila kijana anao wajibu wa kulinda rasilimali hizi katika eneo lolote alilopo kijijini au mjini. Lazima aweze kutetea pasipo kuruhusu ujangili , utoroshwaji wala uharamu wa namna yoyote ile. Vijana wanao wajibu wa kuwakumbusha vongozi wanaopewa dhamana ya kusimamia taifa kuwa uongozi ni dhamana. Hivyo kila kiongozi ni lazima awe mzalendo kulipa taifa kipaumbele katika kusimamia ili kuleta mabadiliko na maendeleo.

WAJIBU WA SERIKALI KWA VIJANA KATIKA TAIFA.

1. Kuwasikiliza na kufanyia kazi hoja zao kuhusu taifa.
Vijana huona mwenendo wa taifa hivyo huwa wanakuwa na shauku ya kurekebisha mahali panapoonekana kuwa hapaendi sawa. Ni wajibu wa serikali kuwasilikiliza vijana na kuzifanyia kazi hoja na mapendekezo yao. Kiongozi asiyesikiliza watu wake ni kama kiongozi kipofu asiyejua alikotoka wala aendako. Hapa pia vijana wanao wajibu wa kushirikiana katika kuvumbua mambo ya msingi ili kuyawasilisha kwa viongozi wao yapate kutekelezeka kikamilifu.

2. Kuwashirikisha katika kuandaa mipango na maono ya taifa. Ukusanyaji wa maoni kwa raia kama vijana wakati wa kupanga mipango na maono ya taifa, hupelekea serikali kuwa na mipango na maono yanayolenga matabaka yote katika jamii. Vijana wanao uwezo wa kutambua changamoto na mapendekezo ya kuzitatua. Serikali iwatumie zaidi hawa kwakuwa uwezo wao wa kufikiri pia ni mkubwa wanao uwezo wa kuitambua kesho(maisha yajayo) kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia hivyo kuwa na mipango na maono inayoendana na mabadiliko ya ulimwengu.

3. Kuwapa nafasi za kugombea nafasi za uongozi na kuteuliwa katika nyadhifa mbalimbali.
Uwezo wa maamuzi wa vijana huambatana na vipaji mbalimbali. Wapo wenye uwezo kusimamia au kuongoza na kuleta mabadiliko katika taifa. Kuaminiwa kwa vijana katika uongozi huweza kuleta matokeo chanya. Yafaa vijana kuwa waadilifu sana katika kutekeleza majukumu ya uongozi kwa kuzingatia miiko ya uongozi pasipo upendeleo wala kukiuka sheria za nchi.

4. Kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za maendeleo binafsi,jamii na taifa.
Kazi ni msingi wa maendeleo ya taifa . Kijana yeyote lazima ashiriki kikamilifu katika kufanya kazi. Haiwezekani kupata mabadiliko na maendeleo katika taifa ikiwa vijana hawatajishughulishi katika kazi za uzalishaji kama kilimo, biashara, uchimbaji madini, uvuvi , shughuli za viwandani na ufundi mbalimbali. Huu ni wakati wa kila kijana kufanya kazi kisasa ili kuongeza uzalishaji zaidi. Serikali inao wajibu wa kuwawezesha vijana katika kuzalisha mfano kutoa ruzuku mbalimbali katika pembejeo za kilimo, vifaa vya uvuvi na uchimbaji wa madini na mitaji. Hii inaenda sambamba na kutafuta soko imara la bidhaa ndani ya taifa na kimataifa ili uzalishaji uwe na tija zaidi na kuboresha miundombinu mbalimbali mfano barabara,nishati na mawasiliano. Hii itapelekea vijana kujituma zaidi pia itapunguza tatizo la ajira kwasababu vijana watajiajiri katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.

5. Kuwaajiri vijana wenye sifa katika fani mbalimbali na kuwatengenezea mazingira mazuri ya wengine kujiajiri.
Serikali inao wajibu wa kuwa na mfumo bora wa elimu ili kutoa elimu yenye viwango bora vitakavyomwandaa kijana kuwa na ujuzi stahiki. Shule ni kama chungu, ukipika vizuri hutoka chakula bora na kitamu(utafurahi kukila), lakini ukipika vibaya chakula chake huwa hata hakitamaniki kukila. Fani mbalimbali kama ualimu, udaktari, usimamizi wa taarifa n.k . Hutoa wahitimu wake kila mwaka hivyo serikali inao wajibu wa kuwaajiri wale watakao kidhi vigezo vilivyowekwa katika fani husika. Vijana wanapokuwa katika majukumu hayo huongeza ubora wa huduma , utendaji kazi wa kuridhisha na kulisaidia taifa kuwa na maendeleo katika sekta mbalimbali. Hii huenda sambamba na serikali kutengeneza mazingira mazuri kuwezesha vijana kujiajiri katika taifa.

MAMBO YA KUEPUKA KIJANA ILI KULETA MABADILIKO NA MAENDELEO KATIKA TAIFA.

1. Kuepuka uraibu wa aina yoyote ile.
Uraibu ni msukumo ulevi au uhitaji uliopitiliza wa jambo au kitu hata kama kinakupa matokeo hasi.Kama kijana anaweza kutana na changamoto ya uraibu wa jambo fulani kama kamari, pombe, madawa ya kulevya n.k. Siri ya kujiepusha na uraibu wowote ule ni kujiepusha nao yaani kutojiingiza(kutojihusisha nao kabisa). Kijana anaweza shawishiwa na makundi mabaya ya vijana na kujikuta katika hali mbaya ya kushindwa kujitoa. Ikiwa utajiingiza ni vema kumwona mtaalamu wa saikolojia ili kupata msaada wa ushauri zaidi.

2. Kuepuka kukwepa majukumu katika ngazi ya familia mpaka taifa.
Majukumu ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Majukumu yanaweza kuja na changamoto mbalimbali ambazo zikawa ngumu kukabili. Lakini kama kijana yafaa zaidi kukabiliana na changamoto pasipokuona kama kuna mtu mwingine wa kuzitatua. Kijana anapokutana na changamoto na kuweza kuzipa utatuzi hupata ujasiri wa kukabili mambo mbalimbali katika jamii na kuyapa ufumbuzi.

3. Kuepuka migogoro ya aina yoyote katika jamii.
Ushirikiano hujengwa na maelewano baina ya watu katika jamii pasipo kuzingatia itikadi za kidini,kikabila na kichama. Kijana ni lazima aepuke makundi yanayochochea chuki dhidi ya mtu mwingine kwa kigezo cha itikadi. Migogoro hudhoofisha ushirikiano na kupelekea uvunjifu wa amani katika taifa.

4. Kuepuka kutumiwa vibaya na mtu, watu , kiongozi au kampuni n.k kujinufaisha kwa kuvunja sheria za nchi.
Kutokana na ushawishi wa vijana , unaweza pelekea kutumiwa vibaya kwa hongo au maelekezo ya kimasilahi. Mfano wakati wa uchaguzi viongozi huweza watumia vijana kuwashawishi watu wamchague kiongozi fulani. Au kutumiwa katika wizi na uovu mbalimbali. Kijana ni vema kuripoti katika vyombo vya sheria pindi jambo kama hilo linapotokea.

5. Kuepuka kujitenga katika masuala yanayohitaji ushirikiano katika jamii na taifa.
Kijana ashiriki kikamilifu kwenye majukumu mbalimbali kwenye jamii na taifa kwani ndiyo humkuza na kumwongezea uzoefu zaidi. Majukumu kama misiba,mikutano , mijadala n.k ni muhimu kushiriki kwani kuna wakati haikwepeki. Kushiriki kwake kunaweza kuwa kimawazo na utendaji. Kushirikiana na watu wengine humwondolea kijana msongo wa mawazo , hujengwa kujiamini na kujulikana na jamii.

HITIMISHO:
kijana ni mtu muhimu sana katika jamii. Jamii inayo wajibu wa kushirikiana na vijana katika kuwapa ushauri unaofaa, kuwaongoza katika njia iwapasayo kuiendea na kuamini kwamba wanaweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii na taifa kwa ujumla. Hakuna mwanadamu anayejua kila kitu hivyo kama kijana asiache kujifunza kila siku. Vijana wenye maarifa sahihi wanaweza kuleta mabadiliko na maendeleo katika taifa.
 
Upvote 5
Back
Top Bottom