Jamii inaamini kuwa kila Mtu anayeugua ugonjwa wa Kifua Kikuu huwa ana maambukizi ya VVU jambo ambalo limekuwa chanzo cha unyanyapaa kwa waathirika
Je, ni kweli kila Mtu mwenye kifua kikuu ana maambukizi ya VVU?
Je, ni kweli kila Mtu mwenye kifua kikuu ana maambukizi ya VVU?
- Tunachokijua
- Kifua kikuu (TB) ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya bakteria na huenezwa kwa njia ya hewa.
Mtu mwenye maambukizi ya kifua kikuu akikohoa, kupiga chafya au kutema mate ovyo husambaza vijidudu hivyo hewani, huweza kumwambukiza mtu mwingine.
Ugonjwa huu huambatana na dalili za Kukohoa kwa muda wa wiki 2 au zaidi, Maumivu ya kifua, Homa za usiku, Kutoka jasho kwa wingi usiku, Kupungua uzito, Kukohoa damu, Kukosa hamu ya kula na mwili kuwa dhaifu
Maambukizi ya VVU/UKIMWI kwa asili yake husababishwa na VIRUSI. Kwa kufuata mchanganuo huu, pamoja na kuzingatia njia za uambukizwaji, JamiiForums imebaini kuwa magonjwa haya hayasabishwi na vimelea vya aina moja, hivyo siyo kweli kuwa kila mtu mwenye kifua kikuu huwa na VVU/UKIMWI.
Uhusiano wa magonjwa haya huchangiwa na kupungua kwa kinga za mwili, hivyo kuyafanya yaende sambamba kwa baadhi ya watu. Kwa lugha ya kitaalam, magonjwa haya ni tegemezi, huishi kwa kutegemeana (TB & HIV Coinfection)
Watu wenye VVU/UKIMWI huwa na hatari kubwa ya kupatwa na kifua kikuu kwa kuwa kama ambavyo jina la ugonjwa huo linavyojinasibisha, huwa na upungufu wa kinga za mwili hivyo ni rahisi kwa miili yao kushambuliwa na bakteria wa kifua kikuu, pamoja na kuamsha ugonjwa kwa baadhi yao ambao huwa na kifua kikuu kilichopooza.
Ikiwa muathirika wa VVU/UKIMWI atatumia vizuri dawa zake, nafasi ya kupatwa na kifua kikuu hupungua sana, na anaweza asipate kabisa.
Pia, kwa mujibu wa tafiti, Matumizi ya dawa za kufubaza Virusi huwa na ufanizi wa zaidi ya 75% katika kukinga kutokea kwa Kifua Kikuu.
Ni muhimu kwa wagonjwa kutumia dozi zao vizuri ili kuepusha maambukizi ya magonjwa haya kwa pamoja kwani huongeza athari za ukubwa wa tatizo pamoja na kufupisha maisha kwa kiasi kukubwa.