MSANII wa muziki wa kizazi kipya, 20 Percent jina lake halisi Abbas Kinzasa juzi alifanikiwa kutwaa tuzo tano kati ya sita kwenye kinyang'anyiro cha tuzo za muziki Tanzania za Kili 2011.
Katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofana kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam, msanii huyo alinyakua tuzo tano huku akiwafunika nyota wengine kama Diamond na Ali Kiba ambao walikuwa wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo mwaka huu.
Msanii huyo ambaye mashabiki walikuwa wakimshangilia kila alipotajwa ingawa aliwakilishwa na prodyuza wake, Man Walter ukumbini hapo, alishinda tuzo ya msanii bora wa kiume, mtunzi bora wa nyimbo, mwimbaji bora wa kiume.
Wimbo wake wa Tamaa Mbaya ulitwaa tuzo ya wimbo bora wa mwaka na wimbo bora wa Afro Pop huku Banana Zorro akisema; Nilijua 20 angewafunika, nyimbo zake zinagusa maisha halisi ya Mtanzania wa kawaida na hata mwaka usishangae akaendelea kutawala.
Wasanii wengine waliofuatia kwa kujikusanyia tuzo mbili kila mmoja ni Linah, JCB na CPwaa. Linah alitwaa tuzo ya msanii mpya anayechipukia na mwimbaji bora wa kike wakati CPwaa na singo yake ya Action alinyakua tuzo ya wimbo bora wa Ragga na video bora ya mwaka.
Wimbo wa Ukisikia Paah wa JCB ambao amewashirikisha Fid Q, Chid Benz na Jaymoe uliwapa tuzo ya wimbo bora wa hip hop pamoja na wimbo bora wa kushirikishwa.
Wasanii wengine waliotwaa tuzo ni Lady Jaydee, ambaye aliibuka msanii bora wa kike, My Valentine wa Jahazi ndio wimbo bora wa Taarab, wimbo bora wa Kiswahili wa bendi ni Shika Ushikapo wa Mapacha Watatu huku Nikikupata wa Belle 9 ukitajwa wimbo bora wa R&B.
Ujio Mpya wa Hardmad akimshirikisha Enika ndio wimbo bora wa Reggae, rapa bora wa bendi kwa mwaka ni Khalid Chuma 'Chokoraa', msanii bora wa Hiphop ni Joh Makini huku Nitafanya ya Kidumu na Jaydee ikibuka nyimbo bora ya Afrika Mashariki na Lamar prodyuza bora.
Wimbo bora wa asili wa Tanzania ni Shangazi wa Mpoki aliofanya na Cassim wakati Nabembelezwa ya Barnaba ndio wimbo bora wa Zouk.
Mashabiki walionekana kufurahia maandalizi pamoja na programu ya shoo hiyo ingawa waliguna kwa nguvu alipotangazwa mshindi wa prodyuza bora wa mwaka ambaye ni Lamar na mshindi wa wimbo bora wa asili, Sylvery Mujuni au Mpoki, mchekeshaji wa Orijino Komedi.
Wengi wao waliwataja msanii Mrisho Mpoto au Mjomba na prodyuza Man Walter kuwa walistahili kwenye badala yao.
Msanii Diamond ambaye aliambulia patupu katika tuzo hizo licha ya kupewa nafasi kubwa alisema, Nimeridhika na mchuano ulikuwa mkali walioshinda walistahili.