incognitoTz
Senior Member
- Apr 19, 2019
- 133
- 172
Separation Ring ni kitu gani?
Roketi kwa kawaida huundwa kwa stages au vipande, ambavyo hutumika kwa wakati tofauti wa kuirusha kwenye obiti. Sehemu kubwa ya uzito wa roketi ni mafuta na injini, kwa kawaida asilimia 95 ya chombo chote ni sehemu hizo. Kwa kuwa roketi hutumia mafuta kwa haraka, ni lazima ibebe kiasi kikubwa cha mafuta na igawanywe katika vipande. Kila kipande kinapomaliza mafuta, hutenganishwa na sehemu iliyobaki ya roketi inayoendelea na safari ili kupunguza uzito. Hivyo si sehemu zote zinazohitajika kwa safari nzima. Sehemu hizi za roketi zinazojitenga zimeunganishwa na eneo linaloitwa "inter-stage section" linalokuwa Pete "Separation ring" ambayo hurahisisha mchakato wa kujitenganisha.
Hivi vipande visivyohitajika vinaenda wapi?
Roketi nyingi bado hazina mifumo ya kisasa ya kutumika tena (re-usable) kama ilivyo kwa roketi za kisasa za Falcon Heavy na Super Heavy booster za SpaceX. Hivyo hulazimika kuacha mabaki ya sehemu za roketi zilizotumika zikielea huko angani kwenye obiti ya chini na baadaye kuangukia duniani.
Kwa nini vipande hivi huachwa viangukie duniani wakati vinaweza kuleta madhara?
Sababu kuu za kuachwa kwa mabaki ya roketi baada ya kutumika ni gharama kubwa ya kubuni na kutengeneza roketi zinazoweza kutumika tena "re-usable rockets", pamoja na ugumu wa kiufundi katika kuhakikisha roketi inarudi salama bila ya kuleta madhara.
Kwa kuwa misheni nyingi za anga za juu hutumika mara moja tu, bado kuna kampuni zinazodhani uwekezaji katika teknolojia ya kutumika tena hauwezi kuwa na manufaa ya kibiashara.
Hali ya mabaki ya vyombo vya angani
Mabaki ya angani yanaenda kuwa tatizo kubwa sana katika siku zijazo zaidi ilivyo sasa. Sekta ya anga imekua sana katika miaka ya karibuni, na kuongezeka kwa mabaki ya vyombo vya angani kama vile setilaiti za zamani, booster za roketi, na mabaki mengineyo yanayotokana na shughuli za kibinadamu angani kumeibua changamoto kubwa ya kiusalama wa vyombo vya angani.
Kwa sasa inakadiriwa kuna zaidi ya mabaki milioni 170 yanayozunguka dunia. Mabaki haya yanasafiri kwa kasi ya wastani wa Mach 22, zaidi ya kilomita 28,000 kwa saa. Kwa kasi hii, hata kipande kidogo kinapogongana na kitu angani, kinaweza kusababisha uharibifu mkubwa sana. Kwa hivyo, kumekuwa na ulazima wa kutafuta njia ya kuondoa mabaki haya, na hapo ndipo tatizo linapoanza.
Zipo nadharia nyingi za kuyaondoa ila kwa uwezo wa kitekinolojia wa sasa, njia inayowezekana ni kuyashusha kutoka kwenye obiti na kuyaacha yaanguke duniani.
Hii hufanywa kwa kufunga vacuum thrusters kwenye setilaiti za kisasa ili zikiisha muda wake wazishushe na kuziangusha, na pia kwa kuhakikisha kuwa first-stage na second-stage booster haziendi mbali zaidi ili ziweze kurudi tena na kuangukia duniani.
Hatari ya njia hii ni kwamba setilaiti na booster nyingi hazina control surfaces wala atmospheric thrusters (mifumo au injini za kuwezesha kukiongoza chombo kikiwa ndani ya anga la dunia) ili kuwezesha usahihi katika kuchagua eneo la kukiangushia chombo hicho (controlled re-entry procedures).
Kwa hivyo, mabaki haya huwa yanajiangukia yenyewe sehemu yeyote kama yakishindikana kuungua na kuteketea wakati wa (re-entry) kuingia duniani. Hali inayofanya mabaki haya kuwa na madhara makubwa kwa mazingira, na hata kuhatarisha usalama watu pale yanapoangukia maeneo yenye shughuri za kibinadamu.