SoC03 Kilimo ni Uhai wa Tanzania, tusikikwepe

SoC03 Kilimo ni Uhai wa Tanzania, tusikikwepe

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Joined
Jul 30, 2022
Posts
321
Reaction score
691
Utangulizi
Kama nchi nyingine za Afrika, Tanzania ina rasilimali nyingi sana ambazo kama zingetumika vizuri, nchi ingeendelea na Maisha Bora kwa kila Mtanzania yangewezekana. Wakati Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete anaingia madarakani kama Raisi wa Tanzania mwaka 2005, Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, ilikuwa kauli mbiu yake katika kampeni zake, na hata baada ya kuingia madarakani.

Bila shaka Raisi Kikwete (ambaye alimaliza muda wake mwaka 2015) alitambua rasilimali tulizonazo (madini, gesi, mito, maziwa, bahari, vivutio vya kitalii, misitu, eneo kubwa na zuri la kilimo, na watu).

Kwa muda mrefu kumekuwa na mijadala na malalamiko kutoka kwa watu wa kada na marika mbalimbali wakihoji ni kwa nini rasilimali za madini na gesi hazipaishi Uchumi wetu wakati tunazo kwa muda mrefu! Ni ukweli kwamba madini na gesi vikitumika vizuri, vinaweza kuleta mapinduzi ya kiuchumi. Watu wengi wanatumia nguvu na akili nyingi kuwazia rasilimali hizi, huku wakisahau kwamba tumekalia ardhi kubwa yenye rutuba, ambapo ingetumika vizuri, yale Maisha Bora kwa Kila Mtanzania yangeonekana.

Uchimbaji wa Madini, Gesi na uchakataji wake unahitaji uwekezaji mkubwa, ambapo kutokana na hali yetu ya Uchumi, serikali inalazimika kutafuta wawekezaji kutoka nje ya nchi. Ni rasilimali inayohitaji muda mrefu (miaka 5 na kuendeleza) kabla ya kupata matunda (faida); vifaa vya gharama kubwa; utaalamu mkubwa (pengine haupatikani nchini), na fedha nyingi. Vyote hivi vinafanya matunda ya rasilimali hizi kuchelewa kuonekana, na pengine hata yakipatikana, sii makubwa kama inavyotarajiwa. Hii ndio sababu ya kwamba, Watanzania wengi hawawezi kujihusisha na kazi za madini au gesi asilia.

Kwa upande wa kilimo, hatulazimiki kutafuta mwekezaji kutoka nje ya nchi kuja kufanya shughuli za kilimo, na wala hatuhitaji mitambo mikubwa, na/au fedha nyingi kwa ajili hii. Tofauti na madini, kila Mtanzania anaweza kufanya kazi za kilimo, awe mjini au vijijini na akaweza kubadilisha Maisha yake kiuchumi.

Kilimo Kimesisitizwa toka Enzi za Ukoloni
Mbali na mashamba makubwa ya mazao ya kibiashara kama pamba, kahawa, chai, katani, na kadhalika (ambayo kwa kiasi kikubwa yalimilikiwa na wazungu), serikali ya ukoloni ililazimisha wananchi kulima mazao hayo ya biashara, pamoja na ya Chakula, kama mahindi, mtama, mihogo, maharage, na mengine.

Baada ya uhuru, na mpaka sasa, serikali awamu zote zimekuwa zikisisitiza na kuhamasisha wananchi kushirki katika kilimo cha mazao mbalimbali ya biashara na ya Chakula kwa lengo la kuwa na usalama wa Chakula, kuongeza kipato ya kaya na Uchumi wa nchi kwa ujumla.

Kaulimbiu Mbalimbali Kuhimiza Kilimo
Kumekuwa na kaulimbiu mbalimbali za kuhimiza uboreshaji wa kilimo nchini Tanzania. Katika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama cha TANU (“Tanganyika African Union”) mkoani Iringa Mei 1972, chama kilitoka na kaulimbiu ya SIASA NI KILIMO.

Katika kipindi cha utawala wa awamu ya kwanza chini ya Hayati Mwalimu Nyerere, kulikuwa na kauli mbiu nyingine, iliyojulikana kama KILIMO CHA KUFA NA KUPONA.

Kilelezo Na. 1: Wananchi Wakishiriki Kilimo Nchini Tanzania
Wakulima shambani 1.png

Chanzo: Google: Kilimo Tanzania

Na wakati wa utawala wa Raisi wa awamu ya nne (Mhe. Jakaya Mrsisho Kikwete), kulikuwa na kauli mbiu “KILIMO KWANZA” Ni kaulimbiu iliyokuwa maarufu sana, ingawa pamoja na kuiwekea mikakati na rasilimali nyingi, haikuleta matokeo makubwa katika kilimo chetu kama ilivyotarajiwa.

Kumekuwa na jitihada nyingi sana za serikali za kuinua kilimo, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa Watanzania wengi katika fani ya kilimo. Wizara ya kilimo, ndio inayoongoza kwa kuwa na wasomi wengi nchini.

Kilelezo Na. 2: Wananchi Wakishiriki Kilimo Nchini Tanzania
Wakulima shambani 2.png

Chanzo: Google: Kilimo Tanzania

Umuhimu wa Kilimo katika Uchumi wa Tanzania

Kwa mujibu wa tovuti kuu ya serikali, nchini Tanzania, Sekta ya Kilimo ni muhimili wa maendeleo ya Uchumi, kwani inachangia kiasi cha nusu ya pato la Taifa; robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi na chanzo cha chakula pamoja na utoaji wa fursa za ajira zaidi ya 75% ya Watanzania.

Kilimo kina mnyororo mkubwa wa thamani, ukianzia kwa mkulima shambani, wasafirishaji wa mazao, wauzaji wa zana na pembejeo za kilimo, wachakataji wa mazao, wauzaji wa mazao ghafi na yaliyochakatwa, nk.

Kilimo cha Tanzania kitakuwa na Tija, endapo Tutabadilisha Mtizamo
Kwa muda mrefu, serikali imekuwa ikihimiza kilimo cha kisasa bila kubadili mtizamo wa wakulima, kutoka kutegemea mvua, na kuhamia katika kilimo cha umwagiliaji. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuna mabadiliko ya tabianchi, hali inayosababisha uwepo wa mvua chache au mvua zisizotabirika. Ukweli huu unaungwa mkono na jarida la HakiArdhi (Machi 11, 2021), ambapo linasema, “kuna athari mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, kama ifuatavyo: uhaba wa maji kutokana na kukauka kwa vyanzo mbalimbali vya maji; majira ya msimu ya mvua kutotabirika maeneo mengi nchini; uharibifu wa miundombinu unaotokana na upepo mkali, mvua kubwa na inayosababisha mafuriko; na ongezeko la magonjwa”.

Kilimo cha umwagiliaji ninachosisitiza hapa ni kile cha kutumia makingamaji (“water sheds”), sambamba na mabwawa, mito. Makingamaji yanasaidia kuzuia maji kupotea, na hivyo kuongeza kiwango cha maji ardhini; maji haya yataongeza kina cha visima vitakavyotumika kumwagilia mashamba wakati wa kiangazi. Kilimo hiki kinaweza kufanywa na wakulima wakubwa na wadogo kwa gharama nafuu. Ni kilimo ambacho kimefanikiwa sana nchini India.

Mapendekezo
Serikali itume wataalamu pamoja na baadhi ya wakulima katika nchi za Asia, hasa India kwenda kujifunza kilimo rahisi cha umwagiliaji.

Serikali pamoja na wadau wengine, iwezeshe wakulima kuwa na vyama au vikundi imara ili viwasaidie kuwa na zana za kisasa za kilimo (kama trekta, mashine za kuvunia mazao na kadhalika) na masoko ya uhakika.

Sambamba na kilimo cha mazao, serikali iwawezeshe wakulima kuwa na mifugo mbalimbali ili wawe na usalama wa Chakula.

Kwa wakazi mijini, serikali na wadau wengine wawezeshe wakazi wake kufanya kilimo cha mjini (“Urban Farming”), ikiwa ni pamoja na ufugaji na kilimo cha bustani za mbogamboga.

Hitimisho
Tukibadilisha mtizamo, tunaweza kuwa na mapinduzi ya kijani nchini Tanzania.

Marejeo
Tovuti Kuu ya Serikali | Kilimo

HakiArdhi (Machi 11, 2021), Uchambuzi wa athari za mabadiliko ya tabianchi na haki za ardhi kwa wazalishaji wadogo

Ridham Kakar (Septemba 01, 2020), Jarida la “Down to Earth”, “Micro-irrigation: The way ahead for sustainable agriculture”.
 
Upvote 8
Huwa hainiingii akilini pale ninaposikia Marekani wakulima ni asilimia 5 tu ya wananchi wote, lakini walisha dunia; Tanzania, wakulima ni asilimia karibu 80, lakini hatujitoshelezi kwa chakula! Tunafeli wapi, miaka zaidi 60 ya uhuru, tayari tuna wasomi wabobezi wengi sana katika tasnia ya kilimo?
 
Wavivu hukimbilia kukodisha ili wao wabaki kuchukua kodi na kucheza bao
 
Back
Top Bottom