Hamza Nsiha
JF-Expert Member
- Jul 25, 2022
- 221
- 197
Kilio changu katika sekta ya Afya.
Ndugu zangu watanzania, leo hii ninawaandikia uzi huu nikiwa na lengo la kuonesha kilio changu katika sekta yetu muhimu ya Afya kuhusuiana na baadhi ya mambo ambayo yamekuwa kizungumkuti katika jamii yetu kwa ujumla. Sekta ya afya ni moja kati ya sekta nyeti kwa wananchi wote bila kujali itikadi zao za vyama, dini au makabila.
Utangulizi
Sekta yetu ya afya imeundwa na idara mbalimbali ambazo hushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha utolewaji bora wa huduma ya afya katika jamii. Katika kuhakikisha huduma bora kwa wananchi wizara ya afya imefanikiwa kuunganisha ngazi zote kuanzia ngazi ya zahanati-kituo cha afya-hospitali ya wilaya-hospitali ya mkoa-hospitali ya kanda/hospitali ya taifa.
Mpaka sasa kuna baadhi ya vitu ambavyo ni dhahiri kuwa sekta ya afya kupitia taasisi zake maalumu haijafanikiwa kuvitilia maanani/mkazo japokuwa vinaonekana kuathiri au kukwamisha huduma bora katika jamii.
Kabla sijaaanza kuelezea dhamira kuu ya uzi huu, ningependa tufahamu mifumo mbalimbali itumikayo kutoa huduma za afya katika jamii. Kulingana na shirika la afya duniani (WHO) imeelezwa kuwa kuna mifumo mikuu mitatu ambayo hutumika katika utoaji wa huduma ya afya kama ilivyoainishwa;
- Mfumo wa matibabu (medical model), huu ni mfumo ambao umejikita zaidi katika ugunduzi wa magonjwa kwa kutumia vipimo mbalimbali pamoja na kutibu magonjwa hayo. Katika mfumo huu, ujengwaji wa vituo vya afya, hospitali na zahanati ndio kipaumbele katika utoaji wa huduma ya afya.
- Mfumo afya ya jamii (social model), katika mfumo huu visababishi vyote vya magonjwa mbalimbali hupewa kipaumbele zaidi kama njia kuu ya utoaji wa huduma ya afya. Mfano uhamasishaji katika usafi wa mazingira.
- Mfumo wa salutojeniki (salutogenic model), katika mfumo huu inaelezwa kuwa endapo kutakuwa na upunguzaji wa msongo wa mawazo kwa watu basi ni dhahiri kuwa itaimarisha afya za watu katika jamii.
Je, Sekta yetu ya afya hutumia zaidi mfumo upi katika utoaji wa huduma kwa watu wake?
Ni ukweli usiopingika kuwa sekta yetu ya afya imewekeza jitihada zaidi katika mfumo wa kugundua ugonjwa na kutoa matibabu zaidi(medical mode) kuliko mifumo mingine iliyoainishwa mfano dhahiri ni kuwa serikali imejikita zaidi katika kutibu magonjwa ya akili kwa kutumia madawa zaidi huku ikisahau kuhusu mazingira kwa ujumla yaliyobeba visababishi vya matatizo hayo (social model).
Ni wakati sasa wa serikali pamoja na taasisi husika kuboresha mifumo yote kwa kiwango kimoja zaidi kwani mifumo yote hii huenda sambamba katika utoaji wa huduma bora kwa jamii. Hii itawezekana kupitia kujenga hospitali za kutosha, uelimishaji wa kina kwa wanajamii kwa ujumla juu ya kupambana na magonjwa pia kutengeneza maisha bora kwa kila mwananchi ili kuondoa misongo mbalimbali ya mawazo kwa wanajamii.
Ni kwanini matatizo ya afya ya akili yanazidi kushamiri huku ikionekana kuwepo kwa muitikio mdogo wa sekta ya afya katika kutafuta vyanzo vikuu vya matatizo hayo?
Hivi sasa kumekuwepo na ongezeko kubwa hususani la watu wenye tatizo la afya ya akili katika jamii zetu. Mfano mzuri huonekana kupitia idadi kubwa ya watu wenye matatizo ya akili (vichaa) katika jiji la Dar es Salaam na baadhi ya miji mkubwa kama Mbeya, Mwanza n.k. huku serikali kupitia sekta ya afya ikifumbia macho katika kung’amua vyanzo mbalimbali vya kwa kushamiri kwa matatizo hayo.
Ni lini sekta ya afya itatilia mkazo uchunguzi wa kina juu ya afya ya uzazi kwa watu wanaowasili hospitali kwa ajili ya kutibiwa magonjwa mengine?
Ni ukweli usiopingika kuwa hivi sasa, tatizo la afya ya uzazi limekuwa sugu hususani katika jamii huku watu wanaoenda kutibiwa magonjwa mengine wamekuwa wakitamani kuzungumzia kuhusiana na matatizo yao yahusuyo afya ya uzazi lakini kutokana na kanuni zinazotumika na watoa huduma wa afya ni ushughulikiaji pekee wa magonjwa yaliyowapeleka hospitali. Mfano watu wengi wenye matatizo ya moyo, kisukari, presha hutamani kugusiwa pia katika suala la afya ya uzazi kwani ni dhahiri kuwa magonjwa haya huathiri afya zao za uzazi.
Hali hii imepelekea kuwapo kwa huduma nyingi za mitaani kuhusu matibabu ya matatizo mbalimbali yahusuyo afya ya uzazi. Mfano matibabu ya nguvu za kiume yameonekana kupata wadau wengi kwa sababu kuwa ni dhahiri fika sekta ya afya imelisahau jambo hili hivyo waathirikq wameona ni bora kutafuta njia mbadala, jambo ambalo ni hatarishi kwani matibabu hayo ya mitaani hayana uhakika juu ya usalama wao.
Picha; Dawa ya asili maarufu kama "vumbi la Kongo" kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kufanya tendo la ndoa, iliyopigwa marufuku kutumika kutokana na kukosekana kwa tafiti za kutosha.(picha kutoka mtandaoni)
Hivyo ni kweli kuwa watu wengi wamekuwa wakitamani kuzungumzia matatizo yao mbalimbali kuhusiana na afya zao za uzazi kiujumla lakini kutokana na jamii ilivyojijengea pamoja na mfumo wetu wa utoaji wa huduma za afya, hautoi majawabu sahihi juu ya ufatiliaji wa masuala haya.
Mapendekezo;
- Ni wakati sahihi wa serikali kuboresha sekta ya afya kwa kuimairisha mifumo thabiti itakayowezesha kulinda afya za watu katika jamii kwa ujumla yenye kuhusisha mifumo yote mitatu kwa pamoja ili kuhakikisha huduma bora kwa wananchi wake juu ya masuala mbalimbali yahusuyo afya kwa ujumla.
- Pia serikali itazame upya mitaala inayotumika kufundishia mashuleni kwa kuongeza elimu juu ya afya ya uzazi katika ngazi zote za elimu, huku ikiongeza pia mtaala kwa vyuo vya afya juu ya uzingatiwaji wa makini wa afya ya uzazi kama sehemu nyeti katika maisha ya kila siku kwa wanajamii.
- Ni wakati pia wa serikali kupitia mamlaka zake husika kuimarisha utolewaji wa elimu kwa jamii nzima kwa kuhusisha makundi yote kwani waathirika wengi wa afya ya uzazi hutoka katika makundi mbalimbali kama vile vijana, watu wazima n ahata wazee bila kuwasahau watoto waliofikisha umri wa kuingia shule.
- Kuboresha tafiti mbalimbali kwa ajili ya kuchunguza magonjwa mbalimbali ambayo hapo awali hayakutiliwa mkazo. Hivyo ni jukumu la serikali kutoa hamasa pamoja na ufadhili kwa wataalamu katika kuboresha tafiti zao ambazo zitasaidia kutafuta majawabu mbalimbali juu ya matatizo hayo.
Ninapenda kuipongeza wizara ya afya kwa ujumla kwa jitihada zote zinazofanyika katika kuhakikisha afya bora kwa wananchi wake. Ni dhahiri kuwa ili sekta ya afya isonge mbele basi ni wazi kuwa inahitaji ushirikiano mzuri baina ya watu wake. Hivyo kilio changu hakina maana kuwa kinakosoa sekta hii bali kukumbusha juu ya baadhi ya mambo ambayo yamesahaulika katika kutiliwa mkazo.
Upvote
16