SoC03 Kingereza kiwe Lugha ya Kufundishia toka Awali hadi Chuo Kikuu kuondoa Utabaka

SoC03 Kingereza kiwe Lugha ya Kufundishia toka Awali hadi Chuo Kikuu kuondoa Utabaka

Stories of Change - 2023 Competition

madametheCHANGE

New Member
Joined
May 22, 2023
Posts
1
Reaction score
2
Kutumika kwa lugha ya Kiswahili katika shule za msingi za serikali ambazo zina idadi kubwa ya wanafunzi ukilinganisha na za sekta binafsi kumempa mzigo mwalimu wa sekondari kuhahakisha anaendeleza maarifa kwa lugha ngeni. Lugha ambayo ingeanza kutumika mapema iwezekanavyo tungemrahishia siyo tu mwalimu, bali pia mwanafunzi mlengwa ambaye wakati mwingine anaonekana hajui chochote katika somo husika, kumbe shida ni lugha.

Kwanini tuanzie elimu ya awali?
(i) Watoto wanapata lugha kwa wepesi, wanavutwa na lugha yoyote inayopatikana kwenye mazingira, wako tayari kujaribu na kuongea vyovyote pasipo kujali kama wanakosea. Ndio maana hakuna mtu kapigwa fimbo au kuvalishwa gunia ili ajue lugha ya kwanza au ya pili, umejikuta unajua kwasababu ipo umesikia toka utotoni na hukutumia nguvu kubwa kuifahamu.

(ii) Kuruhusu matumizi ya lugha mbili tofauti kwa ngazi ya elimu ile ile ni kutengeneza utabaka kati ya wenye nacho na wasio nacho. Kwamba nikitaka mwanangu asome kwa kiingereza lazima nilipie na yule asie na uwezo hana namna asome tuu kwa Kiswahili, kiingereza atakutanacho ukubwani.

(iii) Matumizi ya kiingereza hayaepukiki tukiamua kutumia Kiswahili elimu ya sekondari na kuendelea tutakuwa tumechelewa sana maana wachina na wengineo walianza zamani na wamewekeza vya kutosha. Sisi tukiamua kutumia Kiswahili chetu leo haitokuwa rahisi kwanza kupata wabobezi (maana wengi maarifa wamepata kwa kiingereza) wataalam wa mwanzo walisoma nje ya nchi. Bado gharama ya kutafsiri vitabu vya maarifa wachilia mbali upungufu wa wataalamu wa tafsri sahihi kimaarifa.

(iv) Tukiamua kutumia kiingereza msingi, waalimu wale wale waliopo wanaweza kubadilika ukizingatia serikali inaajiri waalimu wenye sifa na ufaulu mzuri kuliko sekta binafsi. Tuwatumie vizuri, wawajibike ipasavyo watupe msingi mzuri, maana msingi ukiwa imara itarahisisha hatua zinazofuata. Kiukweli wanafunzi kutoka shule binafsi za kiingereza hawahangahiki na masomo ya sekondari kama waliotoka shule za msingi za serikali.

(v) Vitabu vya maarifa vya kiada na ziada pamoja na miongozo vipo, kwani sekta binafsi msingi wanatumia. Hakutakuwa na gharama ya kutafsiri.

(vi) Kutumia lugha moja kutaleta msawazo kimaarifa na kuondoa ulazima wa kutafsiri mtihani katika lugha mbili sababu inayoweza kulegeza au kukaza ugumu wa mtihani husika katika lugha mojawapo.

(vii) Somo la Kiswahili litabaki kufundishwa kwa Kiswahili toka ngazi ya awali hadi chuo kikuu na litapaswa kuwa la lazima kwa msingi na sekondari kwasababu ni lugha yetu ya taifa. Inaunganisha watanzania na kutumika sehemu nyingi, bado wataalamu tunaowatengeneza tunatarajia wahudumie jamii ya Kiswahili. Mfano daktari pamoja na kusoma kwa kiingereza bado atahudumia wagonjwa watakao jieleza kwa Kiswahili.

(viii) Elimu ya msingi inahudumia sehemu kubwa ya wananchi, kwa kutumia kiingereza msingi, tutakuwa na asilimia kubwa ya watu wanaoweza kujieleza vizuri kwa kiingereza tofauti na hali ilivyo sasa na huku masoko ya kimataifa kiushindani, kujieleza kwa kiingereza ni msaada kuweza kuchangamana na kupanua fursa kimataifa.

(ix) Mitihani ya sasa imelenga kupima umahiri, kwa mwanafunzi ambae kiingereza ni tabu siyo rahisi kujibu. Kuliko kuendelea kumpa mitihani miwili kwenye karatasi moja yaani mtihani wa kiingereza na mtihani wenyewe. Ni vyema tukaanzia mwanzoni wanafunzi wakajifunza kwa amani na furaha.

(x) Moja ya sababu kubwa inayopelekea wazazi kuchagua kupeleka watoto shule binafsi ni lugha. Tukiweka usawa wa lugha tutampa mzazi uhuru wa kuchagua shule kwa vigezo vingine muhimu kulingana na uhitaji. Pia itatuwezesha kushindanisha wahitimu shule za binafsi na serikali katika ustadi na umahiri siyo tena uwezo wa kuongea kiingereza kizuri.
 
Upvote 3
Back
Top Bottom