SI KWELI Kipimo cha Mimba kikiwekwa Majimaji ya Nyanya kinasoma 'Positive'

SI KWELI Kipimo cha Mimba kikiwekwa Majimaji ya Nyanya kinasoma 'Positive'

Baada ya kuitathmini taarifa hii, tumebaini kuwa si ya kweli.
Nimekutana na hii stori mtaani kuwa ukiweka Maji ya Nyanya kwenye Kipimo cha Mimba kinatoa majibu yanayoonesha Ujauzito upo.

Kuna ukweli hapa na kwanini iwe Positive, Kwanini isisome negative au abnormal test results?

IMG_8254.jpeg
 
Tunachokijua
Ujauzito (Mimba) ni neno linalotumika kumaanisha kipindi cha ukuaji wa kijusi kwenye tumbo la uzazi (Uterus) la mwanamke.

Ujauzito huanza kuhesabiwa kuanzia siku ya kwanza ya tarehe ya hedhi ya mwisho na hudumu kwa wastani wa siku 280 au wiki 40.

Wakati huu, mwili wa mwanamke hutegeneza kiasi kikubwa cha homoni tofauti ili kukidhi haja ya mabadiliko ya kimwili na kihisia yanayotokea wakati huo.

Homoni hizi huwa na athari za moja kwa moja katika maisha ya kila siku ya mwanamke kwenye kipindi chote cha ujauzito pamoja na ukuaji mzuri wa mtoto kuanzia kiini tete, kijusi na hatimae kiumbe kilicho kamilika.

Baadhi ya homoni zinazozalishwa wakati huu ni hizi;
  1. Human chorionic gonadotropin hormone (hCG). Huzalishwa wakati wa ujauzito pekee, hupatikana kwenye mkojo na damu ya mwanamke mjamzito. Huwepo kwa wingi kwenye miezi 4 ya mwanzoni na kwa kiasi kikubwa ndio huhusika na hali ya kiungulia na kichefuchefu.
  2. Human placental lactogen (hPL). Huzalishwa na kondo la uzazi, huhusika na kutoa virutubisho kwa mtoto pamoja na kusisimua uzalishaji wa maziwa kwenye tezi za maziwa (matiti)
  3. Estrogen, husaidia kulinda ujauzito
  4. Progesterone, hunenepesha ukuta wa mji wa uzazi ili ujauzito uweze kuhifadhiwa vizuri.
Vipimo vya Ujauzito
Vipimo vya ujauzito kwa ujumla wake hulenga kugundua na kuhakiki uwepo wa ujauzito.

Vipimo hivi hutumia hutengenezwa kwa mfumo unaoruhusu kubaini uwepo wa homoni za human chorionic gonadotropin (HCG) ambazo hutengenezwa na mwili wakati wa ujauzito.

Homoni hizi huanza kuzalishwa kati ya siku 6-10 tangu kutungwa kwa ujauzito.

Damu au mkojo unaweza kutumika katika kujipima. Aidha, kipimo cha mkojo ndicho hutumiwa na watu wengi, hupatikana kirahisi kwenye maduka ya dawa na gharama yake huwa ni ndogo.

Madai ya nyanya kusoma positive kwenye kipimo cha ujauzito
Agosti 12, 2023, akaunti moja kwenye Mtandao wa X inayofahamika kwa jina la Sauti ya Afya iliweka chapisho linalodai kuwa kipimo cha ujauzito kianchotumia mkojo kikiwekwa kwenye maji ya nyanya husoma positive.

Andiko hilo lilisema;
Ukiweka kipimo cha mimba -UPT kwenye nyanya kinaonesha positive, UPT inapima HCG - hormone. Nyanya inauwezo wa kuongeza HCG hormone kwa binadamu kwa wale wenye low HCG-level ( HCG-foods). Kaka asikutumie picha ya kipimo, nenda naye hospital.

Ili ithibitike kuwa mwanamke ana ujauzito, kipimo cha ujauzito hupaswa kusoma positive (+ve). Ikitokea kimesoma negative (-ve) hutoa maana kuwa mwanamke hana ujauzito.

JamiiForums ilifuatilia uvumi huu ili kupata uthibitisho wake.

Katika hatua za kuhakikisha, kipimo cha ujauzito kinachotumia mkojo kilinunuliwa kwenye mojawapo ya maduka ya dawa jijini Dar es Salaam.

img_8241-jpeg.2715459

Kipimo cha ujauzito kinachotumia mkojo (UPT) ambacho JamiiForums ilitumia
Aidha, nyanya moja ilinunuliwa kutoka mojawapo ya masoko yanayopatikana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyia jaribio hilo.

img_8243-jpeg.2715461

Nyanya iliyotumika kwenye kuthibitisha madai husika
Baada ya kuandaa vifaa hivi, kipimo cha ujauzito kilitolewa kwenye kifungashio chake, nyanya ilitobolewa na maji yake yakawekwa sehemu safi. Kama kipimo kinavyoelekeza, ncha yake iliwekwa kwenye maji ya nyanya.

img_8244-jpeg.2715462

Kipimo cha ujauzito (UPT) baada ya kuchovya kwenye maji ya nyanya
Baada ya dakika 5, majibu ya kipimo hiki yalisomwa. Mstari mmoja ulionekana ukiashiria kuwa ni negative, yaani hakuna ujauzito. Aidha, hata baada ya kusubiri kwa dakika 10, kipimo hiki kiliendelea kusoma mstari mmoja pasipo kubadilika.

img_8246-jpeg.2715463

Kipimo kikionesha mstari mmoja (Negative, ishara ya kwamba hakuna ujauzito)
Majibu haya yanaenda kinyume na madai yaliyochapishwa na Sauti ya Afya kwenye mtandao wa X.

JamiiForums ilitafuta pia kipimo chenye majibu chanya kutoka kwa mwanamke mwenye ujauzito na kugundua uwepo wa tofauti kwenye muonekano wa mistari yake. Kipimo chenye kuonesha uwepo wa ujauzito hupaswa kuwa na mistari miwili.

img_8248-jpeg.2715464

Kipimo cha chini kikiwa na mistari miwili (Positive) kumaanisha uwepo wa ujauzito.
JamiiForums imebaini kuwa picha iliyowekwa na Sauti ya Afya ilichukuliwa kutoka kwenye video iliyopo kwenye mtandao wa TikTok kwenye akaunti ya Davevo x Dannielo.

Video hiyo inafafanua madai ya maji ya nyanya kutoa majibu chanya (Positive) kwenye kipimo cha ujauzito.

Hata hivyo, jaribio lililofanyika kwenye video hiyo linatoa majibu hasi (negative) kama ambayo JamiiForums imeyapata baada ya kufanya utafiti wake.

Huu ni uthibitisho mwingine kuwa madai yanayotajwa na Sauti ya Afya kuhusu maji ya nyanya kutoa majibu chanya (Positive) kwenye kipimo cha ujauzito kuwa si kweli.
Back
Top Bottom