Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Kipini: Kijiji cha pwani ya Kenya kinachotoweka baharini
Maelezo ya picha,Wageni wakati mmoja walifurahia mandhari ya kupendeza kutoka kwa roshani ya hoteli ya Tana Lodge
Wakati Roberto Macri alipojenga hoteli yake ya kifahari katika kijiji cha Kipini, pwani ya Kenya ilikuwa takribani mita 100 (330ft) kutoka kwenye Bahari ya Hindi.
Kwa karibu miongo miwili biashara yake ilistawi watalii walipowasili kwa wingi ili kufurahia ufuo wa kuvutia pamoja na hali ya hewa nzuri.
Hoteli ya Tana Lodge, iliyojengwa juu ya matuta ya mchanga, ilitoa mandhari ya kuvutia ya lakini sehemu ya jengo lake sasa imemezwa na bahari - moja baada ya nyingine.
"Bahari ilibadilika polepole na kuanza kuivamia hoteli. Jumba la mwisho lilimezwa na bahari mnamo 2019, na hivyo kuashiria mwisho wa hoteli yangu tukufu," mfanyabiashara wa Italia Bw Macri aliambia BBC.
Sasa wakazi wengine wa kijiji cha Kipini, ambao nyumba zao ziko mbali zaidi na hoteli hiyo, wanakabiliwa na hatma hiyo hiyo.
Kipini - iliyojengwa kwenye mkondo mrefu zaidi ya maji nchini Kenya, Mto Tana, ambao unatiririka katika Bahari ya Hindi - ni miongoni mwa vijiji kadhaa vya pwani ambavyo vinatoweka polepole.
"Bahari inasonga mbele kila siku na nyumba zetu zinazidi kuwa dhaifu. Tunaogopa na kufadhaika lakini hatuna la kufanya," Saida Idris, kiongozi wa kijamii, aliiambia BBC.
Alisema watu kadhaa wamefariki dunia na wengine kadhaa hawajulikani walipo baada ya kusombwa na kupanda kwa kina cha bahari, pamoja na upepo mkali na mawimbi makubwa hasa nyakati za usiku.
Kupungua kwa misitu ya mikoko kando ya ufuo - njia kuu ya ulinzi wa pwani dhidi ya mmomonyoko wa ardhi - ndio chanzo cha tatizo hilo.
Misitu ya mikoko imejaa miti na vichaka vinavyostahimili chumvi ambayo huzuia maji ya bahari kuingia kwenye mashamba kwa kuimarisha udongo ambao ungeweza kusombwa na maji.
Chanzo cha kutoweka mikoko hiyo inaonekana kuwa mchanganyiko wa ukataji miti unaofanywa na wenyeji kutaka mbao ngumu zinazotamaniwa – na kupanda kwa maji ya bahari kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, ambayo wanasayansi wanahisi ndiyo sababu kuu.
"Ufukwe wa Kipini unakabiliwa sana na athari za upepo mkali unaoimarisha mawimbi ya bahari," George Odera, mwanasayansi wa Fauna and Flora, kikundi cha uhifadhi wa mazingira, alielezea.
Maelezo ya picha,Kipini iko mahali ambapo Mto Tana unakutana na Bahari ya Hindi
Kipini, pamoja na mitende ya kuvutia na harufu ya viungo na dagaa wa kukaanga, inaibua kile ambacho kila Mkenya anaafiki kuwa taswira ya maisha matulivu ya pwani
Lakini kijiji hiki kinakabiliwa na tishio la kuzama kwani viwango vya maji ya bahari vinaendelea kuongezeka.
Kulingana na Omar Halki, msimamizi wa eneo hilo, karibu kilomita 10 (maili 6.2) ya eneo iliyokuwa nchi kavu imemezwa na bahari katika miaka 10 iliyopita.
"Ni suala la muda kabla ya eneo lote kusombwa na maji," aliiambia BBC.
Kipini ina wakazi 4,000 ambao waliambia BBC kwamba hawawezi tena kuchimba au kujenga misingi imara ya nyumba zao kwa sababu ya kuongezeka kwa kina cha bahari.
Baadhi ya wakazi wa zamani wa Kipini wanakadiria kuwa zaidi ya watu 1,000 wamehamia vijiji vingine katika muongo mmoja uliopita.
Visima vingi vilivyokuwa vikiwasaidia wenyeji kwa maji safi sasa vimegeuka kuwa na chumvi na hivyo kuwalazimu kutafuta vyanzo mbadala vya maji ya kunywa.
Kuongezeka kwa chumvi katika maji ya chini ya ardhi pia kumeathiri sana kilimo.
Kaa na kamba, ambao pia wamekuwa chanzo cha riziki kwa wenyeji, sasa wanaogopa kwani mazalia yao yako ndani ya vinamasi vya mikoko.
Maji yanayoinuka yameathiri karibu nyanja zote za maisha, hata jinsi watu wanavyozikwa.
"Makaburi hayana kina kwa sababu tukichimba futi sita zinazopendekezwa, wafu watazikwa kwenye maji," mkazi mmoja aliiambia BBC.
Kipini iko ndani - Kuanzia ukame na uhaba wa maji katika baadhi ya maeneo hadi mafuriko katika maeneo mengine.
Ni mfano wa kwanza wa kaunti ambayo kijiji chake kinakabiliwa na tisho la kuangamia kutokana na kupanda kwa viwango vya maji ya bahari.
Lakini baadhi ya wenyeji wanasema jiografia ya pwani daima imekuwa ikibadilika - wakionyesha jinsi jamii ndogo ya wavuvi wa Ghuba ya Ungwana ilivyongamizwa miaka iliyopita.
Wengine wanasema Mto Tana unaweza kubadilisha mkondo wake.
"Mababu zetu walituonyesha mahali njia ya awali ya maji ilipita," mkazi Rishadi Badi aliambia BBC, akiongeza kwamba aliambiwa mto huo ulikuwa ukipitia Kipini mzamani za kale.
Lakini Bw Odera, ambaye anachunguza maafa yanayoikabili Kipini, anasema mabadiliko ya hali ya anga ndio yamechangia moja kwa moja kile kinachoshuhudiwa katika kijiji hicho.
“Kinachotokea Kipini si historia, ni tukio la hivi karibuni na ukweli mchungu ni kwamba, hali haijaimarika,” alisema.
Mamlaka za mitaa zinataka kujenga ukuta wa bahari kando ya ufuo wa kilomita 72 (maili 45) ili kuokoa kijiji dhidi ya maji ya bahari.
Ingawa mamlaka inakubali hali ni mbaya, mradi wa ujenzo wa ukuta hao bado haujaanza kwa sababu ya ukosefu wa fedha, anasema Mwanajuma Hiribae, afisa mkuu wa ardhi katika kaunti hiyo.
"Uvamizi wa maji ya bahari ni tatizo kubwa zaidi linaloathiri takribani vijiji vingine 15 na serikali ya kaunti pekee haiwezi kutatua tatizo hilo," aliambia BBC.
Ingawa alisema Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa na UN Habitat wameelezea kuunga mkono mradi wa ukuta.
Kuta kama hizo zimejengwa katika maeneo ya kihistoria kama vile Fort Jesus huko Mombasa na Vasco Da Gama Pillar huko Malindi baada ya ongezeko viwango vya maji ya bahari kutishia vivutio hivi vya watalii.
Lakini wataalam wa hali ya hewa wanasema kujenga ukuta Kipini ni "suluhisho la kimfumo", na kunahitajika kuwa na mipango ya uhifadhi, kama vile kurejesha misitu ya mikoko.
"Bahari si kitu ambacho serikali itaamka siku moja na kudhibiti viwango vya maji yake. Tunafaa kusaidia jamii zetukubadili mtazamo wao wa maisha na kustahimili mabadiliko haya ya hali ya hewa," Bw Odera alisema.
Wenyeji wanasema kuwa wanajihisi kama wageni wa muda katika nyumba zao kila wanatembea ufuoni kujionea jinsi bahari inavyonyemelea makazi yao.
"Tusipopata usaidizi wa dharura ndani ya miaka mitatu, eneo lote la Kipini litamezwa na bahari," Bw Halki alisema.
Kwa Bw Macri, hali imekuwa mbaya na sasa amehamia Malindi mji mwingine wa pwani, ambao ni kilomita 170 (maili 100) kutoka Kipini.
"Eneo hilo lilikuwa kama tunu - kijiji tulivu chenye matuta mazuri ya mchanga yaliyozungukwa na minazi na majengo ya kihistoria karibu na ufuo," alisema.
Kilichosalia katika uwekezaji wake wa dola 460,000 ni kile kilichokuwa nyumba ya meneja, iliyokuwa chini ya mita 50 kutoka baharini ambayo pia inasubiri hatima yake.
Kati ya ekari 10 ambazo zilitumika kwa ujenzi wa hoteli, nne zimezama kabisa.
Bw Macri anashikilia ekari zake sita zilizosalia akitumai kurejea na kuwekeza tena pindi bahari itakapozuiwa kuivamia nchi kavu.
Mkurugenzi Mkuu wake wa zamani, Joseph Gachango, naye hakusazwa.
"Ilinivunja moyo sana kuona hoteli ambayo ilikuwa ikivutia wageni kutoka mataifa ya mbali kama Italia ikiangamizwa na wafanyakazi wake 50 wakipoteza kazi zao," alisema. chanzo.BBC