DALALI MKUU
JF-Expert Member
- May 7, 2022
- 2,011
- 4,705
Jenipher Mgendi N mwimbaji wa Nyimbo za injili Nchini Tanzania amewahi Kutamba an Nyimbo kama Vile Chekundu, Yesu Nibebe;Nipo StudioBaba n.k
Leo anatusimulia Kisa chake kilichotokea Miaka zaidi ya Thelathini iliyopita wakati Huo akiwa Jeshini Huko kabuku Mkoani Tanga. soma mwenyewe
Jeshi la Kujenga Taifa
Kabuku, Tanga, 1993.
--------------------------------------
AFANDE: (Ana cheo cha Luteni, Anaita kwa sauti ya juu) "Kuruta! Wee Kuruta!" (Kuruta ni Askari asiye na cheo...)
WOTE: (Tunashtuka na kuulizana kwa sauti za kunong'ona "tumekosa nini? Au tumetembea kizembe? Au tuliposimama kupiga picha haparuhusiwi? Au kofia zimekaa vibaya? Tumekosa nini?" Tunahofia kugeuka kwani jeshini hakuna jema; lolote laweza kukupata bila kutarajia.
Ni siku tatu tu zilikuwa zimepita tangu kombania yetu ipewe adhabu baada ya mmoja wetu wakati wa mchaka mchaka kuanzisha wimbo uliokuwa unatumiwa kwenye tangazo la dawa maarufu ya wakati huo, ilikuwa inaitwa Dawanol (sijui kama bado ipo).
Basi nasi bila ajizi tukaitikia na kuimba kwa nguvu wimbo huo wenye maneno yanayosema "Kiuno changu chaniuma maumivu tele, dawa ya maumivu dawa yenye nguvu,
dawa ni Dawanol..."
Wakati bado tumesimama afande akaita kwa mara ya tatu na kwa ukali zaidi...
AFANDE: "Kurutaaaa!"
Jeshini mkiwa zaidi ya mmoja anayekuwa mkono wa kulia ndiye anawajibika kusalimia au kujibu pale mnapokutana na afande. Kwa kuwa nilikuwa kulia nikajua tayari nisipoitika yatanikuta makubwa.
MIMI: (Nikiwaambia wenzangu) "Mmh ngoja niende tangulieni nakuja"
Niligeuka na kumfuata afande....
MIMI: "Jambo Afande!" (Salamu ya jeshini ni Jambo, hakuna mambo ya shikamoo...)
AFANDE: (Akiitika kwa ukali) "Jambo! Mbona naita mnajifanya hamsikii?"
MIMI : (Kimya)
AFANDE "Wajeuri sio?"
MIMI "Hapana afande"
AFANDE: "Unaitwa nani?"
MIMI: "Jennifer"
AFANDE: (Anapekua mifuko ya suruali na shati kama anatafuta kitu, kisha anachomoa pakti kutoka mfuko wa suruali na kuchomoa sigara moja)
"Haya, kaniwashie hii sigara"
MIMI (Nimepigwa na butwaa)
AFANDE: (Kwa ukali) "Kuruta umenisikia? Nimesema kaniwashie hii sigara"
MIMI: (Kimya)
AFANDE (Akinisogelea karibu na kunitikisa begani) "Hivi wewe ni kiziwi?"
MIMI: (Nimepatwa na mchanganyiko wa woga, hasira na ujasiri) "Hapana Afande mimi nimeokoka sishiki sigara..."
AFANDE:
"Unasemaje wewe?"
MIMI: "Afande nimeokoka sishiki sigara"
AFANDE: (Anaangua kicheko kilichochanganyika kebehi na hasira)
"Kwa hiyo unakaidi amri halali? Ngoja nikufundishe utii. Yaani kuruta unakaidi amri ya jeshi? Jeshi unatii amri kwanza maswali baadae.
(Kwa ukali) Haya chuchumaa upesi" (Anatishia kunipiga mtama)
MIMI: (Haraka nachuchumaa. Najua tayari yameshanikuta makubwa. Nawaza sijui nitapewa adhabu gani lakini nawaza sana sana nitapewa adhabu ya kuingia lindoni mfululizo maana ndio adhabu iliyokuwa inatolewa mara kwa mara.
Utasikia haya adhabu yako "Guard siku tatu". Kengele ya chakula inapigwa. Najua tayari nashinda na njaa maana chakula ni dakika chache. Halafu ilikuwa siku ya wali na wali unaliwa mara mbili tu kwa juma.)
AFANDE: "Piga magoti na mikono weka kichwani..."
Anaangalia huku na huku kama anayetafuta kitu na kwa mbali anapita Koplo Boko (Jina limebadilishwa kwa sababu za kiusalama )
Anamuita "Koplooooo"
Itaendelea kesho....
HAYA SASA ENDELEA
SEHEMU YA 2
KOPLO BOKO:
(Anakuja mbio na kupiga saluti akimsalimu Afande) "Jambo Afande!"
AFANDE: "Jambo!" (Ananigeukia na kwa sekunde kadhaa ananitazama kwa macho makali kisha anamgeukia Koplo Boko na kumpa maagizo) "Lock-up na Extra Drills" (Yaani nipelekwe mahabusu na kupigwa kwata la adhabu.
Hizo 'Extra Drills' unateswa, unarushwa vichura, unapiga pushapu , unaambiwa ugalegale kwenye mavumbi au matope, unakimbizwa, unasukumwa, unatembelea magoti, unashika masikio, (adhabu ya kuchuchumaa halafu unapitisha mikono chini ya miguu na kuyashika masikio yako....yaani kwa kifupi unafanyishwa mazoezi ya mateso).
KOPLO BOKO:
(Huku akipiga saluti ishara ya kukubali maelekezo)
Afande (Luteni) anaondoka na kuingia ofisini).
KOPLO BOKO Ananigeukia na kunitazama kwa "sura ya kazi"
MIMI
(Matumaini yangu ya kusamehewa yanafifia ghafla maana nilishafurahi moyoni nilipoona Afande ameingia ofisini, Nikapata tumaini kuwa huyu Koplo aliyekabidhiwa jukumu la kunipeleka mahabusu atanionea huruma. Lakini kwa sura hii anayonitazama nayo naanza kukata tamaa).
KOPLO BOKO
( Anaongea kwa amri na kwa ukali kuliko hata Afande Luteni)
"Simama juu!" Ananiamrisha.
MIMI
Nashukuru moyoni kuambiwa nisimame juu maana magoti yameshaanza kuuma na hapo nilipopigishwa magoti pana mawe madogo madogo.
KOPLO BOKO
"Usawa wa Main Gate, mbele kimbia...!"
(Huko Main Gate ndio lango kuu la kuingilia kambini na ndipo ilipo mahabusu. Yaani hapo ulinzi ni mkali sana masaa 24 na kila anayeingia lazima ajitambulishe na kukaguliwa.
Nakumbuka mimi na wenzangu tuliwahi kupangwa lindo la 'Main Gate' na kwa kweli tulikuwa hatupendi kupangiwa hilo lindo sababu unatakiwa uwe makini sana ukipangwa hapo.
Kila anayekuja lazima umsimamishe na kumwamuru ajitambulishe. Kuna siku Afande mkubwa pale kikosini alifika hapo main gate na gari. Waliokuwa lindoni walikuwa makuruta.
Walipomwona kwa kuwa wanamfahamu sana hawakumsimamisha wala kumwamuru ajitambulishe kama inavyopasa.
Badala yake wakamfungulia geti akaingia ndani bila kumtaka ajitambulishe yeye nani na anafuata nini hapo kambini. Kesho yake walipewa adhabu kwa kukiuka utaratibu..."Je kama afande ana pacha wake ambaye ni jambazi amekuja kushambulia kambi nyie mnamfungulia bila kumhoji kwa nini?" Walikiona cha moto).
MIMI: (Naanza kukimbia kuelekea Main Gate huku nikiwaza jinsi gani nitamwingia Koplo Boko anisamehe.
Kukimbia ni jambo ambalo nimeshaanza kulizoea . Kuruta haruhusiwi kabisa kutembea toka siku ya kwanza akisharipoti. Yaani popote unapoenda marufuku kutembea kwa hiyo haikunipa shida.
Pia mchakamchaka wa kila siku asubuhi ulifanya nisione shida yoyote kukimbia kwani tulikuwa tunakimbia mchakamchaka kila asubuhi na kuna wakati tunakimbia mwendo mrefu sana kwenye pori ambalo mkianza kupita hilo pori afande anatangaza "hili pori lina simba...sasa wewe legalega ubaki nyuma..." (sijui kweli au ilikuwa kututisha maselule (wavivu) tuongeze mwendo?
Njaa inazidi kuniuma na kutunisha misuli yake tumboni.mwangu. Kwa mbali nawaona wenzangu wakiwa wamebeba Mestin (Mess Tin, yaani vyombo vya kulia chakula jeshini kama sahani au bakuli la bati lenye umbo la mstatili au mraba na lina mshikio. Roho inaniuma nikiwaza ubwabwa unanipita....
Ghafla namsikia Koplo Boko akiniamrisha kwa ukali...
KOPLO BOKO:
"Hey! Simama...!
Chini...!"
(Akimaanisha nisimame na nichuchumae)
MIMI: (Natii amri.)
KOPLO BOKO: Mbele !
(Yaani niendelee kwenda mbele huku nimechuchumaa) Naenda hatua chache kisha natulia. Naona sasa ni muda muafaka wa kufikisha ombi langu la msamaha kwa Koplo Boko...)
MIMI: (Nikiongea kwa unyenyekevu)
"Afande naomba unisamehe..."
KOPLO BOKO: (Akiongea kwa msisitizo huku akipigapiga makofi ya kusisitiza" "Mbele....Mbele.... Mbele !unanichelewesha"
MIMI: (Najua hawezi kukubali mara moja najipa moyo kuwa hadi mara tatu atakuwa amekubali )
"Afande Naomba basi nikimbie..."
KOPLO BOKO
"Unaleta utani eeh?"
MIMI: "Hapana afande miguu inaniuma sana..."
KOPLO BOKO
"Miguu kuuma kuna ajabu gani?
Hakuna kisichouma... mara ya kwanza lazima iume jikaze!
(Kauli kama hizi hazikuwa ngeni masikioni maana hawa maafande walikuwa ni watu wanaopenda sana utani na vichekesho sambamba na kutumia lugha ngumu au za mafumbo na mizaha lakini sasa ole wako ucheke.
Nakumbuka kuna siku tulikuwa kwenye mafunzo ya jinsi ya kushika silaha (bunduki). Sasa tukawa tunaelekezwa jinsi ya kuishika na mwenzetu mmoja akakosea na ile bunduki akaishika kwa namna ambayo ilikuwa kama ameisogeza karibu naye na Ile sehemu ya kuwekea silaha ameielekeza kwake. Sasa tukiwa katika utulivu, baada ya amri kutoka ya kukaa katika pozi la kumshambulia adui...
Afande akaja kwenye mstari wetu kukagua kama wote tumeshika silaha sawa sawa.
Alipomwona huyo mwenzetu aliyeshika silaha kinyume akaanza kumwita afande mwenzake aliyekuwa upande wa pili...
"Aisee njoo huku ujionee maajabu... kuna mtu huku ameikumbatia silaha badala ya kuelekeza kwa adui...inaonekana huyu amezoea sana kukumbatia wanaume...."
Tulijikuta tumeangusha kicheko na tulipocheka tu tukageuziwa kibao kwanini tunacheka na kujikuta tunapewa adhabu.
MIMI:
Naendelea kutembea kwa kukuchumaa na kutambaa. Naiona Main Gate kwa mbele maana si mbali sana ila tatizo ni namna ya kufika hapo.
Kusema kweli hii namna ya kutembea umechuchumaa inaumiza sana. Nilikuwa sijawahi kuifanya peke yangu mara zote tunakuwa kombania nzima kwa hiyo mara nyingine unajisapoti kwa kumshika wa mbele yako au unatambaa kidogo .
Jua nalo linawaka kwa hasira kali kama ujuavyo jua la Tanga. Nasikia kuchoka.
Tumekaribia sana Main Gate.
Kulala mahabusu hakunipi sana mawazo kama hiyo adhabu ya Extra Drills.
"Ngoja nijaribu mara nyingine kuomba msamaha" najisemea moyoni.
MIMI: "Afande naomba unisamehe, ipo siku nawe utasamehewa......"
KOPLO BOKO
"Usiniletee dini hapa!"
(Mara anatokea askari mwingine nadhani ni rafiki yake. Wanasimama kusalimiana kwa kama dakika moja )
MIMI
(Natumia fursa ya wao kusalimiana kusimama.
Nadhamiria kumbembeleza hadi anisamehe. "Sitaweza extra drills bora wangenipa kung'oa kisiki jamani...... au wangenipa adhabu ya Lindo" nawaza.
"Au nitoroke?
Hivi natesekea nini? Wazo la kutoroka jeshi linapata nafasi kubwa akilini mwangu. Ninachotesekea ni nini hasa? Potelea mbali na hiyo ajira yao.... (Tulipomaliza tu Chuo cha Ualimu tulipangiwa ajira na ilikuwa hakuna kwenda kuripoti kazini hadi kwanza upite Jeshi kwa tuliotoka vyuoni).
Mawazo yangu yanakatizwa na sauti kali ya kushtua ya Koplo Boko
"Heyyyyy !!
"Kuruta nani kakwambia usimame?"
MIMI:
(Wazo langu ni moja tu kuomba msamaha.
Namtazama Koplo kwa macho malegevu ya huruma na kwa sauti ya upole sana huku nikiongea kwa unyenyeke)
"Nisamehe afande...Hivi afande kweli imeshindikana kabisa kunisamehe?"
(Nalazimisha kufinya macho na kuvuta hisia za huzuni ili machozi yatoke. Machozi nayo yananisaliti katika kipindi hiki ambapo ninayahitaji sana..)
KOPLO BOKO (Anatafakari kwa sekunde chache kisha anaongea kwa sauti ya upole kama anayenihurumia)
"Hivi kwani umefanya kosa gani?"
MIMI
(Nikiongea kwa kutia huruma zaidi ) "Eti nimekataa kuwasha sigara..."
KOPLO BOKO : "Sasa kwanini umekataa na wewe si ungewasha tu?"
MIMI: "Mimi nimeokoka afande siwezi kumuwashia mtu sigara...."
KOPLO BOKO:
Upuuzi mtupu. Watu walikuja hapa wakijifanya walokole miezi mitatu tu tunawaona wanasimamisha minazi (kusimamisha minazi ni kusimama gizani au maeneo ya kificho ukiwa na mwanamke au mwanaume (jinsia tofauti)
"Halafu wewe huo ulokole wako ni wa aina gani? Hebu nikueleweshe kwanza....
Sikiliza! Hapa ni jeshini, jeshi halina dhambi ndio maana imeandikwa usiue lakini sisi adui akivamia hapa tunamuua na hatupati dhambi yoyote kwa Mungu. Imeandikwa usizini lakini kwa maslahi ya taifa unaweza kutumwa kuzini na adui ili kufanya upelelezi na kuleta taarifa zake...Kwenye swala la ulinzi wa nchi hakuna dhambi. Umeelewa?
MIMI: (Nimetoa macho sijui kama nimeelewa au la)
KOPLO BOKO
" Kwa hiyo ina maana wewe hapa wakiingia adui utaanza kupiga magoti kusali badala ya kuwafyatulia risasi, si ndio?"
MIMI: (Bado natafakari maneno yake)
KOPLO BOKO: "Jeshini kila kitu ni halali kwa maslahi ya Taifa...Umeelewa?"
MIMI: (Nashusha pumzi ndefu) "Ninachoomba Afande ni msamaha"
KOPLO
(Anatafakari kwa sekunde chache kisha Anaongea kwa sauti ya (chini zaidi kama ananong'ona i) "Sawa mimi nimekubali kukusamehe, ila sasa..... ila sasa .....vipi itakuwaje sasa?"
MIMI: (Kengele ya hatari inalia kichwani kwangu ila najifanya kama sijamwelewa anamaanisha nini) "Itakuwaje kuhusu nini afande sijakuelewa?
KOPLO BOKO
"Acha utoto usichoelewa nini?"
Itaendelea
HAYA SASA ENDELEA
Tumalizie Sehemu ya 3 na ya Mwisho
---------------------------------------------------------------
MIMI: "Afande ukinisamehe sitakuwa na cha kukupa wala kukulipa ila Mungu atakubariki sana...."
KOPLO BOKO (Akisonya na kubana pua kuigiza majibu yangu)
"Ukinisamehe Mungu atakubariki!!" Mpuuzi kweli wewe...! Yaani mimi nikusamehe niwekwe lock-up, nilimwe 'guard' za kutosha halafu eti Mungu atanibakiri! (Anasonya tena).
Tumefika Main Gate.
"Haya nenda ukanyung'unywe...".(Kunyung'unywa ni msemo tulioukuta jeshini ikimaanisha kuteswa)
Nadhamiria moyoni mwangu kuwa kuanzia sasa sitajibu tena kitu na wala sitaomba msamaha wala huruma kwa yoyote. Nitatumikia adhabu yoyote nitakayopewa.
Tunapoingia tunawakuta MP wawili. Hawa ni mapolisi wa jeshi (Military Police) ambao kama sikosei mojawapo ya majukumu yao ni kuwaadabisha wanajeshi wanaofanya makosa.
Koplo Boko amerudia tena ile sura ya kazi aliyoivaa mwanzoni na moja kwa moja ananiongoza kwenye chumba cha MP na kunikabidhi kwao. Kisha anaondoka kwa mwendo wa ushindi huku akinitupia jicho kama anayeniambia "haya baki ukione cha moto si unajifanya mjuaji?"
MP: "Wewe kwanini unakaidi amri ya afande? Haya chini!"
Ni mtu wa miraba minne halafu amekwenda hewani. Buti alilovaa tu nahisi lina kilo 5 akikupiga nalo lazima uvunjike mguu.
Nachuchumaa upesi.
"Twende kichura
Hey hay hey hay fungua hatua hizo...."
Kwa ufupi nanyungunywa kwa dakika chache lakini kisawasawa na baada ya hapo MP ananipeleka mahabusu.
Anaponifungulia mlango wa mahabusu ananiambia
"Haya ingia ufanye maombi".
Sishtuki hizi lugha nimeshaanza kuzizoea ila hofu yangu ni hizo extra drills. Sijibu kitu bali naingia ndani na tofauti na matarajio yangu kuwa nitakuwa peke yangu, nakutana na watu wanne, yaani wanaume wawili wakiwa wamelala huku mmoja ameelekea ukutani na mwingine amelalia mgongo anatazama dari.
Mavazi yao yamejaa matope yaliyokauka na wanaonekana wamechoka sana. Kijana mwingine wa kiume alikuwa ameketi sakafuni huku akiwa kashika tama na amepasuka mdomoni (Nilidhani amepasuka mdomo kwa kipigo lakini baadae nilikuja kujua kuwa amepasuka baada ya kupigwa na radi akiwa mule mule mahabusu, radi ilipenya dirishani ikampasua mdomo).
Pia alikuwemo mdada amejiinamia na sura ameifunika haionekani vizuri. Nafurahi angalau tupo wadada wawili...Kifo cha wengi harusi.
"Habari zenu?"
Hawajibu isipokuwa mkaka aliyeshika tama.
Natafuta kona yangu kisha nami naketi sakafuni.
Baada ya dakika chache yule mdada aliyejiinamia na kufunika uso kwa mikono yake anainua uso na ninapomtazama vizuri namtambua naye ananitambua na sote tunatabasamu. Tulikutana mtoni siku chache zilizopita tulipoenda kufua na kuchota maji.
"Pole" Namuanza
"Asante".....anajibu kwa sauti ya uchovu.
"Umefanya kosa gani?" Ananiuliza.
"Nimekataa kuwasha sigara ya afande" Mimi namjibu. Anacheka kwa sauti hafifu. Anaonekana amechoka sana.
"Na wewe umefanya nini?" Namuuliza.
Anaguna na kushusha pumzi "Jana nilikuwa natoroka kupitia ile njia ya mchaka mchaka nikiona gari au nikiona wanajeshi najificha porini. Wakati nakaribia kufika Kabuku Nikakutana na Afande (Anamtaja jina) akiwa na wenzake wakanitambua na kuniuliza kibali cha kutoka kambini(Anaanza kulia) ndio wakanipandisha kwenye lile kalandinga na nikarudi nao...(Anazidi kulia)
"Polee Suzy usilie!" Naanza kumbembeleza huku nacheka kimoyomoyo.
Kwa wakati ule sikuwa mkomavu sana kwenye mambo ya imani kwa hiyo nilipofika mule wala sikufanya maombi yoyote wala kuwaza lolote la kiMungu ila nilikuwa na amani tu kuwa nimeshinda jaribu la kuwasha sigara.
Haukupita muda mrefu nikapitiwa na usingizi ambao haukudumu sana kwani nilishtuliwa na sauti kali ya MP aliyefungua mlango kwa nguvu huku akitutaka sote tutoke nje upesi.
Tulitoka nje na kunyung'unywa kisawasawa kwa kwata za vichura, kugalagala mavumbini, pushapu, kimbia-kaa, kutengeneza reli (unaweka mikono juu ya mabega ya aliye mbele yako na yeye hivyo hivyo halafu mnaanza kukimbizwa ole sasa utoe mikono).
Tulinyung'unywa tukanyung'unyika mpaka kagiza kalipoanza kuingia ndipo tukarudishwa mahabusu.
Tulijitupa sakafuni kila mtu akigugumia kwa maumivu kivyake.
Ashukuriwe Mungu alfajiri kesho yake tuliruhusiwa kurudi kwenye kombania zetu japo hata kutembea ilikuwa shida. Ilichukua zaidi ya juma moja maumivu kuondoka na mwili kurudi kwenye hali yake ya awali.
Baada ya hapo sikuwahi tena kupewa adhabu ya peke yangu na hatimaye kipindi cha ukuruta kilipoisha nikateuliwa kuwa Karani wa Kombania na muda mwingi nikawa nafanya kazi za ofisini kama usafi, kupanga mafaili, kutumwa kupeleka barua za kiofisi na kupanga zamu za ulinzi za kombania yangu.
HITIMISHO
1. Popote unakuwapo onesha msimamo wako na imani yako na hii itakuwa ni ulinzi kwako mwenyewe. Wakishajua itikadi yako hawatakushirikisha mambo yasiyofaa na hiyo itakusaidia wewe binafsi katika ujumla wake.
2. Uaminifu unalipa. Wale wale walioniadhibu kwa kukataa kuwasha sigara ndio hao hao walioniteua kuwa karani na kufanya niishi kwa raha baada ya ukuruta.
3. Kuna mambo ambao utafanyiwa katika maisha si kwa sababu unachukiwa, bali Mungu huyaruhusu ili kukukomaza na pia kukupima ili ufae kwenda viwango vingine.
4. Jeshi la Kujenga Taifa ni zuri vijana wasiliogope. Unajifunza kuishi na watu wa aina zote na kuishi mazingira yote. Unajengewa ujasiri na uwezo wa kuvumilia magumu.
5. Kila gumu lina mwisho. Unapokuwa jeshini siku moja huonekana kama wiki lakini hatimaye tulimaliza. Hakuna refu lisilo na mwisho vumilia. Maisha hayana urahisi na vitu vizuri au vya thamani na vya kudumu havipatikani kwa wepesi yabidi kuvumilia kama walivyosema wenzetu "No pain, no gain...No Sweat no Sweet...No Cross no Crown..."
6. Watu ni mtaji. Jeshini ni sehemu ambayo watu wengi huongeza idadi ya watu unaofahamiana nao. Kuna watu tulikutana jeshini na baada ya kumaliza jeshi tukaendeleza urafiki wetu na sasa wamekuwa marafiki wakubwa na zaidi ya marafiki wamekuwa ndugu baada ya kuweza kudumisha urafiki kwa zaidi ya miaka 30 tangu kumaliza jeshi .
7. Wewe ambaye ulipita jeshini ongezea la kwako ......
MWISHO