Kisa Kipya cha Sungura, Alitoka Siku Moja

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2006
Posts
33,771
Reaction score
41,027
Hiki kisa kinakuja, Ukae chini tulia,
Ni cha Sungura mmoja, hapa nawasimulia,
Ilikuwa siku moja, njaa imemshikia,
Njaa imemshikia, Sungura nawaambia!

Ni Sungura yule yule, aliyezizira ndizi!
Ni yule wa mwaka ule, aliyeleta mapozi,
Tuliyemsoma shule, miaka ile ya enzi,
Miaka ile ya enzi, Sungura nawaambia!

Karudi kakasirika, huku tumbo languruma,
Tumbo lake kalishika, huku meno kayauma,
Jasho linamdondoka, huku anahema hema,
Huku anahema hema, Sungura nawaambia!

Sungura akaondoka, kusaka matunda yale,
Akaondoka na shoka, na mkuki na mishale,
Akawaomba mahoka, na akachanjwa na chale,
Na akachanjwa na chale, Sungura nawaambia

Sungura alitafuta, na kutafuta mitini,
Akatafutafuta, msituni mashambani,
Na mwisho akayapata, matunda alotamani,
Matunda alotamani, Sungura nawaambia.

Akayaona mtini, hakuuliza ya nani,
Yameiva kama nini, kajiambia moyoni,
Tunda hili tunda gani, hakuuliza kichwani,
Hakuuliza kichwani, Sungura Nawaambia!

Karuka tena karuka, mwishowe kayafikia,
Ishirini kayashika, Sungura kashangilia,
Tabasamu likatoka, kacheka hata mkia!
Kacheka hata mkia, Sungura nawaambia!

Katafuna kwa haraka, na kumeza pole pole,
Akayala akicheka, akilamba na vidole,
Na njaa ikamtoka, tumbo limejaa tele,
Tumbo limejaa tele, Sungura nawaambia!

Mwishowe akasinzia, na ndoto ikamjia,
Mbali akakumbukia, ndizi alizoachia,
Bahati kajipatia, matunda amejilia,
Matunda amejilia Sungura nawaambia!

Mara kaanza kulia, na ndoto ikapotea,
Tumbo ameshikilia, hakuna cha kuchekea,
Maumivu asikia, huku anachechemea,
Huku anachechemea, Sungura nawaambia!

Kakimbia kijijini, huku analia lia,
Kagaragara na chini, jamani anaumia,
Kaulizwa shida nini, kisa kawasimulia,
Kisa kawasimulia, Sungura nawaambia!

Kaulizwa tunda gani, alilokula jamani,
Akasema mti gani, mapovu yako kinywani,
Kumbe ya sumu watani, yamtokea puani,
Yamtokea puani, Sungura nawaambia!

Akasema nimekoma, nisaidieni jamani,
Nimekoma vya kukoma, mengine sitotamani,
Sasa nimepata homa, hainitoki mwilini,
Hainitoki mwilini, Sungura nawaambia!

Akapoteza fahamu, mauti yako njiani,
Kumbe kali ile sumu, hakuna dawa porini,
Masikini marehemu, yamemkuta jamani,
Yamemkuta jamani, Sungura nawaambia!

Kaditamati natama, beti zangu zimegoma,
Ya Sungura nimesema, ya tamaa isokoma,
Tamaa ina gharama, yaweza toa uzima,
Yaweza toa uzima, Sungura nawaambia!

Na. M. M. Mwanakiiji (Sauti ya Kijiji)
 
Fumbo mfumbue mjinga mwerevu ang'amua S3 siyo tunda la sumu,ndio muarubaini wa kero za muungano.S2 ndizi tulozoea, imedumaza makuzi, haina virutubisho muhimu. Jamani nyakati zatupita.
 
Watanzania mmehariniwa nyinyi mwisho hata sala ya Baba Yetu mtadhani ni ya kisiasa!
 
dah nilikuwa nataka kuchangia hao wa juu wameshanikata utamu
 
Malenga wetu Mzee Mwanakijiji, nakusalimia mzee wetu. Kama hadhira yenye ukosefu wa elimu ya kutosha nimeshindwa kung'amua ujumbe kusudiwa ktk shairi lako. Kama hutojali naomba uliweke shairi lako ktk maelezo mafupi ya kawaida ili nami, Mtanzania wa kawaida toka shule za kata, niweze kujifunza. Natanguliza shukurani.
 
unataka kunambia sungura hana bahati kwa kukosa kuyala matunda enzi zile na unasema hata akipata matunda 20 atakufa kwa mana atayala kwa pupa bila kuwa makini nakukubali malenga wangu malengawangu
 

Uzuri wa kazi kama hii ni wewe kama msomaji kufikiria maana yake kwa undani wake na inakuwa huru kutafsiriwa tofauti tofauti.. sungura ni nani? matunda ni nini? na kwanini?
 
Uzuri wa kazi kama hii ni wewe kama msomaji kufikiria maana yake kwa undani wake na inakuwa huru kutafsiriwa tofauti tofauti.. sungura ni nani? matunda ni nini? na kwanini?

malenga wangu watu wanaotafsiri nyimbo enzi zile walisababisha kufungiwa nyimbo ya tx mpenz (dereva wangu tulia) mana watu walitafsiri kwa mtindo hasi mpaka wakaifungia
 
Uzuri wa kazi kama hii ni wewe kama msomaji kufikiria maana yake kwa undani wake na inakuwa huru kutafsiriwa tofauti tofauti.. sungura ni nani? matunda ni nini? na kwanini?

Sawa mkuu lakini kwa kizazi cha leo ni wachache sana wataweza kutafsiri kazi kama hizi, je, ujumbe utawafikiaje?
 
Sungura kafaa???
Sasa tutapata wapi shairi lingine la sungura ndizi mtini
 


Hivyo ilivyo inanoga zaidi.
 
Sungura kafaa???
Sasa tutapata wapi shairi lingine la sungura ndizi mtini


"Kumbe wala hakufa, Sungura alizimia,
Labda ni kifafa, tabibu atatuambia,
Matunda si ya maafa, tusubiri watanzania,
Tusubiri watanzania, stori itaendelea"
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…