SoC03 Kisiki cha Sodoma na shina jipya linalomea

SoC03 Kisiki cha Sodoma na shina jipya linalomea

Stories of Change - 2023 Competition

Kalamu Nzito

JF-Expert Member
Joined
Aug 13, 2015
Posts
349
Reaction score
805
Mwaka 1990 mwandishi Ralph Epperson alichapisha kitabu kinachoitwa “The New World Order.” Katika ukurasa wa 10 wa kitabu hicho kuna maandiko yanayosomeka:

“New World Order inajuimisha mabadiliko katika:

Ndoa za jinsia moja zitahalalishwa; wazazi hawatoruhusiwa kulea watoto wao (litakua jukumu la Serikali) wanawake wote wataajiriwa serikalini na hawatoruhusiwa kuwa wamama wa nyumbani; taraka zitaongezeka kwa urahisi na ndoa za mwenza mmoja zitatoweka taratibu.”


Historia ya mwandishi huyu haielezi kama ni nabii au mtabiri. Lakini kwenye karne ya 21 tunaona maandiko yake yanatimia hususan, msitari wa kwanza wa aya hiyo. Miaka 25 baadae tangu kuchapishwa kwa kitabu hicho, Mahakama kuu nchini Marekani inatoa uamuzi unaoeleza:

“Marekebisho ya 14 (ya katiba) yanaitaka kila nchi kurasimisha ndoa kati ya watu wa jinsia moja na kuzitambua ndoa kati ya watu wawili wa jinsia moja pale ambapo ndoa yao ilirasimishwa kihalali na kufungwa nje ya nchi.”

Moja ya changamoto zinazoikumba jamii yoyote ile ni mapokeo. Mapokeo kwenye imani, siasa, elimu, utamaduni na kwenye nyanja nyingine muhimu tofautitofauti. Mazuri yanaigwa na mabaya yanaachwa. Hii ni namna nzuri kabisa ya kukua kwa jamii inayojifunza kutoka katika jamii nyingine. Hakuna chujio la maarifa na taarifa kwenye mboni na masikio ya mwanadamu. Chujio pekee ni weledi tuliopewa na Mwenyezi Mungu katika kujua lipi ni jema na lipi ni baya.

Mapenzi ya jinsia moja ni mjadala unaoibua hisia na mitazamo tofauti ulimwenguni kote. Hapa kwetu Afrika, kwa sehemu kubwa mapenzi ya jinsia moja yanapingwa vikali. Idadi kubwa ya wanaopinga mambo haya wanasema kwamba huo sio utamaduni wa Muafrika. Lakini je, utamaduni wa Muafrika ni upi? Dini zilizotawala Afrika hivi leo hazikua sehemu ya utamaduni wa muafrika. Mifumo ya kisiasa na elimu inayotawala sasa haikua sehemu ya utamaduni wa Muafrika. Hayo yote hayakuwepo katika mfumo wa jamii zetu lakini tuliyapokea na tunayaishi. Ni jamii chache sana zinazoishi katika mifumo ya tamaduni zao za asili. Kuna machanganyiko wa tamaduni kwenye jamii zetu. Hoja hii imekua nyundo ya wanaharakati wa mapenzi ya jinsia moja katika kutetea hoja zao.

Katika mtazamo wa kidini na kiimani, hakuna dini yoyote kati ya zile zinazotoka katika uzao wa Ibrahim (Abrahmic religions) ambayo inaunga mkono mapenzi ya jinsia moja. Ukichunguza maandiko, katika vitabu alivyoviandika Musa maarufu kama Torati, ambavyo vipo katika vitabu vya dini zote za uzao wa Ibrahim, mapenzi ya jinsia moja yanapigwa vikali ikielezwa kuwa ni chukizo kwa Mungu.

Katika mtazamo wa kisayansi, wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja mara nyingi wamesikika wakikijitetea kuwa hivyo ndivyo walivyozaliwa. Hata wasomi na wanataaluma mashughuli wamesikika wakieleza haya. Dr. Benjamin Neale kutoka Broad Institute nchini Marekani, ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya vinasaba aliwahi kunukuliwa na jarida la New York Times akieleza kuwa:

“Mapenzi ya jinsia moja yameandikwa katika vinasaba vyetu na ni sehemu ya mazingira yetu… ni sehemu ya aina yetu na ni sehemu ya namna tulivyo.”

Hata hivyo, haijathibitika kisayansi kuwepo kwa vinasaba vya ushoga.

Awali, wakati karne ya 20 inaanza kuelekea ukingoni, harakati za mapenzi ya jinsia moja zilianza kwa kutaka watu wa jamii hiyo watambulike kwenye jamii. Walitaka wapewa haki na vipaumbele kama makundi mengine muhimu. Wakati huo, mataifa mengi yalikua kimya kwenye suala hilo kwa kutoonesha kukubali au kupinga suala hilo. Hakukua na sheria za wazi zinazolinda maslahi ya kundi hili moja kwa moja.

Kadri miaka ilivyozidi kusonga, harakati hizo zikaanza kuelekezwa katika kutafuta haki ya ndoa baina ya watu wawili wa jinsia moja. Mathalani, mwaka 1971 Mahakama kuu ya Minnesota huko Marekani, ilitilia mkazo wa katazo juu ya ndoa za jinsia moja katika kesi ya Baker dhidi ya Nelson, wakati huo mambo haya yakiwa bado hayajapokelewa kwenye jamii. Hata hivyo, maamuzi hayo yalikuja kutenguliwa rasmi kwenye kesi ya Obergefell dhidi ya Hodges (2015) ambapo maamuzi ya kesi hii yalifungua njia katika kuhalalisha na kurasimisha ndoa za jinsia moja.

Barani Afrika, Afrika kusini ilikua nchi ya kwanza kurasimisha ndoa za jinsia moja mnamo mwaka 2006. Lakini pia ni nchi ya tano duniani kurasimisha ndoa za jinsia moja. Mapenzi ya jinsia moja ni haki ya kikatiba nchi Afrika kusini kama inavyoainisha katika Ibara ya 9 (3) cha katiba ya nchi hiyo. Vilevile, ndoa za jinsia moja zilirasimishwa kwenye sheria ya Civil Union Act iliyotungwa mwaka 2006.

Hata hivyo, serikali za nchi nyingi barani Afrika bado zimekua na kigugumizi kwenye suala zima la mapenzi ya jinsia moja. Tayari nchi 22 zimekwishahalilisha mapenzi ya jinsia moja kwa kufuta zile sheria ambazo zilikua zinatoa adhabu kwa washiriki wa mapenzi ya aina hiyo. Baadhi ya nchi hizo ni Angola (2021), Botswana (2019), Mozambique (2016), Lesotho (2010) na Shelisheli (2016).

Licha ya hayo, zipo nchi barani Afrika ambazo zinaendelea kupinga wazi mapenzi ya jinsia moja. Mathalani, mwaka huu bunge la Uganda limepitisha muswada ambao unafanya mapenzi ya jinsia moja kuwa kosa la jinai. Muswada huo umeweka adhabu kali kwa mtu yeyote atakayekutwa akijihusisha na masuala hayo. Adhabu haitotolewa kwa wanaofanya tu, bali hata wale wanaotangaza, kutetea, kufadhili na mambo mengine ya namna hiyo.

Pamoja na kwamba utamaduni wa kiafrika umepoteza ladha yake ya asili kwa kuchangamana na tamaduni za kigeni, hili haliifanyi Afrika kuwa jalala la tamaduni za majaribio. Afrika inahitaji uhusiano na mataifa yaliyoendelea ambao utaimarisha uchumi, sayansi na teknolojia pamoja, afya na elimu. Hakuna faida yoyote Afrika itapata kutokana na mapenzi ya jinsia moja.

Jamii inaongozwa na taratibu na sheria. Sheria zetu ziwe wazi katika kukataza mapenzi ya jinsia moja. Sheria za Tanzania bado kwa kiasi kikubwa zipo kimya kwenye masuala ya mapenzi ya jinsia moja. Kama sheria inaweza kuchochea kwa kutoa uhuru wa mapenzi ya jinsia moja kama ilivyo kwa nchi nyingine, ni imani yangu kwamba sheria pia inaweza kukataza na kutokomeza umomonyokaji huo wa maadili.

Ni wajibu wa serikali, taasisi za kidini na mashirika ya kijamii kukemea kwa uwazi suala hili. Lakini wajibu mkubwa unaanzia nyumbani kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Kisiki cha Sodoma kimeanza kustawi. Ni ishara tosha kwamba mizizi ya kisiki hicho haikufa. Hata hivyo kwa pamoja, tunaweza kuilinda Tanzania na Afrika kwa ujumla dhidi ya umomonyokaji huu mkubwa wa maadili.

Mola atulinde sisi na vizazi vyetu.
 
Upvote 4
Back
Top Bottom