Hapa ninakuunga mkono Mkuu. Sera ya Tanzania ya lugha imepotoka. Nakumbuka tangu mwaka 1969 Serikali ilitangaza nia ya kukifanya Kiswahili sio lugha ya Taifa tu bali lugha ya kufundishia, alkini sera hii daima haikutekelezwa badala yake tunawasumbua wanafunzi. Tunawaumisha vichwa wanafunzi wetu ambao inawabidi wafikirie katika Kiswahili wakati wanapokumbana na swali katika lugha ya Kiingereza. Mtoto hujifunza zaidi katika lugha yake ya kwanza. Faida yake watoto wanakuwa wepesi wa kufahamu na wabunifu kwa kutumia lugha yao kuliko kutumia lugha ya kigeni. Hapa hatusemi kuwa Kiingereza kiwachwe, bali kisomeshwe kama lugha ya pili tangu miaka ya mwanzo ya elimu.
Wanaotetea Kiingereza wanadai kuwa Kiswahili hakijitoshelezi. Hii si kweli. Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili imekuwa ikisanifisha Kiswahili kwa muda mrefu katika nyanja zote na tayari kuna makabrasha kwa makabrasha ya maandishi yaliyokaa katika makabati bila ya kupelekwa kwa watumiaji.
Kiswahili kina utajiri mkubwa na ulaini wa kulibadilisha neno lolote la lugha ya kigeni (hasa kutoka Kiingereza tunachoking'ang'ania) na kulitohoa kukidhi matamshi, maana na maandishi ya Kiswahili.
Wakati umefika kukifanya Kiswahili lugha ya kufundishia viwango vyote vya ellimu.