Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Kitabu cha maisha ya Sheikh Sayyid Omar Abdallah maarufu kwa jina la Mwinyi Baraka kilochoandikwa na Prof. Mohamed Bakari kimewasili nchini.
Naogopa kuandika pitio la kitabu hiki kwa kuwa nahisi huu ni mzigo ambao mimi sina uwezo wa kuubeba.
Kwanza kwa uzito wa mwandishi mwenyewe Prof. Mohamed Bakari na pili kwa uzito wa Mwinyi Baraka.
Mwinyi Baraka akifahamika sana Afrika ya Mashariki na ilikuwa kawaida yake akifika katika miji ya nchi hizi kufanya darsa ambazo zilijaza wasikilizaji iwe Dar es Salaam, Nairobi, Mombasa, Kampala au miji midogo ya pembezoni.
Mwandishi anakumbuka kumsikiliza Sheikh Sayyid Omar Abdallah kwa mara ya kwanza mwaka wa 1964 Moshi akiwa mtoto mdogo kwenye Maulid ya Mfungo Sita yaliyokuwa yanasomwa kwenye kiwanja cha mpira cha Muslim School wakati wa East African Muslim Welfare Society.
Mwinyi Baraka alijaliwa haiba ya kumfanya mtu yeyote ajihisi ni sehemu ya sheikh na alikuwa na kipaji cha kuzungumza cha kumfanya msikilizaji asichoke kumsikiliza, msikilizaji akiwa wa daraja lolote la elimu awe na elimu ndogo au sheikh mkubwa wa kutajika.
Lakini kubwa sana ambalo sheikh kwa hakika alikuwa hodari ni ule uwezo wake wa kuzungumza na wale wasiokuwa na adabu ya elimu wale ambao walihisi wao wanajua na wakataka kujipima na yeye iwe katika elimu ya sekula au ya dini.
Wale ambao walijaaliwa kushuhudia mjadala wa aina hii yale waliyojifunza kutoka kwa Mwinyi Baraka yamebaki katika kumbukumbu zao maisha.
Mwanafunzi asiye na adabu katika semina iliyotayarishwa na Vijana wa Kiislam wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam pengine kwa chuki tu ya Uislam na kwa kumwangalia sheikh kwa mavazi yake ilimshangaza kafika vipi kuzungumza ndani ya Nkrumah Hall, ukumbi ambao umeshuhudia wasomi wakubwa wa dunia wakialikwa vipi huyu mzee mwenye kilemba na kizibau na yeye azungumze ndani ya ukumbi ule.
Kijana kutokana na maudhui ya mazungumzo ya Mwinyi Baraka katika swali lake alimwambia sheikh kuwa fikra zake hazina nafasi katika ulimwengu wa ''scientific materialism.''
Alimjibu kijana kwa kwanza kumsomea kutoka kichwani ukurasa mmoja kutoka kitabu cha mwanafilosofa wa Kifaransa Jean-Paul Sartre kwa Kifaransa kisha akafanya tafasiri kwa Kiingereza.
Ukumbi ulikuwa kama umemwagiwa maji baridi.
Ulikuwa na ukimya usiokuwa wa kawaida.
Alimaliza kwa kumweleza kijana kuwa hayo ambayo yeye kayaona ya leo ni ya zamani sana na wasomi wengi wameyazungumza kwa miaka mingi iliyopita.
Kisha akahitimisha kwa kumwambia kuwa walimu wake pale Chuo Kikuu watamsaidia kwa kumsomesha zaidi.
Hadhira haikutambua kama kusaidiwa huko ni kufunzwa adabu ya elimu ama somo lenyewe.
Kijana na walimu wake waliokuwa pale ukumbini waliondoka vichwa chini.
Huyu ndiye Mwinyi Baraka ambae sote tunamshukuru Prof. Mohamed Bakari kwa kuandika maisha ya msomi huyu wa Chuo Kikuu Cha Oxford, Uingereza.
Kitabu kitapatikana Ibn Hazm Bookshop Msikiti wa Manyema na Msikti wa Mtoro, Tanzania Publishing House na Masomo Bookshop Zanzibar kwa bei ya TShs: 45,000.00.