Kitabu: Desturi za Wachagga

Kitabu: Desturi za Wachagga

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
9,189
Reaction score
16,128
Kitabu hiki kizuri sana. Kina mengi ya kujifunza yenye msaada hata leo.

Kimetungwa na S. J. Ntiro
Kuchapwa 1953.
Unaweza kukisoma ndani ya maktaba app. TuPM Kuungwa.


DIBAJI YA WATOAJI KITABU

Juzi juzi mtaalamu mmoja wa mambo ya Afrika aliandika:

"Bila mikusanyo mingi ya hakika ya mambo ya zamani tuyaonayo katika historia, na bila kufahamu vema hali ya nchi yetu ilivyokuwa hapo kale, basi hatutakuwa na nguvu za kuendelea mbele nasi tutapata hasara tu, maana tutakosa kuwa na usawa na ufungamano."

Afrika ya Mashariki ni nchi isiyo na vitabu vingi vya historia. Wareno waliandika mambo kadha wa kadha ya wakati waliotawala, lakini hayapatikani wala hayasomeki ila kwa shida. Kiswahili peke yake kilikuwa na maandishi yake kabla ya mwanzo wa kazi ya Dr. Krapf 1844, nayo yalitaja hasa mashindano ya Waarabu waliopigania dola zao na enzi zao pwanipwani.

Lakini kuna sehemu nyingine za maarifa ya historia ambayo ni bora sana, lakini hayo hayajajulikana na wataalamu wengi bado ila wachache tu. Maarifa hayo ni desturi na masimulizi ambayo mpaka sasa yana nguvu katika maisha ya Afrika ya Mashariki. Mfuatano wa vitabu unaoitwa DESTURI NA MASIMULIZI KATIKA AFRIKA YA MASHARIKI utawaonyesha Waafrika na waandishi njia ya kuvumbua mambo hayo kama Wazungu wachache tu wawezavyo, ili kuandika habari za baadhi ya desturi ambazo wamezizoea, na kuhifadhi masimulizi ya kale ambayo yamepitishwa kwa midomo. Kama tujuavyo siku hizi wazee hawawasimulii vijana kama ilivyokuwa desturi katika siku za zamani.

Vile vile, pamoja na mfuatano huu wa vitabu vyenye maarifa ya maisha ya makabila, kuna mwingine ambao unatolewa siku hizi mfano wa huo. Vitabu vyake vina habari za maono ya wasafiri wa zamani waliokuja huku Afrika ya Mashariki, na mambo yaliyowapata.

Mifuatano miwili hiyo ya vitabu inakusudiwa kuwapa vijana wa Kiafrika na watu wa mataifa mengine nafasi kubwa ya kujifunza historia ya nchi hii pamoja na masimulizi na desturi.
 
YALIYOMO
1 DIBAJI YA WATOAJI KITABU
2 SEHEMU YA KWANZA-KABLA YA WAZUNGU
3 MAHALI MLIMA WA KIBO ULIPO
4 UZURI WA KIBO
5 WACHAGGA NA MLIMA WA KIBO
6 FAIDA YA UREFU WA MLIMA KATIKA NCHI
7 ASILI YA WACHAGGA
8 VITA KATI YA WACHAGGA WENYEWE
9 VITA KATI YA WACHAGGA NA MAKABILA MENGINE
10 MATOKEO YA VITA JUU YA NCHI
11 NGUVU ZA WAGANGA KATIKA NCHI
12 NGUVU ZA “WAMANGI” JUU YA RAIA
13 KOO ZA KABILA LA KICHAGGA
14 CHAKULA KIKUBWA CHA WACHAGGA
15 VITU VYA KUPENDEZA MAISHA HAVIKUWAKO
16 SEHEMU YA PILI - USTAARABU WA WAZUNGU
17 WAARABU NA UTUMWA
18 DINI YA KIKRISTO NA UTUMWA
19 DINI YA KIKRISTO NA UCHAWI
20 DINI YA KIKRISTO NA TAABU ZA AFYA
21 SERIKALI YA KIDACHI NA WACHAGGA
22 VITA YA 1914-1918, KATI YA WADACHINA WAINGEREZA
23 SERIKALI YA KIDACHI NA ILE YA KIINGEREZA
24 MWANZO WA KAHAWA KILIMANJARO
25 K.N.C.U. KAMA ILIVYO SIKU HIZI
26 SEHEMU YA TATU-SIKU ZIJAZO
27 K.N.C.U. KATIKA SIKU ZIJAZO
28 UTAWALA WA KIENYEJI
29 “VIHAMBA” VYA WACHAGGA
30 BIASHARA NA WAHINDI
31 BIASHARA ZA KILIMANJARO
32 NI LAZIMA WACHAGGA WAIPENDENCHI YAO
33 SERIKALI YA KIINGEREZA NI KIONGOZICHA WACHAGGA
 
SEHEMU YA KWANZA-KABLA YA WAZUNGU



MLANGO WA I

MAHALI MLIMA WA KIBO ULIPO

Kibo ni mlima ulio mrefu kuliko milima mingine yote ya Afrika. Urefu wake toka usawa wa bahari ya Hindi mpaka kileleni wapata futi 19,700. Maana ya neno hili Kibo ni madoadoa, yaani alama nyeupe na nyeusi, kwa umbali kama uonekanavyo na sababu ya mtelemko wa barafu juu ya jabali lake. Alama hizi huonekana wazi zaidi baada ya mvua au wakati wa baridi nyingi juu ya mlima.

Mlima wa Kibo una kilele kingine cha pili kiitwacho Mawenzi. Urefu wake ni futi 17,388. Maana ya neno hili Mawenzi ni "pengo". Kuna hadithi maarufu ya Wachagga jinsi Mawenzi ulivyopata "pengo" hili. Mwisho wa hadithi hii ni kwamba mlima huu ulikuwa ukitoa moto hapo zamani.

Mlima wa Kibo uko kati ya Tanganyika na Kenya. Mpaka wa nchi hizi mbili umegawa mlima sehemu mbili: sehemu moja iko Tanganyika na sehemu nyingine iko Kenya. Sehemu ya Tanganyika ndiyo kubwa na yenye rutuba zaidi kuliko ile ya Kenya.

 
MLANGO WA 2

UZURI WA KIBO



Kibo ni mlima wenye kupendeza macho. Mtu akiona Kibo mara ya kwanza atafurahiwa kupita kiasi. Ikiwa haukufunikwa na mawingu atauona mlima mrefu wenye theluji na barafu ya milele. Jua likitokea upande mmoja, theluji na barafu humetameta vizuri mno. Lakini kwa upande mwingine weusi wa majabali na barafu huonekana vizuri zaidi. Wakati mwingine majabali huwa yamefunikwa na theluji nyembamba inayoonckana kama kioo. Vitu hivi vyote vikionekana kwa wakati mmoja machoni pa mtu anayeuangalia mlima kwa mara ya kwanza humstaajabisha sana. Ikiwa mlima umefunikwa na mawingu ni vigumu kuona cho chote. Wakati mwingine mawingu mengi huzunguka mlima, na upande wa chini wa mawingu haya huwa na mawingu mazito; na juu yake huwa na mawingu meupe. Weupe wa mawingu haya huendelea kuwa mwembamba mpaka mwisho wake sehemi ya juu ya mlima huonekana peke yake. Kuna wakati mwingine mawingu haya yanapoonekana kama yanatembea kuuzunguka mlima, na mlima nao huonekana kama unaelea juu ya mawingu.

Misitu iliyo katika shina la mlima huo huonekana vizuri, hasa ukiwa mbali nao: weusi wa misitu huonekana vizuri mbele na chini ya weupe wa theluji katika mlima. Mito michache hutokea juu ya misitu pamoja na chemehemi nyingi. Nchi ya Kilimanjaro hupata mvua nyingi kwa sababu ya misitu hii iliyo mikubwa. Uzuri wa mlima huu huonekana kwa njia nyingi na unapendeza kila mtu anayeutazama.
 
MLANGO WA 3

WACHAGGA NA MLIMA WA KIBO

Kwa kila Mchagga, Kibo ni kitu kilicho ndani kabisa. Hata kama Mchagga yuko mbali na nchi yake namna gani, mlima huu uko ndani ya roho yake na fikara zake. Ni kama kusema mlima huu uko ndani ya damu yake. Pengine hii ndiyo sababu mojawapo inayomfanya Mchagga asipende kuondoka katika nchi yake. Kwa desturi Mchagga ni mtu anayependa kuishi katika nchi yake, kuwa mfugaji au mkulima na kuishi maisha ya kujitegemea mwenyewe. Usemi mmoja wa Kichagga wasema, "Nyumbani kwa mtu ndipo mahali pakubwa kuliko mahali pengine po pote, hata kama ni juu ya jiwe." Wachagga wengine wanaamini kuwa Mchagga akiondolewa Kilimanjaro hawezi kuishi miaka mingi. Kwa upande wa Machame kuna mahali mlima unapoonekana kama ng'ombe aliyesimama. Theluji ikipungua juu ya mlima, ng'ombe huyu huonekana mdogo kuliko kawaida. Wachagga wanamwita "ng'ombe wa Mungu".
 
MLANGO WA 4
FAIDA YA UREFU WA MLIMA KATIKA NCHI


Urefu wa mlima wa Kibo una faida nyingi katika nchi. Wachagga wanaishi katika miteremko ya mlima na karibu wote wanaishi kati ya mwinuko wa futi 3,000 hata futi 6,000 kutoka usawa wa Bahari ya Hindi. Kwa kuwa mlima ni mrefu sana, mito huwa na maji meupe yenye baridi sana yasiyokauka hata mara moja. Maji ya mito michache hutokea juu ya mlima na kupita misituni ambapo yanaongezeka kwa chemchemi, na mwishowe yanawafikia watu.
Wachagga huchimba mifereji ya maji kutoka katika mito, mifereji hii hutumiwa kwa kunywesha mashamba yao ya ndizi, mbeke, mahindi, maharagwe, na ya mavuno mengine. Wakati wa mvua mito yote hufurika na mifereji huharibiwa na maji. Baada ya mvua kila mwaka mifereji huchimbwa ili maji ya kunywesha mashamba yapatikane. Kila Mchagga ni lazima ajibidiishe na kufanya kazi ya kuchimba mifereji, na asipojibidiisha ndizi hukatwa kutoka migomba yake na kuliwa na watu. Wakati wa mvua, maji ya mifereji hayatakiwi mashambani, kwa hiyo haidhuru kama mifereji ikiwa haina maji. Maji safi ya mito na ya mifereji hutumika kwa kunywa, kupika chakula na pombe ya Kichagga.

Misitu ya mlima wa Kibo ina faida nyingi mno kwa Wachagga. Wachagga huchukua vyeti kwa utawala wa kienyeji ambavyo huwapa ruhusa ya kukata miti kwa kujengea nyumba zao. Misitu hii ina miti ya namna nyingi ya kujengea nyumba. Miti mingi huchukua muda wa miaka mingi kukua. Miti hii wakati ikizeeka huko misituni huanguka chini na sehemu ya nje huoza. Miti ya namna hii Wachagga wakiikuta huipasuapasua katikati na kutoa vipande vikubwa, na kutoa nguzo nyingi zilizochongwa za kujengea nyumba katika mti mmoja. Kama miti iliyoanguka haipatikani ni lazima wakate miti iliyosimama. Kwa faida ya misitu kwa maisha ya Wachagga wa baadaye, ingekuwa ubora kuitumia ile miti iliyoanguka chini tu.

Wachagga hukata fito za kujengea nyumba kutoka msituni. Fito hizi hupendwa na watu kwa kuwa haziingiliwi na mchwa kwa urahisi. Fito za namna nyingine zikichimbiwa udongoni huliwa na udongo baada ya miaka michache. Kamba za kufungia fito wakati wa kujenga nyumba hupatikana misituni; kamba hizi zina nguvu kuliko zile zipatikanazo katika mashamba ya wenyeji.

Siku hizi ni watu wachache sana waendao misituni kutafuta nguzo, fito, na kamba za kujengea nyumba zao, kwa sababu kuna miti mingi ya kigeni iliyopata kuingia kutoka nchi za mbali ambayo kwa jumla huitwa, "Miti Ulaya”. Miti hii haina nguvu kama ile ya misituni, kwa hiyo nyumba zijengwezo kwa miti hii huanguka baada ya miaka michache. Sababu ya nyumba kutokuwa na nguvu ni kwa kuwa watu wa siku hizi hawana uangalifu juu ya kujenga nyumba za kienyeji kama watu wa zamani. Labda wana shughuli na kazi nyingi kuliko babu zao. Wanasoma shule, wanalima na kuuza kahawa. Wanafanya kazi kama za ukarani, ualimu na nyinginezo. Zote hizo ni kazi ambazo babu zao hawakuzifanya.

Urefu wa mlima wa Kibo huleta faida nyingi zitokazo misituni. Si ajabu kusema kuwa maisha ya Wachagga yanategemea urefu wa Kibo.
 
MLANGO WA 5

ASILI YA WACHAGGA



Wachagga ni kabila lenye mchanganyiko wa makabila mengi sana. Makabila haya yameingia katika nchi ya Kilimanjaro katika nyakati tofauti. Makabila mengi yameingia Kilimanjaro yakikimbilia mwinuko wa nchi ili yaweze kuwaepuka maadui wao. Makabila mengi yalivutwa na rutuba ya nchi. Kwanza walijenga nyumba zao porini, lakini baadaye walipanda milima na kushika mahali kulikokuwa na vyakula zaidi. Iliwapasa kuwaheshimu wakubwa wa nchi ili wawaruhusu kuingia katika nchi. Makabila mengine yaliwafuata watu waliokuwa wakiishi katika nchi kwa kusudi la kuwanyang'anya mali, kama ng'ombe, mbuzi, na kondoo zao. Mara kwa mara mapigano yalitokea. Wenyeji waliwakimbilia kwa mikuki na marungu kuwazuia wasichukue mali zao. Wakati mwingine makabila yaliyoingia yalishindwa na wenyeji, lakini wakati mwingine ilikuwa kinyume. Kwa ufupi, hizi ndizo sababu kubwa zilizovuta makabila mbalimbali yaliyoingia Kilimanjaro.

Lugha za Kichagga ni uthibitisho mmoja mkubwa wa kuonyesha kuwa asili ya Wachagga ni makabila mengi. Nchi nzima ya Kilimanjaro imegawanyika katika sehemu ndogo ndogo 22 za watu wasemao lugha tofauti za Kichagga. Maneno ya sehemu moja ni tofauti na maneno ya sehemu nyingine kwa namna wanavyotamka ijapokuwa mtu wa sehemu moja anaweza kuelewa asemayo mtu wa sehemu nyingine. Tofauti ya namna hii katika sehemu za kabila moja si nzuri kwa sababu ni rahisi kuleta matangamano katika nchi.

Sehemu kubwa ya asili ya kabila la Kichagga ni Masai. Masai ni watu wapendao ng'ombe. Waliingia Kilimanjaro wakapigana na wenyeji na kuwanyang'anya ng'ombe na mbuzi na kondoo: kila wakati Masai walipokuja ilikuwa vita. Wengi wa Masai walifukuzwa na kurejea maporini ambako wanaishi mpaka leo, lakini wengi wao walibaki katika nchi wakageuka kuwa Wachagga. Kupata wanawake lilikuwa kusudi lingine lililowafanya Masai kupigana na watu waliokaa Kilimanjaro. Baada ya vita ambazo Masai walishinda, waliwachukua wanawake mateka Masaini. Tangu zamani za kale desturi ya kuwavizia wanawake na kuwaiba inaendelea mpaka hivi leo kidogo kidogo maporini. Siyo kwamba Masai wanawatesa wanawake hawa ila waliwapeleka kuzidisha kabila lao.

Wasambaa, Wapare, Wameru na Wakilindi ni makabila yaliyoingia Kilimanjaro katika nyakati mbalimbali. Makabila haya manne yaliingia kwa upole na utaratibu kuliko Masai. Mpaka leo hivi Wapare wanaingia Kilimanjaro ya mashariki kwa wingi.
 
MLANGO WA 6

VITA KATI YA WACHAGGA WENYEWE

Makabila haya yote yalipokwishaingia Kilimanjaro, ndipo jina la Wachagga lilipoanza. Nchi nzima ilikuwa na sehemu 22, na kila sehemu ilikuwa na "mangi" wake. "Mangi" wa sehemu moja alikuwa hana uhusiano na "mangi" wa sehemu nyingine. Alikuwa akiwatawala watu wake kama alivyopenda bila kumshauri "mangi" jirani yake juu ya jambo lo lote. Kila "mangi" alikuwa bwana mkubwa miongoni mwa watu wake, alipewa heshima na watu wake. Misukosuko mingi iliyotokea Kilimanjaro ililetwa na fitina kati ya watu wa "mangi" mmoja na wale wa 'mangi" mwingine.

Mara nyingi njaa ni kitu kilicholeta vita kati ya mangi" mmoja na "mangi" mwingine. Njaa ilitokea mara kwa mara kwa kuwa watu hawakujua njia za kuweka vyakula vya kutosha kwa wakati wa shida ya chakula. Kama chakula kilipungua katika nchi ya "mangi" mmoja wale watu hawakuweza kupata chakula kutoka kwa watu wa "mangi" wa sehemu nyingine kwa sababu walikuwa maadui, hapo ilibidi kupigana au kufa kwa njaa. "Wamangi" wengine waliokuwa na nguvu waliwanyang'anya wenzao milki zao na kuwa na nchi kubwa zaidi. Walipigana na wale "wamangi" ambao hawakuwa na nguvu kama wao. Kwanza waliwauliza waingie katika milki yao: mara nyingi walikataa na vita ilianza. Yule aliyeshinda ndiye aliyetawala mwingine pamoja na nchi yake yote; lakini ilikuwa vigumu kumtawala "mangi" na watu wake wote. Mara nyingi "mangi" aliyeshindwa aliviziwa na kuuawa kwa hila. Kwa desturi ya Kichagga ilikuwa aibu kubwa kumuua "mangi" au mtu mkubwa katika nchi baada ya mapigano.

Mara nyingi magombano kati ya watu wa "mangi" mmoja na mangi" mwingine yalitosha kuleta vita kati ya "wamangi" wawili. Baada ya ugomvi, watu walikwenda kumwarifu "mangi" wao. "Mangi" wao alifikiri bila shaka yule "mangi" mwingine aliwatuma watu wake kumchokoza yeye na raia zake. Matokeo yake yalikuwa mapigano kumwonyesha "mangi" mwenzake kama ni lazima apewe heshima kwa kuwa alikuwa mkubwa kuliko yeye.

Wivu ni kitu kingine kilicholeta vita kati ya "mangi " mmoja na "mangi" mwingine. Ikiwa "mangi" mmoja alikuwa na nguvu kuliko mwingine, aliona wivu juu ya "mangi" yule. Alitafuta njia ya kumchokoza ili vita itokee, na baada ya kumshinda alichukua mali yake yote. Mali yote iliyoletwa kutoka kwa "mangi" aliyeshindwa iliwekwa mikononi mwa "mangi" aliyeshinda. Aligawanya mebele mateka haya kati ya majemadari wake na sehemu ya mateka ilipelekwa nyumbani kwake.

Mara kwa mara ndugu wa ukoo wa "kimangi" walichochea fitina wakigombea utawala. Matokeo ya fitina yalikuwa nchi kugawanyika sehemu mbili; sehemu moja ilimfuata mwingine. Vita kati ya wamangi" wa Kichagga ilikuwa vibaya kwa kuwa badala ya kuunga nguvu zao ili nchi iendelee mbele, iliwabidi kutumia nguvu nyingi wakipigana wenyewe kwa wenyewe. Watu walichimba mahandaki marefu ambayo yaliwachukua muda mrefu. Uzuri wa mahandaki haya ni kuwa yaliwafanya Wachagga kutumia akili zao na wengi wao waliweza kuishi humo kwa siku nyingi na kupona. Handaki lilichimbwa kama yadi 10 kwenda chini. Maadui waliingiza maji ya mfereji katika handaki, lakini maji yalitokea mtoni. Kwa pembeni ya handaki walitengeneza vyumba ambavyo walijificha na kuwavizia maadui walioingia. Pia katika baadhi ya vyumba hivi ndimo walimoweka ng'ombe, mbuzi, kondoo na mali zao zote. Wakati mwingine maadui waliyafukia mahandaki haya na watu walitoka nje kwa njia ya mtoni.

Wakati vita hivi vilipokuwa vikiendelea, watu wengine waliishi ndani ya mapango. Mapango haya yalitengenezwa katika majabali ya pande za mito mikubwa. Mahali palipokuwa na maanguko ya maji palifaa sana kwa maana sauti za watu, na ng'ombe, na mbuzi, na za kondoo hazikusikiwa na maadui. Wakati wa usiku ndio uliokuwa wakati wa kutoka nje na kwenda kutafuta vyakula. Lakini maadui walishambulia vyakula vyote; vile ambavyo hawakuweza kula au kubeba wakavichoma moto.

Katika vita hivi watu wazima waliuawa pamoja na watoto wa kiume lakini wale wadogo walichukuliwa mateka pamoja na mama zao na watoto wa kike. Mateka wa kiume walikuwa watumwa na kufanya kazi ngumu za kupasua kuni, kulisha ng'ombe, kulima na kukoroga pombe ya Kichagga. Mateka wengine wa kiume walifanya kazi zao vizuri sana, ili mabwana wao wawapende na kuwapa mashamba na kuwaoza. Mateka wanawake na watoto wa kike karibu wote waliolewa, wachache walikuwa vijakazi kwa "wamangi" na kwa watu wakubwa; lakini mateka wengine waliweza kutoroka na kurudi makwao. Kwanza walijifanya kama wao ni wenyeji na kutoroka pole pole.
 
MLANGO WA 7

VITA KATI YA WACHAGGA NA MAKABILA MENGINE



Vita vilitokea kati ya Wachagga na makabila mengine ya pembeni. Kusema kuwa Wachagga walipigana na makabila mengine ya pembeni siyo kusema watu wa Kilimanjaro nzima walijiunga na kupigana na maadui wao, ila ulikuwako wakati ambao makabila ya pembeni yalishambulia "mangi" mmoja. “Mangi" huyo aliyeshambuliwa kama alikuwa na nguvu kuliko wenzake aliwaita na kuwaamuru wapigane upande wake, au kama sivyo, kila "mangi" alijipigania upande wake na kujaribu kuwafukuza maadui. Vita ya namna hii haikuendelea kwa muda mrefu kwa sababu maadui wakisha teka ng'ombe na watu walitoroka na kwenda zao. Baada ya miezi michache pengine walirudi na kuendelea kuzishambulia nchi zilizo majirani.

Hapa Masai ni mfano mzuri. Ijapokuwa wengi wa Masai walikuwa wamekwisha geuka kuwa Wachagga, wengi wao walibaki nje wakijaribu kushambulia mara kwa mara na kukimbia; kama walishambulia watu wa "mangi mmoja walirudi baada ya muda na kushambulia majirani.

Nchi ya Kilimanjaro ilivuta makabila mengi walio majirani kwa kuwa ilikuwa na vyakula vingi. Bila shaka Wachagga hawakuyapenda makabila haya yaingie na kupunguza vyakula vyao. Migogoro mingi ilitokea kati ya Wachagga na makabila haya; Wachagga walijiona kuwa na nguvu kuliko makabila mengine. Zilikuwako sababu nyingine ndogo ndogo zilizowafanya Wachagga wapigane na makabila ya pembeni, lakini hizo ndizo sababu kubwa.
 
MLANGO WA 8

MATOKEO YA VITA JUU YA NCHI

Hakuna kitu ambacho kilizuia maendeleo ya nchi Kilimanjaro kama vita. Vita ilifanya nchi kurudi nyuma miaka mingi kwa sababu ya mapigano yaliyotokea baada ya watu kufika huko. Karibu maisha yote yalitumiwa kujitengenezea njia za kujilinda maadui badala ya kuendesha ustaarabu na mambo yenye manufaa kwa nchi. Mikuki ya kupigania vita ilitengenezwa: chuma cha kutengenez mikuki kilipatikana katika nchi za mbali. "Wamangi" waliwatuma watu wao kwenda kununua vyuma, na wengi wa waliuawa njiani na maadui, wale waliookoka walichuku muda mrefu kurudi

Ngao nyingi zilitengenezwa kwa makusudi ya vita na hii ikawa kazi ngumu. Baadhi ya ngao zilitengenezwa kwa ngozi ya ng'ombe, zingine kwa ganda la mti mkubwa na zingine kwa ngozi ya wanyama wa porini. Si kweli kusema kuwa ilikuwa vibaya kutengeneza vyombo hivi vya vita kwa kuwa viliwafundisha Wachagga kutumia akili zao. Kwa hiyo vita na hivi vilikuwa na manufaa pia kwa Wachagga.

Nchi haikuwa na amani kwa sababu haikuwezekana kujua vita itatokea lini. Kila Mchagga aliishi na wasiwasi wa roho. Walilima vyakula lakini hawakujua kama watavuna kabla vita haijatokea. Wanawake wajawazito na watoto wadogo waliona taabu kwa sababu iliwabidi kukimbia maadui walipokuja!

Watu wakubwa katika nchi walikuwa na raha kwa sababu walikuwa na vijakazi na watumwa wa kuwafanyia kazi kwa kuwa walikuwa na nguvu ya kuwapa chakula, na vita ilipokuja walipigana na maadui kabla wao au maadiu kushindwa. Ijapokuwa watu wadogo walijipatia hifadhi kadha wa kadha kwa matajiri, mara nyingine waliona taabu kuwategemea watu wengine ambao walikuwa wakubwa na wenye mali. Watu ambao ni maskini walikuwa na raha fulani walizopewa na mabwana zao, lakini walibaki na umaskini wao bila kuwa na njia ya kufanikiwa. Hawakuweza kupata mali wenyewe na kwa sababu hii uchungu wa siku zote uliwaingia mioyoni mwao.

Kwa upande mwingine vita hizi za zamani ziliwapa watu manufaa ambayo yaliendelea nao mpaka leo hivi. Ijapokuwa Wachagga walirudi nyuma, walakini walijifunza kutumia akili zao za kichwa, na kugundua namna ya kuchimba mahandaki na kutengeneza mikuki na ngao, na kuchungua habari za maadui.
 
MLANGO WA 9

NGUVU ZA WAGANGA KATIKA NCHI

Waganga walikuwa na nguvu katika nchi, na kupewa heshima nyingi. Walikuwako waganga wa namna nyingi; kama wale wa kuleta na kukomesha mvua, wa kutibu wagonjwa na wale waliokuwa na ujuzi wa kutazama utumbo wa ng'ombe au mbuzi na kondoo. Kila Mchagga aliamini kuwa maisha yake yalikuwa mikononi mwa waganga ambao walijua habari zote za miili yao. "Wamangi" waliwaheshimu waganga pia kwa sababu kila kitu waganga walichosema Wamangi" walifuata. Kama “wamangi" walitaka kitu fulani kifanyike waliwaita kwanza waganga na kuwauliza kama ilikuwa vizuri kitu hicho kitendeke au sivyo. Kama waganga walisema kisitendeke, "wamangi" hawakukifanya

kitu hicho.

Waganga walikuwa na maarifa mengi. Walipewa heshima na watu kwa sababu walikuwa na kazi ya kutunza afya ya watu. Walikuwa na madawa mengi ya majani na maganda ya miti yaliyoponya magonjwa mengi. Ni ajabu kwamba magonjwa mengine yaliyoponywa na madawa haya wakati Wazungu walipofika, hawakuweza kuyaponya kwa madawa ya Kizungu. Mpaka leo hivi yako magonjwa fulani ambayo huponywa na madawa haya lakini madawa ya Kizungu hushindwa.

Waganga hawa walijidai kuelewa na matumbo ya ng'ombe na mbuzi na kondoo; wakati mbuzi wa kutambika alipochinjwa, waganga walikuja kutazama utumbo wake Kama utumbo huo ulikuwa namna fulani, vitu vingi vibaya vilitokea katika nchi.

Waganga walijidai kujua mzunguko wa jua na mwezi. Walitoka nje usiku na kuangalia rangi yake. Kama ulikuwa na rangi nyekundu katika mawingu yaliyouzunguka, walihesabu vitu vingi vilivyotokea mwaka ule. Kama mwezi ulikuwa na rangi nyeupe tu, hii ilikuwa dalili nzuri. Waganga hawa walikuwa wamejifunza kuwa mwezi ulikuwa na rangi fulani saa fulani usiku. Saa zile zilipofika waliwaambia watu waende kutazama mwezi. Walipoona kuwa mwezi ulikuwa na rangi zile walizosema waliamini kuwa waganga walisema kweli.

Wakati “mangi” fulani alipotaka kwenda kupigana na "mangi" mwingine, alimwita mganga na kumwuliza kama watu wake watashindwa au hapana. Kama alisema watashinda "mangi" alimwuliza siku nzuri ya mapigano. Baada ya kutafuta sababu nyingi za kupendelea siku fulani kwa kuanza kupigana mganga alikwenda kwa "mangi" na ku- mwambia siku yenyewe, na siku ile ile vita ilianza.

Waganga walitunga maarifa mengi ya hila ambayo karibu yote yalikuwa ya kujipatia chakula na mali kutoka kwa watu. Kama mbuzi ilichinjwa kwa tambiko, lile tambiko halikutokea vema kama watu wa nyumba ya yule mtu aliyetambikiwa walikula nyama ya yule mbuzi. Nyama karibu zote zilichukuliwa na yule mganga. Watu waliamini kuwa ikiwa mganga hakupewa ujira wake wa kutosha hata kama alitengeneza tambiko la mtu, tambiko lile halikutokea; kwa sababu hii mganga alipewa hata zaidi ya ujira wake ili afurahiwe na kufanya kazi yake vizuri.

Watu maskini katika nchi hawakuweza kulipa ujira wa waganga ijapokuwa walijua iliwabidi kufanya hivyo ili taabu zao ziishe, iliwalazimu kukopa mbuzi na kondoo na kuwalipa waganga. Madeni haya yalizidi hata mwishowe walishindwa kuyalipa. Umaskini siku zile ulikuwa kitu kibaya kwa watu ambao hawakuweza kujisaidia. Watu hawa hawakupenda kuwa maskini bali maisha yao yaliwafanya hivyo. Wachawi waliroga watu na walikuwa na maarifa mengi ya udanganyifu mtupu. Hawakupewa heshima yo yote katika nchi, na walipopatikana kama wanaroga watu walishtakiwa na kuteswa sana hata kuuawa. Makusudi ya wachawi yalikuwa mabaya kwa sababu walitaka kuwaua watu na Wachawi walikuwa na madawa yaliyowekwa katika vibuyu na pembe. Waliwadanganya watu kuwa madawa haya yaliweza kuponya magonjwa. Walipowatibu watu walipigapiga vibuyu na pembe na kuwaambia watu kuwa madawa yaliweza kuponya magonjwa yao. Walipowatibu na kusema hivyo walitazama mbinguni na kutema mate, na huu ulikuwa udanganyifu mtupu.

Wachawi walizika vitu walivyopaka madawa karibu na nyumba za watu. Watu walisadiki vitu hivi viliweza kuwaletea magonjwa. Ilisadikiwa kuwa hakuna mtu aliyeweza kutibu magonjwa yaliyoletwa na vitu vile isipokuwa wachawi. Mara wachawi waliitwa na kuondoa vitu vile, na baada ya kazi yao wakapewa mbuzi au kondoo. Wakati mwingine kama mchawi alimchukia mtu au mwanamke fulani, alimnyemelea usiku na kumzikia vitu vya madawa chini ya kitanda chake.

Maisha ya Wachagga yalitawaliwa na nguvu za waganga ambao waliwatendea mema na walipewa heshima. Lakini wachawi walikuwa watenda maovu na walilaaniwa. Maisha yalikuwa ya taabu kwa mambo haya, na Wachagga wengi waliona kuwa ni nguvu za ajabu ambazo hawakuwa nazo.
 
Back
Top Bottom