Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Nimebahatika kuwajua wazalendo hawa watatu ambao nimeandika historia zao katika TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.
Tewa Said Tewa mbali ya kuwa waziri katika serikali ya Tanganyika baada ya uhuru mwaka wa 1961 alikuwa pia ni Rais kwa upande wa Tanganyika wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) Umoja wa Waislam wa Afrika ya Mashariki nafasi ambayo ilimsababishia matatizo makubwa kiasi cha kupelekea kupoteza uongozi katika serikali na EAMWS kupigwa marufuku Tanzania mwaka wa 1968.
Kwa kinywa chake Tewa Said Tewa alinieleza maisha yake yote kuanzia wakati wa TAA hadi kuwa mmoja wa watu 17 walioasisi TANU mwaka wa 1954.
Sheikh Rashid Sembe ataingia katika historia ya uhuru wa Tanganyika kama shujaa wa Azimio la Tabora la mwaka wa 1958 pale TANU katika mkutano wake wa mwaka Tabora, ulipoamua kuingia katika Kura Tatu jambo ambalo lilitishia TANU kugawika katika makundi mawili, lile la Rais wa TANU Mwalimu Julius Nyerere aliyetaka TANU ishiriki uchaguzi na lile la Sheikh Suleiman Takadir Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU aliyekuwa akiongoza kambi ya upinzani wa Kura Tatu ndani ya chama.
Sheikh Rashid Sembe ni katika waasisi wa TANU Tanga mwaka wa 1955.
Sheikh Sembe ni kati ya wanachama wa TANU Tanga ambao wakiongozwa na Mwalimu Nyerere na Amos Kisenge kutoka Makao Makuu, New Street Dar es Salaam waliweka mkakati maalum wa kuwashinda wapinzani wa Kura Tatu katika mkutano wa siri uliofanyika Tanga mjini na kufuatiwa na dua makhsusi Mnyanjani kuomba Mungu aivushe TANU katika mtihani ule.
Nilibahatika kuisikia historia hii ambayo hadi siku ile haikupatwa kuelezwa popote kutoka kinywa cha mwenyewe muhusika mkuu Sheikh Rashid Sembe nikiwa nimekaa kwenye sebule ya nyumba yake Barabara ya 14 Tanga.
Zuberi Mtemvu ni baba yangu.
Kila tulipokaa mazungumzo yetu yalikuwa historia ya TANU na alinisomesha mengi hasa jinsi alivyokasirishwa na TANU kupiga kura Tabora mwaka 1958 kukubali kuingia katika Uchaguzi wa Kura Tatu, uchaguzi uliomlazimisha mpiga kura kumpigia kura Mzungu, Muasia na Mwafrika.
Kwa ajili hii Zuberi Mtemvu alitoka TANU na kuunda chama chake African National Congress (ANC) maarufu kikijulikana kama Congress akiwa na Said Chamwenyewe ambae kama Mtemvu walikuwa wanachama shupavu wa TANU Chamwenyewe akiwa pia katika Baraza la Wazee wa TANU.
Kuanzia mwaka wa 1958 Zuberi Mtemvu na Julius Nyerere walinuniana na hawakusema maisha.
Kitabu hiki kinapatikana Ibn Hazm Media Centre Msikiti wa Mtoro, Manyema na Mtambani kwa bei ya shs: 2000 tu.